loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hili la kuchezea afya za watu lisifanyiwe masihara

Uamuzi wa Serikali kuifungia kwa muda usiojulikana Hospitali ya Chuo cha Kimataifa cha Matibabu na Teknolojia (IMTU), kinachohusishwa na utupaji wa viungo vya binadamu mithili ya takataka, ikielezwa kina mapungufu kadhaa yanayohusu uendeshaji wa hospitali.

Yametajwa baadhi kuwa ni kutokuwa na wauguzi wa kutosha, kutokuwa na vifaa vya kutosha ikiwemo kifaa cha kuchomea taka ngumu, kuchanganya dawa zilizokwisha muda na ambazo hazijaisha muda wake na pia wauguzi kufanya kazi ambazo si zao, ili mradi tu kila kitu kionekane kinakwenda sawa.

Lakini kabla haya hayajaisha, gazeti hili lina habari nyingine inayoeleza Serikali mkoani Rukwa imekataa kukitambua chuo cha tiba Rukwa College of Health and Allied Sciences kikielezwa kinaendeshwa kienyeji, kwani hakina kibali cha wizara husika kinachosiruhusu kufundisha, lakini mitaala yake imedaiwa kuwa imepitwa na wakati na hapo kabisa kwenye muundo wa sasa wa wizara.

Na katika kuthibitisha kuwa kimekerwa na uendeshaji wa chuo hicho, idara ya afya mkoani Rukwa imewapiga marufuku wanachuo wake kwenda Hospitali ya Mkoa na nyingine mkoani humo kwa mafunzo ya vitendo.

Kwa ujumla, tunapongeza uamuzi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wa kuifungia hospitali yenye dosari za kiutendaji ya IMTU, lakini pia mkoa wa Rukwa kwa uthubutu wa kutokifumbia macho chuo kinachoonekana kutokidhi kutoa taaluma nyeti kama ya afya ya mwanadamu.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk John Gurisha amekaririwa akisema atahakikisha chuo hicho na vingine vinafuata taratibu, badala ya kuwa sehemu ya kupika watu watakaochezea maisha na afya za watu badala ya kuwaponya.

Kwa ujumla, haya yaliyojitokeza IMTU na mkoani Rukwa, yanaonesha jinsi afya za Watanzania zilivyo hatarini, zaidi zikichezewa na watu walioaminiwa kuwa wangekuwa waangalizi wa afya za Watanzania kutokana na kuwa wanataaluma katika sekta ya afya.

Na afya za Watanzania zinaingia majaribuni kutokana na kile kinachoweza kuelezwa kuwa ni uzembe wa watendaji katika wizara ya afya waliopaswa kusimama kidete kuhakikisha kila kitu katika sekta ya afya kinakwenda sawa.

Lakini haiingii akilini kuona hospitali kama IMTU iliyopo chini ya maili 10 tu kutoka makao makuu ya wizara, inafanya madudu ya kutisha kama ya kuchanganyia wagonjwa dawa zilizokwisha muda wake.

Watendaji wa wizara wangekuwa makini, wala tusingefika huku. Tushukuru tu kwamba kubainika kwa utupaji holela wa viungo vya binadamu ndiko kulikobaini haya, vinginevyo, bila shaka wagonjwa wangeendelea kuchezewa kwa kupewa dawa zisizostahili kwa matumizi ya binadamu.

Kama haya yanatokea katika hospitali kubwa kama IMTU, hali ikoje katika hospitali nyingine na vituo vya afya kote nchini?

Kuna mengi ya kujiuliza, lakini ifike mahali watendaji katika wizara watimize wajibu wao ili wanataaluma wake wafanye kazi kwa kufuata misingi halisi ya sekta husika, badala ya kugeuza afya za Watanzania mtaji wa kujinufaisha kiuchumi, lakini bila kujali athari zaidi zitakazowakumba watanzania wenzao.

Ndiyo maana tunasema, kwa hili la kuchezea afya za Watanzania, hakika lisifumbiwe macho.

RIPOTI ya 15 kuhusu uchumi wa Tanzania ya ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi