loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hili la wanafunzi kuoa wake watatu tusilikubali

Habari hii haikuwa hadithi ya kufikirika bali ni hali halisi inayotokea katika wilayani zetu mbili za Kalambo na Sumbawanga mkoani Rukwa.

Ukweli kuhusu vitendo hivyo ulibainika wakati wa kikao cha siku moja cha wadau wa elimu kilichowakutanisha Waratibu Elimu Kata na Maofisa Elimu wa wilaya hizo mbili.

Kikao hicho kilifanyika chini ya asasi isiyo ya kiserikali ya TMEP kupitia Mradi wake wa Afya ya Uzazi na Jinsia unaotekelezwa mkoani Rukwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Resource Oriented Development Initiative (RODI).

Ilielezwa kuwa sababu kubwa ya kuwepo kwa hali hiyo ni mwamko mdogo wa elimu kwa upande wa wazazi na walezi kiasi cha kuwaozesha watoto wao mara tu wanapoingia Kidato cha Kwanza.

Ilidaiwa kuwa hatua hiyo hufuatiwa na ile ya kuwaacha wake zao kwenye vijiji wanavyotoka na kisha wao kwenda shuleni na baadaye kulazimika kukatiza masomo na kurejea nyumbani mara kwa mara ili kuwajibika kwa familia zao.

Taarifa hizo za ndani ya kikao hicho pia zilifafanua kwamba kati ya watoto 80 wanaojiunga Kidato cha Kwanza ni wanafunzi 30 tu ndiyo hufanikiwa kuhitimu Kidato cha Nne.

Pamoja na sababu zilizotolewa, tunapenda kueleza wazi kwamba tabia hii si nzuri na kwa kweli vitendo kama hivi havipaswi kuachwa kuendelea kufanywa na wazazi, walezi na hata wanafunzi wenyewe.

Kwa kuruhusu wanafunzi kuoa katika umri mdogo tena idadi kubwa namna hiyo ya wake inawanyima watoto wetu ufunguo bora wa maisha yao ya baadaye pamoja na kulinyima Taifa nguvu kazi ya wataalamu katika nyanja mbalimbali siku za usoni.

Ni kutokana na ukubwa wa suala hili, tunawashauri viongozi wa ngazi zote katika wilaya hizo mbili wakiwemo wa serikali, kisiasa na hata wananchi kwa ujumla wao wakatae hali hii kuendelea kuota mizizi kwani inarudisha nyuma vita dhidi ya ujinga, maradhi na umasikini aliyoanzishwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere baada ya kupata Uhuru Desemba 9, 1961.

Swali la kujiuliza ni je, mwanafunzi mwenye majukumu ya kuwa na wake hadi watatu anawezaje kufuatilia masomo yake darasani na kufanya vizuri?

Tunajiuliza inakuwaje wazazi na walezi wanashindwa kuwaelekeza wanafunzi hao kwamba masuala ya kuoa au kuolewa yanaweza kusubiri hadi watakapokuwa kwanza watu wazima na pia hadi hapo watakapohitimu elimu yao ambayo ndiyo ufunguo wa maisha?

Ni lazima hatua za makusudi zichukuliwe dhidi ya wazazi, walezi na hata wanafunzi wenyewe kwa vitendo hivyo za kufifisha juhudi za serikali za kuwapatia wananchi wake elimu bora kwa kadiri inayvowezekana ili waweze kupambana na maisha ya baadaye ipasavyo.

Kampeni ya makusudi pia ya kuwahamasisha wazazi na walezi juu ya umuhimu wa elimu inapaswa pia ifanywe katika maeneo haya ili kutafuta suluhisho la kudumu la tatizo hilo.

Tunaamini kwamba kama hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika katika suala hili la kufifisha elimu, kutakuwa na uwezekano mkubwa wa kulikomesha jambo hili kwa sababu watakaochukuliwa hatua za kisheria watapewa adhabu wanayostahiki kwa kosa hilo na hivyo kuwa funzo kwa watu wengine kuachana na tabia hii isiyovumilika.

Hili linawezekana na sote tushikamane katika kulikataa hususan kwa wenzetu wa Mkoa wa Rukwa ambao wana wajibu wa kuikabili hali hiyo kwa umuhimu unaostahili.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi