loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hongera JK, Chadema kwa kukuza demokrasia

Jengo hilo limegharimu jumla ya Sh bilioni 1.4 ambapo halmashauri yenyewe imechangia Sh milioni 18 za ujenzi huku fedha zilizobaki zikitolewa na Serikali.

Kitendo kilichotokea katika hafla hiyo ni kitendo ambacho kamwe hakiwezi kupita bila kupongezwa kwa sababu kilionesha namna muundo wa vyama vingi vya siasa tulioukubali kwa hiari yetu mwaka 1992 unavyoanza kujiimarisha na kukubalika na pande zote za wadau yaani chama tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM), vyama vya upinzani na serikali.

Halmashauri ya Wilaya ya Karatu inaongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambapo viongozi wake watatu; Mwenyekiti wa Wilaya, Lazaro Massey na wabunge wawili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Cecilia Paleso (Viti Maalumu) na Israel Natse (Karatu) kwa nyakati tofauti walimpongeza Rais Kikwete kwa kuunga mkono kwa vitendo juhudi za wananchi wa wilaya hiyo kujiletea maendeleo bila kujali itikadi za vyama.

Lakini pia kwa upande wake, Rais Kikwete alisema ‘’Katika kusambaza maendeleo sisi hatuwezi kubagua. Hiyo ndiyo demokrasia na Serikali yetu inaheshimu sana demokrasia na misingi ya utawala bora.’’ Tunachojifunza juu ya tukio hilo zima ni kwamba inapokuja suala la kuwaletea maendeleo wananchi, sote kama Watanzania hatuna budi kushirikiana kwa hali na mali bila kujali itikadi za vyama vyetu, rangi zetu, makabila yetu au dini zetu ili kuleta maendeleo katika jamii na nchi yetu kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi kwa lengo la kuimarisha ustawi na maisha bora ya watu wetu.

Viongozi wa Chadema wametoa funzo lingine katika tukio hili ambalo liko wazi kabisa kwamba si kila jambo linalofanywa na serikali iliyopo madarakani linastahili kubezwa bali pale panapostahili kupongezwa hatuna budi kufanya hivyo.

Tanzania hivi sasa ina zaidi ya vyama 19 vya siasa vilivyosajiliwa Miongoni mwa vyama hivyo ambavyo vina wabunge na madiwani ukiacha hivi viwili vya CCM na Chadema ni pamoja na CUF, UDP na TLP.

Ni ukweli kwamba kwa wakati mmoja ni chama kimoja tu ndicho kinaweza kuongoza serikali kwa mujibu wa Katiba ya sasa na hivyo tukiachia malumbano ya hoja wakati wa kampeni za uchaguzi, akishapatikana mshindi sote tushirikiane katika kujiletea maendeleo na kuendeleza vita dhidi ya magonjwa, maradhi na umasikini.

Tunapenda kuipongeza hatua hii iliyofikiwa na kutoa mwito kwa vyama vyote vya siasa kuendeleza ushirikiano wa aina hii kwa manufaa ya wananchi wetu wote.

Mambo yanayoashiria kututenga au kututumbukiza katika chuki, uhasama, upotevu wa amani na utulivu wetu kamwe yasipewe nafasi ili kuhakikisha kwamba moyo huu wa kuendeleza demokrasia ya kweli na ya kiustaarabu haivurugwi na watu wachache wenye nia mbaya na taifa letu.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi