loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Huruma yageuka shubiri

Niwakumbushe pia kwamba kutokana na maadili ya kitaaluma sitaweza kuwataja wahusika, lakini naamini yaliyomo kwenye vituko hivyo ni muhimu kuyafahamu kwa minajili ya kupata funzo na tahadhari.

Ilikuwa ni jioni moja katika moja ya vilinge vya burudani hapa jijini Dar es Salaam nilipokuwa na rafiki yangu wa siku nyingi tukibadilishana mawazo baada ya kazi za kutwa nzima. Rafiki yangu huyo alianza kunisimulia yaliyomkuta katika jiji la Arusha mwezi uliopita akiwa katika safari ya kikazi.

Hoteli aliyofikia ilikuwa na eneo la wazi la kupata nyama choma kama ilivyo katika hoteli nyingine jijini Arusha.

Katika harakati hizo alisema alijitokeza dada mmoja aliyemwomba kinywaji na kisha kuketi naye kubadilishana mawazo jioni hiyo. Kwa mujibu wa rafiki yangu mazungumzo yalikolea hadi majira ya saa 3.30 usiku ambapo rafiki yangu alimuaga yule dada kwenda kujipumzisha.

Alisema alikuwa hana mpango wowote naye baada ya mazungumzo na vinywaji.

Kwa mujibu wa rafiki yangu, siku iliyofuata alikuwa anaondoka alfajiri kuwahi ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), lakini wakati anatoka kwenye hoteli hiyo kuelekea kwenye gari, ghafla alishuhudia yule dada aliyekuwa naye kwenye vinywaji jana yake jioni, akijitokeza ghafla na kumvamia huku akipiga kelele nipe changu kabla hujaondoka, tena kwa sauti kubwa.

Wakati akiwa bado haamini kilichokuwa kinatokea yule dada aliendelea kupaza sauti, lakini kilichomwokoa ni kwamba walinzi wa hoteli walimkamata dada husika na kubaini hila aliyokuwa nayo, hivyo kumdhibiti na kumtimua maeneo hayo.

Jasho lilimtoka kwa huruma yake tu kwa dada huyo. Kukosa alichotafuta ndicho kilichomfanya amtege ili ajipatie kipato kwa hila.

Lakini kisa kingine kilichofanana na hicho kilitokea Dar es Salaam na kwa bahati mbaya ni rafiki yangu huyo huyo wakati anasimulia kisa hicho kwa wafanyakazi wenzake ofisini, naye akapewa kisa kingine.

Baba mmoja aliyekuwa na umri wa makamo alikuwa katika gari yake akitoka katikati ya jiji la Dar es Salaam kwenda kwake Bunju, njia ya kuelekea Bagamoyo.

Ilikuwa ni majira ya saa 3.00 usiku. Alipofika maeneo ya Mwenge huku akiwa anasotea foleni alijitokeza dada mmoja aliyekuwa amevaa sura ya huzuni na kukata tamaa kwa kusotea usafiri wa kwenda Tegeta. Baba wa watu alikubali ombi lake la kutaka ampatie lifti hadi Tegeta alikokuwa anaelekea yule dada.

Bila kusita mzee wa watu alikubali kumpatia lifti. Lakini alipofika maeneo ya Tegeta yule dada aliomba kushuka na kwa mshangao wake aliposimamisha gari tu yule dada badala ya kushuka, akaanza kupiga kelele huku akisema kwa sauti 'nipe kilicho changu, hapa hatoki mtu'.

Vurugu zikaanza ndani ya gari na watu kujitokeza kujua kulikoni. Kwa mujibu wa msimulizi wangu, inaelekea yule dada aliandaa wapigapicha kwani walikuwepo eneo hilo.

Baba wa watu alilazimishwa kutoa Sh 200,000 kwa kuhofia kwamba huenda picha walizokuwa wanampiga zingeweza kutumika katika mitandao au magazeti ya udaku. Huruma yake imemponza.

Matukio hayo mawili yanatokea na huenda yataendelea kutokea katika jamii yetu, lakini la msingi hapa ni lazima tuwe makini, hasa kwa kina baba. Matukio yote mawili yamefanywa kwa mitego iliyopangwa kwa umakini na binti zetu.

Ni vizuri tukawa makini katika mahusiano au kuwa na ukarimu kwa watu ambao hatuwajui. Si ujinga kujiuliza mara mbilimbili katika suala zima la kumpatia mtu msaada. Huruma zao ndizo zilizowaponza.

Waziri Mkuu Mstaafu, ...

foto
Mwandishi: Nicodemus Ikonko

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi