loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

IDDI MARODA: Mzee aliyepigana vita ya pili ya dunia

Hivi karibuni nilipata fursa ya kukutana na Mzee Iddi Maroda ambaye alizaliwa wakati nchi inatawaliwa na Wajerumani na baadaye Waingereza na kupata kufanya kazi mbalimbali kwa Wazungu na Wahindi na pia kukutana na changamoto mbalimbali katika kazi ya utafutaji wa kipato.

Anasema alizaliwa mahali ambapo kwa sasa ipo stendi ya mabasi Mjini Shinyanga, lakini wakati huo kulikuwa ni vichaka na nyumba chache za wenyeji zilizojengwa kwa nyasi na kuezekwa kwa udongo. Hata hivyo, kwa sasa Mzee huyu anaishi kwa mwanawe ambaye ni mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Buzuka.

Mzee Maroda ni mcheshi na mtu anayependa utani lakini kama humfahamu vizuri unaweza ukaogopa hata kumuuliza swali ukidhani ni mkali ama mtu asiyependa kuongea.Nilipofika kwake na kuwaambia: “Mzee Maroda, leo nimekutembelea na nina maswali kadhaa ya kukuuliza kuhusu hostoria ya maisha yako na nchi yetu kwa ujumla,” yeye, baada ya kunikaribisha, akanijibu: “Lakini sitaki kuulizwa yale ambayo sijayaona bali uulize niliyoyaona.”

Alinijibu hivyo akiwa hacheki mithili ya mtu aliyechukizwa na kumbe alikuwa ananiangalia kuona kama mimi ni mvumilivu ninapoongea na watu wa aina mbalimbali ama la. Mzee huyu anasema alizaliwa mwaka 1918 (Sawa na Hayati Nelson Mandela) wakati vita ya kwanza ya dunia inamalizika lakini hakumbuki mwezi na tarehe.

Anasema alizaliwa nyumbani kupitia wakunga wa jadi na kwamba jina Shinyanga halikuwepo wakati huo isipokuwa mji ambao leo unaitwa jina hilo ulijulikana kwa jina la Beda, likimaanisha nchi ya Chief Kudulilwa. Anasema alipokuwa kijana alishiriki mengi, ikiwa ni pamoja na harakati za kuwaondoa wakoloni.

Anasema alipigana vita vya pili vya dunia vya mwaka 1939 hadi mwaka 1945 na kwamba aliwahi pia kuwa mwanachama wa chama cha TAA. Anasema wakati chama cha Tanganyika African National Union (Tanu) kilipoanzishwa mwaka 1954 alijiunga nacho na kwamba alishiriki pia kuuza kadi za chama hicho kwa siri kwa kuwa kilikuwa kinapigwa vita na watawala wa kikiloni.

Anasema kingine alichoshuhudia machoni mwake ni kuanzishwa kwa mgodi wa almasi wa Williamson pale Mwadui, wilayani Kishapu. “Kwa hiyo baadhi ya mambo niliyoshuhudia ni namna jina la Shinyanga lilivyopatikana, mgodi wa almasi wa Williamson ulivyoanza, chama cha Tanu kuzaliwa mpaka kumng’oa mkoloni na kuipandisha bendera ya Tanu... Nilishiriki katika mapigano ya vita vya pili vya dunia ambapo nilichukuliwa na wazungu na kwenda nchini Italia,” anasema.

Kupatikana jina la Shinyanga

Mzee Maroda anasema mkoa wa Shinyanga zamani ulikuwa unajulikana kwa jina la Beda. Wakati huo, Wazungu wakitawala nchi, kulikuwa hakuna usafiri wa uhakika kutoka eneo moja kwenda jingine kama ilivyo sasa bali watu walilazimika kutembea kwa miguu.

Anasema Wazungu walipotaka kusafiri kuna wakati waafrika walikuwa wanalazimika kuwabeba kwenye machela, na hasa kuwatoa mkoani Tabora mpaka Shinyanga.

“Walikuwa wanawabeba kwa kupokezana kutoka uchifu mmoja mpaka mwingine. Yaani waafrika walikuwa wakikusanyika kwa chifu fulani na hivyo wazungu wakawa wanawatumia machifu hao katika kila kituo kupata watu wa kuwabeba. Mzee Maroda anasema eneo la Shinyanga mjini lilikuwa chini ya mtawala aliyeitwa Chifu wa Beda na kule Old Shinyanga kulikuwa na mtawala mwingine aliyeitwa Chifu Tinde.

“Kwa hiyo utaona Wazungu walipokuwa wakihitaji watu wa kuwabeba katika machela lazima wapitie kwa machifu mahali ambapo kuna mkusanyiko wa watu,” anasema.

Anasema siku moja mzungu mmoja alikuwa amebebwa katika machela na muda mwingi alikuwa kasinzia. Yeye na msafara wake walipofika eneo ambalo leo linaitwa Old-Shinyanga kulikokuwa na kambi yake akashituka usingizini na kuuliza hapa ni wapi baada ya kuona miti aina ya mibono mingi ambayo kwa kabila la Kisukuma inaitwa manyanga.

“Kwa hiyo waliokuwa wamembeba wakasema kwa kilugha kuwa miti hiyo ni Manyanga. Kwa hiyo mzungu alipotaka kurudia kutamka neno ‘manyanga’ akasema Shinyanga na kuwachekesha wabebaji wake ambao waliendelea kulitumia kama mzaha hadi likazoeleka na hasa kwa vile mzungu huyo alihamishia kambi yake kutoka mahala ambapo leo panaitwa Old Shinyanga na kuisogeza eneo lililokuwa na mibono na kusema “kuanzia leo hii nitakuwa hapa Shinyanga, akimaanisha kwenye miti ya manyanga.”

Anasema baadaye ililetwa gari moja ya mtawala (DC) ambayo ilikuwa inazunguka mkoa mzima na kwa vile ilikuwa ni gari ya kwanza kabisa kufika mkoani humo ilikuwa ikiwashangaza watu wengi. Anasema gari hiyo aina ya Bedford ilikuwa ya wazi. Anasema gari hiyo ilitumiwa na ma-DC kutoa taarifa kwa wakuu wa mikoa (PC) ambapo mkoa wa Shinyanga ulikuwa ukitoa taarifa zake jijini Mwanza kwani ulikuwa ni sehemu ya mkoa huo.

Mkoa wa Mwanza ulijumuisha pia ile ambayo kwa sasa inajulikana kama mikoa ya Kagera, Mara, Shinyanga na Tabora. Anasimulia kwamba wakati reli ya kati inaanza kujengwa pale Old Shinyanga ndio yalikuwa makao makuu ya mtawala (DC), na baadaye makao ya DC yakahamishwa na kusogezwa yalipo hivi sasa na kukawa mji na watu wakauzoea hadi leo.

Elimu kipindi cha ukoloni

Mzee Maroda anasema kwa upande wake yeye hakubahatika kupata elimu yoyote kwa maana kwamba hakusoma. Anafafanua kwamba kipindi anazaliwa na kuikuta nchi ikitawaliwa na Mjerumani, mkoa mzima wa Shinyanga kulikuwa na shule moja katika eneo la Old Shinyanga.

Alipoingia Mwingereza (baada ya vita kuu ya dunia ya pili), alianzisha ujenzi wa shule katika sehemu wanazoishi machifu pekee ambapo watoto walisoma kuanzia darasa la kwanza mpaka la nne.

Anasimulia kwamba utawala wa Mwingereza ulijenga shule nyingine ya juu katika eneo la Ibadakuli na mtoto anapofaulu yale madarasa manne sasa aliweza kuendelea mpaka darasa la nane na akifaulu darasa la nane alikuwa anapelekwa mkoani Tabora kwa masomo ya juu zaidi.

Kupigana vita ya pili ya dunia

Mzee Maroda anasema alikuwa ni miongoni mwa vijana waliopigana vita vya pili vya dunia mwaka 1939-45. Anasimulia kwamba yeye alichukuliwa kama kijana shupavu akitokea nchi za Afrika kwenda nchini Ita- lia am- bapo wali- fikishiwa porini kwenye mapigano.

Anasema alichokishangaa huko ni kuona hata nyama ya binadamu ikiliwa kwa sababu ilifikia wakati watu wanakosa maji na chakula. Anasema watu wengi walikufa kwa njaa na hivyo kilichokuwa kikifanyika ni wale waliokuwa wamekufa wanachunwa ngozi na kubanikwa kisha kuliwa kama chakula huku mapigano yakiendelea.

Anasema wapiganaji waliweza kuishi porini kwa muda wa wiki mbili wakipigana huku kukiwa hakuna chakula wala matunda. Anasema nyoka akionekana aliuliwa na nyama yake kuchomwa na kuliwa pia.

Bila kueleza kama naye alilazimika kula nyama ya binadamu ama la, Mzee Maroda anasema: “Wakati wa vita lilikuwa jambo la hatari sana. Watu walikuwa wanakufa hovyo. Namshukuru Mungu kwamba mimi mpaka leo hii niko hai na salama.”

Anasema alichukuliwa kwenda vitani wakati mapigano hayo yakiwa tayari yameanza na hii ni kutokea mwaka 1943 mpaka 1945. Baada ya kutoka Italia akiwa salama, mwaka 1946, Mzee Maroda anasema aliamua kuoa mke na kuishi naye.

Kuingia kwenye siasa

Anasema mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Abdallah Kandoro, aliyekuwa ni mwenyekiti wa chama cha Tanganyika African Association (TAA) kilichoanzishwa mwaka 1929 alipita pale Shinyanga akitokea mkoa wa Kagera akisambaza kadi za chama hicho na ndipo naye alipoamua kujiunga nacho.

Lakini kwa bahati mbaya anasema, Chifu wa Ibadakuli, Kidaha Makwaya, alikuwa akikipinga chama cha TAA na kuungana na wazungu kwa kuwa ndiye walimfanya kuwa mkuu wa machifu wote katika mkoa wa Shinyanga tangu ukijulikana kama Beda.

Anasema wao waliendelea kuwa wanachama wa TAA kwa sababu kilikuwa kinajali maslahi ya waafrika licha ya kupigwa sana vita na wazungu na baadaye wakasikia fununu kwamba kuna chama cha Tanu kimeanzishwa. Hii ilikuwa mwaka 1954.

Anasema baadaye ofisi ya Tanu ilianzishwa Mwanza wakati huo yeye alikuwa amekwenda kutafuta maisha Geita katika eneo lililofahamika kwa jina la Sima ambako ndiko alikojiunga na Tanu. Anasema alichukua kadi kadhaa za chama hicho akawa anaziuza kwa siri kwa kuwa wakoloni na vibaraka wao walikuwa hawakipendi chama hicho.

Anasema mwaka 1958 aliuza kadi nyingi sana kwa kujificha lakini siku moja mwaka huo huo wenzake aliokuwa nao karibu walimtaja kwenye serikali ya wakoloni, akakamatwa na kutupwa gerezani alikosota kwa muda wa mwezi mmoja. Anasema alitoka ndani baada ya Mwasisi wa Tanu, Mwalimu Julius Nyerere kupata taarifa kuwa kuna watu wamekamatwa na kufuatilia na ndipo wakaachiwa huru.

Anasema baada ya kuachiwa huru aliendelea kuuza kadi na kukiunga mkono chama cha TANU na mwaka 1960 alipewa madaraka ya kuwa mwenyekiti katika tawi la Sima mkoani Geita. “Sasa masuala ya kukamatwa kamatwa na serikali ya wakoloni yalianza kupungua na hata mikutano ya hadhara ilianza kufanyika mchana badala ya usiku kama ilivyozoeleka kwa kuogopa serikali ya wakoloni,” anasema.

“Siku ya nchi yetu ilipopata uhuru mwaka 1961 nilitokea Geita kuelekea Mwanza huku nikiwa na msafara wa magari matatu niliyokuwa nimepewa na waarabu kuandamana nayo baada ya kuwa wamekikubali chama cha Tanu. Siku hiyo tulikuwa na furaha kupindukia. Tulikesha tukifurahi kwa kupandish bendera ya Tanu na kushusha ya mkoloni,” anasema Maroda.

Anasema baadaye alijiuzulu nafasi ya uenyekiti na kuwa askari wa Tanu. Anasema alipata madaraka makubwa kutokana na kuelewa mambo mengi ya kiaskari kutokana na uzoefu alioupata vitani.

Kazi zilizompa riziki

Anasema mwaka 1948 alianza kazi za vibarua kwa wahindi na baadaye wakampa kazi ya ukaguzi wa zao la pamba pale wanapolinunua kutoka kwa wakulima. Anasema kazi hiyo ilimfikisha mpaka nchini Uganda alikoishi kwa muda wa miaka sita. Anasema kazi hiyo ilimpatia mshahara ambao wakati huo aliuona ni mkubwa wa shilingi 40 kwa mwezi.

“Nilishirikiana nao kujenga jineri ya kuchambulia pamba mkoani Geita ya Kasamwa. Kwa kweli Wahindi walinifurahia sana na kuniongeza mshahara hadi kufikia shilingi 50, kwa mwezi,” anasema.

Anazidi kusema: “Nilipopelekwa nchini Uganda, nilikuwa napokea mshahara wa shilingi 200, tofauti na nilivyokuwa huku Tanzania. Mshahara wangu huo ‘mkubwa’ ulipotoka, kwa mara ya kwanza nikanunua baiskeli aina ya BS. Mimi pia nilijihusisha na kilimo cha pamba,” anasema Maroda.

Mgodi wa Williamson kuanzishwa

Mzee Maroda anasema mwaka 1936 alikuja mzungu mmoja aliyefahamika kwa jina la Mecky ili kuchimba madini ya almasi eneo la Kizumbi, Shinyanga ambapo naye alienda kuomba kazi ya kuchekecha mchanga uliokuwa ukitoka katika mashimo. Anasema alikubaliwa na akijiunga na vijana wenzake, wakati huo wakilipwa ujira wa senti 20 mpaka senti 30 kwa mwezi.

“Huyu Williamson alikuwa mtumishi wa Mecky. Wakati huo kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la James Nkida alikuwa rafiki sana wa Williamson. “Siku moja, Nkida aliomba ruhusa kwenda kuwasalimia wakwe zake. Alipofika eneo la Mwadui akabanwa haja kubwa na kwenda kujisaidia kwenye kichaka. Ndipo akaona jiwe linalofanana na haya yaliyokuwa yanapatikana kwenye mgodi wa Kizumbi kwa mzungu Mecky. Akaamua kulichukua na kuweka mfukoni kisha kuondoka nalo,” anasema.

Mzee Maroda anazidi kusimulia kwamba alipofika ofisini alimwita rafiki yake, Williamson na kumtaka aliangalie jiwe hilo alilonalo kama linafanana na hayo wanayoyapata hapo Kizumbi. “Kwa uzoefu wa kulitazama likaonekana kufanana na ndipo akamwambia ni lenyewe ila usimwambie mtu mwingine na twende ukanioneshe mahali ulipoliokota jiwe hili,” anasema.

Siku iliyofuata anasema waliongozana kwa kutembea kwa miguu kutoka Kizumbi mpaka eneo alikoliokota jiwe hilo ambapo ni Mwadui, mahala uliko mgodi wa almasi sasa.

“Pale Mwadui wakakuta mawe ya aina hiyo ni mengi ila wazee wa kabila la Kisukuma walikuwa wakiyaona na kuyaita jina la Mbura huku wakiwa hawafahamu umuhimu wake,” anasema na kuongeza kwamba mawe hayo pia Wasukuma walikuwa wakiyatumia kuchezea bao.

Anasema baadaye Nkida na Williamson wakaamua kuanza kuchimba kwa kutumia jembe na kila wakichimba wanaona kinachotoka hawakijui kwa sababu walikuwa hawana vifaa. Anasema waliamua kwenda kwenye duka la Mhindi mmoja kukopa vifaa vya kuchimbia huku wakipata vibarua sita wa kuwasaidia.

“Hatimaye waliacha kazi kwa mzungu Mecky na kuhamia Mwadui na baadhi ya vibarua. Williamson alianza kuuza almasi aliyokuwa akiipata Mwadui katika mgodi mwingine uliokuwa Geita na sehemu zingine. Hatimaye akaenda nje ya nchi kutafuta zana za kuchimbia. Mara mgodi ukawa maarufu. “Niliacha kazi Kizumbi nikajiunga na Williamson ambapo alikuwa akinipa mshahara wa shilingi saba. Tulikuwa naye wote kule Kizumbi tukiwa tumeajiriwa sehemu moja lakini mwenzetu mara akatajirika kwa njia hiyo,” anasema Maroda.

Anasema hata mzungu Mecky naye hakuanzia moja kwa moja kuchimba madini Kizumbi, bali alitokea katika mchimbo ya dhahabu ya Geita ambapo wote kwa pamoja walianza kupeleka almasi walizokuwa wakizipata katika migodi waliyoibua kwenye mgodi mkubwa wa Geita.

“Ila mgodi wa Williamson ulipata umaarufu mkubwa ghafla. Ukaajiri vibarua wa kutosha. Kuna wakati alitangaza kwa wafanyakazi kuwa atakayepata jiwe la dhahabu ampelekee na kumpa motisha ya senti 10,” anasema Maroda na kwamba pesa hiyo ilikuwa inamwezesha mtu kulipa kodi ya kichwa kwenye serikali ya kikoloni.

Wakati nchi hii inapata uhuru, Maroda anasema kuwa kodi ya kichwa ilikuwa imefikia shilingi 60 ambapo nayo ilikuwa ni ngumu kupatikana na hivyo watu walijikuta wakilazimika kufanya vibarua kwenye maeneo mbalimbali ya wazungu na wahindi ili kuweza kufanikisha ulipaji wa kodi hiyo.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

Mzee Maroda anasema kuwa suala la muungano wa Tanganyika na Zanzibar lililofanyika mwaka 1964 hakushiriki kutokana na kujikita zaidi kwenye masuala ya utafutaji pesa ili kujinyanyua kimaisha pamoja na familia yake. Ila anasema alikuwa akiona shamrashamra ya kuanzishwa kwa muungano huo ambao anasema kila Mtanzania wakati ule aliuunga mkono.

Yeye anasema Muungano ni jambo zuri ambalo limewawezesha watu wa Tanganyika na Zanzibar kuwa ndugu na hivyo anauombea udumu hata baada ya yeye kuondoka duniani.

Anasema wanaoonekana kutoupenda muungano huo hawajui historia na umuhimu wa kuungana ili kuwa kitu kimoja Mzee Maroda alikuwa na mke ambaye kwa bahati mbaya alifariki dunia. Walibahatika kupata watoto wanane ambapo mpaka hivi sasa anaishi kwa mwanawe wa pili kuzaliwa aliyepo mtaa wa Buzuka ambaye ni mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo anayefahamika kwa jina la Issa Maroda.

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Kareny Masasy

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi