loader
Dstv Habarileo  Mobile
Ifahamu Hifadhi ya Ruaha iliyo kubwa kuliko zote nchini

Ifahamu Hifadhi ya Ruaha iliyo kubwa kuliko zote nchini

Hili ni swali muhimu hasa kwa wale Watanzania ambao mpaka leo hawajausahau ule wimbo maarufu uliokuwa ukiimbwa katika shuleni za msingi kwa miaka ilee. “Mbuga za wanyama Tanzania, ya kwanza ni Serengeti, Ngongoro, Manyara na Mikumi…ooh Tanzania oyee.”

Kabongo ni Ofisa Utalii wa Ofisi ya Utalii ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inayojumuisha mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Rukwa na Katavi. Mbali na hifadhi ya Ruaha, katika mikoa hiyo kuna hifadhi nyingine kama Udzungwa, Kitulo na Katavi ambazo umaarufu wake unakua siku hadi siku.

Wakati wimbo uliokuwa unasifia mbuga za Tanzania ukiwa haupotei vinywani mwa Watanzania, Hifadhi ya Ruaha ilikuwa na ukubwa wa kilometa za mraba 1,300 tu. Hii leo kwa mujibu wa Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Ruaha, Dk Christopher Timbuka, hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilometa za mraba 20,380.

Ukubwa huo unaifanya hifadhi hiyo iwe kubwa kuliko zote Tanzania na ya pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya Hifadhi ya Kruger iliyopo Afrika Kusini; Hifadhi ya Serengeti inakuwa ya pili kwa ukubwa nchini ikiwa kilometa za mraba 14,763.

Dk Timbuka anasema ukubwa wa eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha inatokana na kuongezwa katika hifadhi hiyo, bonde la Ihefu linalopakana na Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya. “Mwaka 2006, Serikali iliwaondoa na kuwalipa fidia wananchi waliokuwa wakiishi na kufanya shughuli zao katika bonde hilo,” anasema.

Anasema katika bonde hilo kulikuwa na aina mbalimbali za wanyamapori waliokimbia shughuli za binadamu; hata hivyo wanyama hao wanaendelea kurejea huku uoto wa asili ukizidi kushamiri. “Changamoto kubwa tuliyonayo ni kulinda bonde hili na kuboresha miundombinu yake kwa faida ya Watanzania wote na kwa ajili ya kukuza utalii katika Hifadhi hii ya Ruaha,” anasema Dk Timbuka.

Aidha asilimia 56 ya maji yake hutiririkia katika Mto Ruaha Mkuu na hatimaye Bwawa la Mtera kunakozalishwa umeme wa Gridi ya Taifa. Mbali na kufikika kwa ndege, Hifadhi ya Ruaha inafikika kwa njia ya barabara; ikiwa ni kilometa 120 kutoka mjini Iringa, kilometa 322 kutoka Mikumi.

Pia ni sawa na umbali wa kilometa 369 kutoka mkoani Dodoma, kilometa 615 kutoka Dar es Salaam, km 502 kutoka Mbeya na 807 kutoka Arusha. Akizungumzia maumbile asilia ya kijiografia hifadhini, anasema ina mito, kuta za bonde la ufa, chemichem za maji, vilima na uoto wa asili wa Zambezi na Savana huku hali ya hewa ikianzia mita 750 hadi 1900 kutoka usawa wa bahari.

Dk Timbuka anavitaja vivutio vikuu vya utalii hifadhini kuwa ni pamoja na Mto Ruaha Mkuu, makundi makubwa ya Tembo, Simba, Pundamilia, Nyati na Twiga. Mbali na ndege wa aina mbalimbali anawataja wanyama wengine waliopo hifadhini kuwa ni tandala wadogo na wakubwa, viboko na mamba, fisi, duma, palahala, korongo, swala granti, mbwa mwitu, chui, pofu, pundamilia, kuro, ngiri na swala pala.

Ofisa Utalii wa hifadhi hiyo, Eva Kwele anasema Watanzania wanatakiwa kuitembelea hifadhi hiyo kubwa kuliko zote nchini na kwa kufanya hivyo si tu kwamba watakuza utalii wa ndani lakini pia watajifunza mengi yanayohusu wanyama. Akitoa takwimu za watalii wa nje na wa ndani, Kwele anasema katika kipindi cha miaka mitano (2008/2013) hifadhi hiyo ilipokea watalii 83,723 tu na kati yao 46,944 walitoka nje huku 36,779 wakiwa wa ndani.

Idadi hiyo ni nusu ya watalii wanaotembelea Hifadhi ya Arusha, kwa mwaka na ni zaidi ya mara nne ya watalii wanaotembelea Hifadhi ya Serengeti na Kilimanjaro kwa mwaka.

Katika kuboresha shughuli za utalii katika hifadhi hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Mipango na Utalii wa Tanapa, Dk Ezekiel Dembe anasema Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) inakazana kuifanya Ruaha iwe kiini cha hifadhi zote za Kusini kwa kuwa na wageni wengi na kuongeza mapato yake.

“Mbali na utalii wa kutumia magari, tumeongeza utalii wa kutembea kwa miguu, utalii wa usiku, utalii wa kutumia tufe,” anasema. Anasema utalii wa tufe unalenga kuwapunguzia watalii uchovu unaosababishwa na matumizi ya muda mrefu wa magari. Kupitia utalii wa tufe (anga) watalii watakuwa na fursa ya kuangalia vivutio mbalimbali vilivyoko katika hifadhi hiyo kubwa.

Katika kuboresha huduma za utalii, Kwele ambaye ni Ofisa Utalii wa hifadhi hiyo anasema utalii wa kutembea kwa miguu unawavutia watalii wengi na ni chanzo kikuu cha mapato cha hifadhi hiyo. “Utalii wa aina hii upo katika maeneo mengi duniani na hupendwa sana na watalii kwasababu huwafanya wawe jirani na mazingira,” anasema Godwell ole Meing’ataki.

Meing’ataki ni Mratibu wa Mradi wa miaka mitano wa Kuimarisha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST). Anasema mradi huo unaendelea kuboresha mazingira ya hifadhi na maeneo yote ya hifadhi Kusini mwa Tanzania ili kulinda baionuwai yake kwa maendeleo ya taifa.

Dk Dembe anasema Tanapa inaendelea kuhamasisha wadau wengine wa sekta ya utalii kuboresha huduma zingine za kitalii ili kuvutia watalii wengi katika hifadhi hiyo. Anazitaja huduma zinazotakiwa kuboreshwa kuwa ni pamoja na ya mahoteli, barabara, viwanja vya ndege na kampuni za kusafirisha watalii.

Taarifa iliyotolewa na Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) imezitaka nchi za Kiafrika kukuza utalii wake wa ndani kama mkakati wake wa kwanza kabla ya kuhangaikia watalii wa nje hiyo ikiwa ni njia muafaka ya kuboresha uchumi wao. Katibu Mkuu wa UNWTO, Taleb Rifai alinukuliwa na vyombo vya habari kwenye mkutano mkuu wa shirika hilo uliofanyika Agosti, 2013 nchini Zambia akisema “takwimu zinaonesha utalii wa ndani umekuwa msingi wa shughuli za kiuchumi katika nchi nyingi.”

Rifai anasema takwimu za mwaka 2012 zinaonesha zaidi ya watu bilioni moja walisafiri kama watalii wa kigeni duniani kote huku watalii wa ndani, ndani ya mipaka ya nchi zao walifika bilioni 5. “Ingawaje watalii wa ndani hawakuchangia upatikanaji wa fedha za kigeni, walisaidia katika nchi zao kutengeneza ajira mpya na ukuaji wa miundombinu,” anasema.

Katika kusaidia kukuza utalii wa ndani, Klabu ya Wanahabari Mkoa wa Iringa (IPC) pamoja na waandishi wengine mkoani hapa wameanzisha kampeni waliyoipa jina “Hifadhi ya Ruaha, Iringa… Itembelee… Jivumbulie” Ni hivi karibuni kwa kupitia kampeni hiyo ya “Hifadhi ya Ruaha, Iringa….Itembelee….Jivumbulie” wanahabari 16 kutoka mkoani Iringa walikwenda kutalii katika mikoa ya Kaskazini ili wajifunze yale yaliyosaidia kukuza sekta ya utalii katika kanda hiyo.

Mbali na kutembelea kampuni za utalii, hoteli zinazotoa huduma kwa watalii, wafanyabiashara wa bidhaa za kitalii, walifanya utalii katika hifadhi za Serengeti, Manyara, Tarangile, Arusha na Kilimanjaro.

Baadhi ya mambo waliyojifunza na ambayo wamayaingiza katika kampeni yao ili kukuza utalii katika Hifadhi ya Ruaha ni pamoja na; Huduma za Hoteli Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Mkoa wa Arusha una vitanda zaidi ya 3,000 vya kulala wageni kwa siku; takwimu hiyo inaweza kuwa mara 10 ikilinganishwa na hali ya huduma hiyo mkoani Iringa.

Hakimu Mwafongo mwandishi wa gazeti la Mwananchi anasema “wajasiriamali jitokezeni, ichangamkieni fursa hii, jengeni hoteli za kitalii, mtafanya biashara kubwa kama wenzetu wa Arusha, mtakuza utalii, uchumi wa Mkoa wa Iringa na Taifa kwa ujumla.” Kwa upande wake Dk Dembe anasema “kwa kuanzia maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa hoteli za kitalii yanapatikana ndani ya Hifadhi ya Ruaha.”

Kampuni za Utalii

Katika Mkoa wa Arusha na Moshi kuna kampuni za utalii zaidi ya 380 wakati mkoani Iringa kampuni hizo hazifiki 10. Mwandishi wa Habari wa Kitulo FM, Conrad Mpilla anasema “hii ni fursa nyingine ya uwekezaji;itawahakikishia wawekezaji mapato ya uhakika lakini itasaidia kukuza utalii katika Hifadhi ya Ruaha. Kampuni hizo zina kazi nyingi ikiwemo ya kusafirisha na kuongoza watalii.”

Dk Dembe anasema “pamoja wawekezaji katika mikoa ya Kusini kuchelewa kuichangamkia fursa hii, tunaendelea kuwahamasisha.” Biashara zinazohusiana na utalii Hii ni fursa kubwa na imewainua kiuchumi vijana wengi Arusha na Moshi, anasema Ofisa Mahusiano Mwandamizi wa Tanapa, Catherine Mbena.

Mwandishi wa Habari wa Channel Ten mkoani Iringa, Clement Sanga anasema “vijana tusiiache fursa hii; biashara ya vinyago na vitu mbalimbali vya utamaduni wa Kiafrika vinawapa fedha vijana wengi katika mikoa hiyo ya Kaskazini; tupunguze kunywa pombe na anasa zingine, tugeukie fursa hii.”

Wabeba mizigo ya watalii

Hii ni fursa nyingine inayoweza kuinua huduma ya utalii mkoani Iringa; kazi hii katika mikoa ya Arusha na Moshi inafanywa na vijana kupitia kampuni za utalii. Mwandishi wa Star Tv mkoani Njombe, Mercy James anasema “Tumeona Arusha na Hifadhi ya Kilimanjaro; vijana wa mkoani Iringa wanaweza kufanya kazi hii ya kuwasaidia watalii; Hifadhi ya Udzungwa na Kitulo zinahitaji watoa huduma wa aina hiyo.”

Vyakula vya jadi

Hii ni fursa nyingine inayoweza kuvuta watalii wengi; kwenye baadhi ya hoteli huko Arusha tumeshuhudia vyakula vya jadi kama ugali wa muhogo, kisamvu na nyama za wanyama wadogo wa kufugwa kama simbilisi na sungura vikiuzwa na kuchangamkiwa na wageni wengi.

Mwandishi na mtangazaji wa Redio Ebony FM ya mjini Iringa, Raymond Francis anasema “wenyeji wa Iringa mbali na kuwa aina nyingi ya vyakula vyao vya kijadi, wanaweza kutengeneza vyakula vya aina hiyo na kupata wageni wengi.”

Shule za utalii na utawala wa hoteli

Ili kuvutia watalii, wawekezaji mkoani Iringa wanatakiwa kubadilika kwa kuajiri au kufanya kazi na watu wenye ujuzi katika eneo hilo. Mwandishi wa Kujitegemea, Francis Godwin anasema muda umefika kwa wawekezaji kuichangamkia fursa hiyo kwa kuanzisha vyuo vitakavyotoa wataalamu watakaofanya kazi katika sekta hiyo ili wasaidie kuinua huduma za utalii mkoani Iringa.

Vituo vya Utalii na Utamaduni

Huko Kaskazini eneo hili pia limepiga hatua kubwa; kabla ya watalii kupelekwa hifadhi hupendelea kutembelea vituo hivyo ili kupata taarifa za vivutio mbalimbali.

Vituo hivyo vinaweza pia kutoa huduma zingine kama za kutembelea na kuangalia hifadhi za nyoka, upandaji wa ngamia na biashara ya bidhaa za makabila mbalimbali ya mikoa hiyo. Denis Mlowe wa Tanzania Daima anasema “hii ni fursa nyingine mkoani Iringa. Inawezekana na ina nafasi kubwa ya kuinua utalii wa ndani.”

Mtandao wa barabara

Ukiacha Hifadhi ya Serengeti kwa sababu ya kisheria, hifadhi nyingine zote katika mikoa ya Arusha na Moshi, barabara zake hadi getini zimejengwa kwa kiwango cha lami au ziko jirani na barabara kuu za lami. Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 Rais Jakaya Kikwete alitoa ahadi ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kilometa 104 kutoka Iringa Mjini hadi katika geti la kuingilia Hifadhi ya Ruaha.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Iringa, Mhandisi Paulo Lyakurwa anasema ahadi hiyo imeanza kutekelezwa na kwamba Sh bilioni 96.4 zitatumika kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Sera ya Utalii

Kwa kupitia Kifungu cha 14.5 cha Toleo la mwaka 1991 la sera ya utalii Serikali itekeleze ahadi ya kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha utalii wa wananchi unaimarishwa na kuendelezwa.

Kifungu cha 14.6 cha sera hiyo kinazungumzia kutazama upya sheria zilizopo zinazohusu biashara ya utalii kwa nia ya kuzifanyia marekebisho ili kuimarisha na kuendeleza shughuli za utalii nchini.Aidha sheria mpya zitatungwa kukidhi haja na mazingira yaliyopo katika kuendeleza utalii.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Frank Leonard

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi