loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JABIRY ‘DRAGON’: Apania makubwa katika Kick-boxing

 

Ni kauli ya Kaizirege Jabiry ‘Dragon’ (28), mchezaji wa kickboxing. Jabiry ni mzaliwa wa Mkoa wa Dar es Salaam, na amekuwa akiupenda mchezo huo kiasi cha kupata wakati mgumu kutoka kwa ndugu zake waliokuwa wakimzuia wakihofu kuletewa kesi na kugombana na majirani.

Dragon mpole kwa kumtazama usoni, anasema kabla ya kuingia rasmi katika mchezo wa kickboxing, alianza kwa kuushabikia. Anasema hatua hiyo ilimpa shida enzi za utoto wake kutokana na wazazi wake kuchukizwa na kitendo cha mtoto wao kuupenda mchezo huo wakihofu kwamba ungemuingiza katika suala zima la ukorofi kwa watoto wenzake.

“Ukweli nilipata shida sana kuwadhihirishia wazazi wangu kuwa kamwe siwezi kuwa mkorofi kwa kuupenda na kuanza kujifunza mchezo huu, lakini baadaye kidogo walianza kunielewa kwa kuwa hawakuwahi kupokea kesi yangu yoyote kuwa nimepigana au kumpiga mtu.

“Namshukuru Mungu kuanzia hapo nilianza kuungwa mkono na wadau mbalimbali wakiwemo ndugu zangu hatua ilinifanya nipate mafanikio ya kimchezo hadi kuwa bingwa wa mchezo huo katika mkoa wa Mwanza kipindi hicho nikiwa nasoma sekondari,” anasema Dragon.

Anasema hadi sasa, tayari ameshacheza michezo 28 ndani na nje ya Tanzania na katika hiyo, ameshinda michezo 25 zikiwemo knockout (KO)10, huku akipoteza michezo mitatu katika michezo hiyo aliyoicheza katika vipindi tofauti hadi mwanzoni mwa mwaka huu.

Anasema kimsingi mchezo wa kick-boxing ungeweza kulitangaza Taifa na kuleta medali nyingi iwezekanavyo endapo kama viongozi na wadau wangeupa umuhimu mkubwa kwa kunyanyua vipaji vinavyochipukia sambamba na kutoa motisha kwa wachezaji waliopo.

“Nasikitika sana kuona wadau wa mchezo huu ndiyo waliochangia kuuzorotesha kwa kiasi kikubwa na kurudisha nyuma maendeleo ya kickboxing hapa nchini. “Sijui nini sababu ila naamini ipo siku mabadiliko yatakuja na Tanzania itaweza kujitangaza vyema kimataifa tofauti na ilivyo sasa,” anasema.

Anasema Kick-boxing ilikuwa juu Tanzania, lakini kwa sasa huioni wala kuisikia kutokana na matatizo hayo yaliyopo miongoni mwa wadau na viongozi wa mchezo huo. Anasema wengi ni kama wamekuwa na chuki binafsi baina ya wenyewe kwa wenyewe au wao na wachezaji suala ambalo kamwe haliwezi kuufanya mchezo uendelee.

“Kwa sasa Tanzania sina mpinzani wa kweli ukiacha Kaseba ambaye ni kiongozi wangu na mchezaji mwenzangu katika timu namshukuru kwa kunipa ushirikiano mkubwa hadi kufika mahali hapa nilipo na hivyo ndivyo viongozi wanatakiwa kuwa,” anasema Dragon.

Aidha, anasema msingi wa mchezo au kazi yoyote ni nidhamu, jambo analosisitiza kuwa ndiyo lililochangia mafanikio yake hadi hapo alipo na pia kumtangaza vyema kimichezo ndani na nje ya Tanzania. Sambamba na kupata mechi nyingi ambapo baadaye mwezi huu, anatarajia kwenda Canada kupambana na Jackson Paul wa nchi hiyo.

Anasema ili kuuendeleza mchezo huo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, aliamua kuanzisha sehemu ya mazoezi (gym) iitwayo ‘Dragon Fitness Center’ iliyopo Oysterbay. Anasema gym hiyo ni maalumu kwa ajili ya kufundisha kick-boxing na mazoezi mengine kwa watu wenye mahitaji. Anasema pamoja na kuwa mchezaji wa mchezo huo, kitaalamu pia ni mwalimu wa mchezo.

Anasisitiza kuwa suala la nidhamu analolisimamia ndilo linalowafanya wanafunzi wake kunufaika na kile anachokifundisha. Kocha mchezaji huyo anaamini siku moja mchezo huo utapata umaarufu nchini kutokana na mapenzi ya vijana wanaojitokeza katika gym yake na sehemu zingine alizozishuhudia.

Aliwataka viongozi wa kitaifa wanaosimamia michezo kutupia jicho katika klabu za kick-boxing ili kuona moyo walionao vijana hao. Aidha, anasema kimsingi mchezo wa Kick-boxing haufanyi kwa lengo la ‘kuuza sura’ na zaidi, anafanya kutokana na mapenzi aliyonayo huku akiwataka vijana waliopo kwenye fani hiyo kuacha kufikiri kuwa kuna kuuza sura unapokuwa ndani ya ulingo.

Anasema ili kupata mafanikio ni vyema vijana wakaacha kukurupuka na badala yake wakae chini na kutafakari nini wanakusudia kukifanya ndipo wachukue uamuzi wa kufanya hivyo jambo analosema kuwa litawasaidia kulinda sifa zao na kujitengenezea sifa wao sanjari na Taifa lao.

WATANZANIA kama walivyo watu wa mataifa ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi