loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Jamii ijenge utamaduni kuzuia uhalifu

Vitendo vya uhalifu ni kama vile wizi wa mali binafsi na mali za umma, ubakaji, mauaji, kushambulia na kujeruhi, ugaidi, kumiliki silaha kinyume na sheria na makosa mengine mengi ambayo ni kinyume na sheria za nchi.

Uchunguzi wa polisi na tafiti mbalimbali kuhusu uhalifu zinaonesha kuwa wahalifu wanafahamika na wanapanga mipango na kutekeleza uhalifu wao wakiwa ndani ya jamii lakini watu inachelea kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama.

Ripoti za utafiti zinaeleza kuwa kila mtu akiamua kutoa taarifa za kufichua wahalifu na kuripoti matukio ya uhalifu au kuzuia uhalifu ni wazi kuwa vitendo vya uhalifu havitakuwepo.

Kila mmoja ndani ya jamii ana jukumu la kuzuia uhalifu katika mazingira aliyomo pasipo kumpa mhalifu fursa yoyote ya kutenda uhalifu kwa kuwa jukumu la Ulinzi na Usalama ni wajibu wa Jamii nzima.

Hivyo hatuna budi kukubali kuwa uwezo wa mhalifu kutenda au kutotenda uhalifu upo mikononi mwa jamii husika. Mhalifu anaweza kutenda uhalifu kwa kudhamiria, kushawishiwa au kwa kutumia fursa ya kimazingira inayompa mwanya wa kutenda uhalifu pale anapoona aidha, nyumba imeachwa wazi, mzigo unasindikizwa bila ulinzi ama vitu vya thamani vimeachwa mahali popote bila uangalizi.

Pia, mhalifu hutumia nafasi hiyo kutenda uhalifu wake akitimiza usemi usemao “kosa moja goli moja” ikimaanisha kwamba kitendo cha kutokuwa makini na ulinzi wa mali zako au mali zilizo chini ya himaya yako kinampa mhalifu nafasi ya kutekeleza mipango yake ya kutenda uhalifu.

Nachelea kusema kuwa, watu wengi huwapa wahalifu fursa ya kutenda uhalifu pasipo kujijua. Kitendo cha kufumbia macho vitendo vya uhalifu pasipo kuripoti vinawajengea wahalifu mazingira na fursa ya kutimiza kutimiza azma yao.

Ieleweke wazi kuwa, jamii inapaswa kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Jeshi la Polisi katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao kwa kutoa taarifa za uhalifu na kufichua wahalifu ili kuzuia mianya ya kutendeka kwa uhalifu.

Wananchi wana jukumu la kuendeleza kasi ya kushirikiana na jeshi la polisi, vikundi vya ulinzi shirikishi pamoja na askari kata/shehia waliopo katika maeneo yao, huku wakipanga kwa pamoja na kutekeleza mikakati ya kutatua kero za kiusalama katika makazi yao.

Jambo uliloliona, ulilosikia, ulilogusa au kunusa katika eneo lililotendeka uhalifu ni moja ya mambo muhimu yanayotakiwa kutolewa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili kurahisisha, kubainika na kutambulika kwa uhalifu na wahalifu ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Ni wajibu wetu kama raia wema wa Tanzania kuhakikisha tunatimiza majukumu yetu ipasavyo ili tuweze kuimarisha usalama wetu wenyewe na kujenga ustawi wa Taifa.

Ushirikiano wa jamii na Jeshi la Polisi ndio mhimili mkuu wa kuimarisha usalama.

Uhalifu unaweza kuzuilika kwa kutompa nafasi au fursa mhalifu kutimiza kusudio lake, jambo pekee linalomzuia asitende uhalifu ni mazingira yanayomnyima fursa ya kutenda bila kukamatwa au kujulikana. Jamii inapaswa kudumisha ulinzi na usalama wa maisha na mali zao, amani na utulivu kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.

Tabia hii itasaidia kujiletea maendeleo na kuinua hali ya maisha kwa Ulinzi shirikishi unalenga katika kuondoa mazingira ya kutokea tendo lolote la uhalifu katika makazi yetu, hivyo ni vyema kila mmoja wetu afahamu kuwa mkakati wa kuzuia uhalifu unaanzia ngazi ya familia, mtaa, kata/shehia, tarafa, wilaya, mkoa hadi taifa kwa ujumla.

Ili kufanikiwa kuondoa kero ya uhalifu katika nchi yetu, uongozi wa Shehia, Mtaa, kijiji au kitongoji hauna budi kujenga ubia wa dhati na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana katika kubaini na kufichua uhalifu na wahalifu ili makazi yao yaendelee kuwa salama.

Ni vyema kutambua kuwa jukumu la kuzuia uhalifu ni la jamii nzima kila mwananchi ana wajibu wa kuzuia uhalifu kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu waliopo kwenye jamii.

WIZARA ya Viwanda na Biashara imepania ...

foto
Mwandishi: Tamimu Adamu, Jeshi la Polisi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi