loader
Picha

Jamii kiini mmomonyoko wa maadili

Mapema juzi bungeni Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ilikiri kwamba hivi sasa tatizo la mmomonyoko wa maadili ya Kitanzania unaongezeka kila uchwao, huku ongezeko la maudhui yasiyofaa kwa maadili ya nchi yetu yakishamiri mitandaoni.

Matukio haya yanaonesha kuna mahali jamii imeshindwa ama kutimiza wajibu wake au kuna ulegevu wa baadhi ya sheria na kanuni zinazodhibiti mwenendo wa maudhui hayo hususan mitandao.

Ni ukweli usiopingika kwamba wazazi na viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kujenga au kuchangia kuporomoka kwa maadili hivyo ni vyema wakatumia nafasi zao kikamilifu kuijenga jamii yenye maadili.

Tunaposema maadili ni mchanganyiko wa vitu vingi vinavyoambatana na ustaarabu, utiifu, imani, heshima, nidhamu, huruma na upendo.

Wazazi na viongozi wa dini tunaamini wana mchango mkubwa katika kujenga maadili ya Mtanzania, lakini kwa dunia ya leo baadhi ya wazazi wanachangia mmomonyoko huo kwa njia moja au nyingine.

Kuchangia huku kunatokana na mtindo wa maisha wa leo ambao, katika jamii wengi wa leo wanadhani mtoto ni yule uliyemzaa mwenyewe na yule wa jirani jukumu la ulezi siyo lako na hata kama ukimuona anafanya au wanafanya matendo yasiyofaa huwezi kumkanya.

Mtazamo huo ndiyo umechangia zaidi mmomonyoko wa maadili ingawa pia hata utandawazi una mchango wake kwa kuporomoka maadili lakini kama jamii ikisimama kwenye nafasi yake, maadili yatarudi kwenye mstari.

Aidha kupitishwa kwa kanuni za maudhui mitandaoni, redioni na kwenye runinga kutasaidia kujenga upya kama siyo kupunguza mmomonyoko wa maadili uliopo hivi sasa kwani kila mtu kuanzia mtoto hadi mzee, anaweza kusema lolote liwe jema au baya na jamii ikaona ni sawa tu.

Hatua iliyochukuliwa na wizara kudhibiti maudhui ni jambo jema linalopaswa kuungwa mkono na pia jamii nayo ni vyema sasa ikajitathmini na kuangalia je imetimiza wajibu wake?

Ifike mahali suala la maadili lisiwe la mzazi na wanawe bali liwe jambo la jamii kuitana na kuonyana.

Hivi sasa tumeshuhudia hata baadhi ya wazazi wanaongoza kwa kuwatusi watoto wao hata watu wengine na jamii inaona ni sawa tu, jambo ambalo siyo sahihi hata kidogo kwani kuendelea kunyamaza kunachangia kuongezeka zaidi kwa mmomonyoko huo na pia hata watoto wanaona matusi na mambo mengine yasiyofaa ni sehemu ya maisha.

Tuamke sasa suala la maadili ni la jamii yote na kila mmoja wetu anapaswa kujihoji kama ametimiza wajibu wake na kutambua kuwa maadili siyo kitu binafsi bali tunapaswa sote tuwajibike.

UKOSEFU wa vibanda vya kujihifadhi wasafi ri wakati wa wakisubiri ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi