loader
Picha

JICHO: Hawajui madhara ya tumbaku au wameamua kujimaliza kiafya?

Je, kama bidhaa husika ni hatari kwa afya, kwa nini zao na bidhaa zake zinaendelea kuzalishwa na kutumika? Je, inawezekana jamii kuacha kutumia tumbaku? Jicho langu limepata sehemu ya majibu kutoka katika taarifa ya Chama cha Kudhibiti Tumbaku Tanzania (TTCF) iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji, Lutgard Kagaruki.

Hivyo nimeona pia nikushirikishe msomaji sehemu ya taarifa hiyo inayosema: Kila mwaka, tumbaku huua takribani wavutaji milioni saba duniani na wengine 700,000 wasiovuta, bali wanaovutishwa moshi wa tumbaku.

Baada ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), kugundua kuwa tumbaku ni janga la kimataifa, lilitunga Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Tumbaku wenye madhumuni ya kulinda kizazi cha sasa na kijacho dhidi ya majanga ya kiafya, kijamii, kiuchumi na kimazingira, yatokanayo na matumizi ya tumbaku na moshi wake.

Mpaka sasa nchi 180 zimeridhia mkataba huu. Nchi zilizoutekeleza, matokeo yameonekana kwenye kupungua kwa matumizi ya tumbaku na magonjwa yatokanayo na bidhaa hii. Magonjwa hayo yamekuwa yakigharimu siyo tu jamii, bali pia serikali, katika kuyatibu.

Nayo ni saratani, magonjwa ya moyo, kisukari na magonjwa sugu ya kifua na ukosefu wa nguvu za kiume. Tanzania iliridhia mkataba huu Aprili 2007, hivyo ina wajibika kuutekeleza kikamilifu.

Wakati nchi za Afrika Mashariki zina sheria madhubuti ya kukidhi matumizi ya tumbaku zinazoendana na matakwa ya mkataba, kwa upande wa Tanzania haijakidhi hilo. Vile vile, hapa nchini uzalishaji wa tumbaku unaongezeka wakati Kenya na Uganda kilimo hicho kikishuka na kujikita katika kulima mazao mbadala.

Kinachosikitisha ni kuona kampuni zikija nchini na kufungua ofisi na kueneza kilimo cha tumbaku. Kama Kaulimbiu ya mwaka huu ya Shirika la Afya Ulimwenguni ya Siku ya Kutotumia Tumbaku Duniani ilivyosema, ‘Tumbaku tishio la maendeleo’; hakuna nchi duniani iliyoendelea kupitia biashara ya tumbaku.

Ndiyo maana biashara hii imekufa katika nchi zilizoendelea ilikoanzia, huku kampuni za huko zikikimbilia kwenye nchi zinazoendelea, kuendeleza biashara hiyo. Kwa mfano, Malawi inayoongoza kwenye kilimo cha tumbaku katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, pato lake la Taifa (GDP) ni la chini sana, huku robo tatu ya nchi hiyo ikiwa jangwa, kutokana na ukataji miti kwa ajili ya kukaushia tumbaku.

Hapa nchini, mkoa wa Tabora unaoongoza kwenye kilimo cha tumbaku, pia upo ukataji mkubwa wa miti ya kukaushia tumbaku. Kati ya mwaka 2010/11 Tabora ilipoteza miti yenye gharama ya zaidi ya Sh bilioni 20 iliyokatwa kukaushia tumbaku.

Zaidi ya hapo, sehemu zinazolima tumbaku mara nyingi ni masikini; kwa mfano, wakati wastani wa pato la Mtanzania ni Sh 362,000, kwa Tabora ni Sh 297,000. Kuhusu afya, utafiti uliofanyika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na Hospitali ya Taifa Muhimbili mwaka 2009, ulionesha kuwa saratani inayohusishwa na matumizi ya tumbaku moja kwa moja.

Matibabu yake hulisababishia taifa hasara ya zaidi ya Sh bilioni 89 kwa mwaka. Utafii uliofanyika Hospitali ya Taifa Muhimbili mwaka 2014 ulionesha kuwa, gharama za matibabu ya magonjwa ya moyo yanayohusishwa na matumizi ya tumbaku, yaligharimu zaidi ya Sh bilioni 400 kwa mwaka. Hii ni kwa hospitali mbili tu nchini ikihusisha magonjwa mawili tu yanayosababishwa na tumbaku

JUZI iliibuka taarifa katika mitandao ya kijamii juu ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi