loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JICHO LANGU: Inasikitisha, kumtupa mtoto kama taka!

Haustahili msamaha zaidi ya sheria kuchukua mkondo wake. Hakika Mungu alikuwa pamoja na mtoto huyu. Si mwingine, bali ni mtoto aliyepewa jina la Bahati huko wilayani Ruangwa, mkoani Lindi. Mama yake mzazi baada ya kujifungua, alipomtupa chooni, hakuzama.

Alibaki akielea kwenye kinyesi kabla ya kuokolewa na wasamaria. Polisi ilikuwa ikiendelea kumsaka mama anayehusika. Tukio hili la hivi karibuni, linasikitisha sana. Inasadikiwa mtoto huyo alizaliwa Julai 21 mwaka huu. Akatupwa kwenye choo cha shule mjini Ruangwa.

Asubuhi, wakati wanafunzi wanafanya usafi , walisikia sauti ya mtoto akilia ndani ya shimo la choo. Walitoa taarifa kwa walimu. Jitihada zilifanyika kwa kushirikiana na Polisi; mtoto akaokolewa akiwa hai.

Naambiwa mtoto huyo sasa yuko chini ya uangalizi wa madaktari na wauguzi wakisaidiana na watumishi wa Idara ya Ustawi wa Jamii. Mungu aendelee kumsimamia malaika huyu.

Tukio hili ni sehemu ya vitendo vya ukatili kwa watoto ambavyo hutokea mara kwa mara nchini. Ukiacha vile ambavyo huripotiwa kwenye vyombo vya habari, vipo vingine ambavyo huishia kwenye jamii.

Hivi karibuni, imeripotiwa kuwa mama mmoja mkoani Kagera amemziba pua na mdomo mtoto wake mwenye umri wa miezi tisa na kusababisha kifo chake. Alipohojiwa, amedai amefanya hivyo kwa sababu ya hali ngumu ya maisha.

Kwa maana kwamba hawezi kumudu gharama za malezi. Hata hivyo, ukifuatilia matukio ya utupaji watoto, siyo tu kwa Tanzania. Bali hata nchi nyingine, zikiwamo zilizoendelea. Zina watu katili ambao hukatisha maisha ya watoto kwa sababu wanazozifahamu wao.

Niliwahi kusoma kwenye mtandao, nchini Japan, hospitali moja iliamua kuanzisha huduma maalumu kwa watu wanaotupa watoto wachanga. Ilitengeneza chumba cha kutupia watoto hao kuwanusuru na vifo.

Hospitali hiyo ya Jikei inayomilikiwa na Kanisa Katoliki , iliyoko Kusini mwa Mji wa Kumamoto, ilichukua jukumu hilo kunusuru maisha ya viumbe hao kutokana na utupaji watoto kukithiri katika maeneo mbalimbali.

Ingawa nchi hiyo inapinga utupaji wa watoto, iliona tatizo limezidi kuwa kubwa hivyo ikaamua kutengeneza chumba hicho kunusuru roho za watoto hao. Wanaofanya vitendo hivyo, wanaweza kudhaniwa wana matatizo ya akili.

Ukweli ni kwamba wengi wao huwa na akili timamu. Tatizo ni ukatili unaochochewa na ubinafsi. Utasikia wahusika wakijitetea eti umasikini ndiyo sababu ya kufanya hivyo. Lakini binafsi, sioni kama huo ni utetezi wa kutenda uhalifu huo.

Baadhi ya watuhumiwa wa vitendo hivyo, hudai kufanya unyama huo kwa madai ya kuwahofia wazazi na walezi wao. Kundi hili linahusisha pia wanafunzi. Lakini utetezi huo kamwe hauwezi kupata msamaha siyo tu wa sheria, bali hata kwenye jamii.

Kama wanafahamu hawana uwezo wa kulea, kwa nini waruhusu kubeba ujauzito? Haiingii akilini kuona mtu anavumilia miezi tisa yote ya ujauzito, lakini anaishia kuua mtoto. Hali ngumu gani hiyo ya maisha?

Kama ni hivyo, basi masikini kibao tunaoambiwa wanaishi chini ya dola moja, wasingezaa. Hapa kikubwa ninachokiona, wengine hufanya hivyo kukwepa majukumu ya kulea kwa lengo la kuendelea kuponda starehe au kubaki na usichana.

Kwa mama mwenye roho ya uzazi na huruma, ni bora angembeba mtoto kwa usalama na kwenda kumlaza sehemu salama ambayo angeweza kuokotwa na wasamaria kuliko kumuua. Vipo vituo vya kulelea yatima karibu kila mji.

Kwa nini watu hawa wasiwapeleke na kuwaacha kwenye vituo hivyo wakaokolewe na wasamaria badala ya kutumbukiza mtoto chooni au kumkaba mpaka afe?

Naamini vitendo vinaweza kupungua kama si kukoma iwapo jamii itashirikiana na polisi kufichua wahalifu. Nina imani haiwezi kuwa kazi ngumu kwa polisi kutafuta na kupata mtu aliyetumbukiza mtoto chooni kwa sababu mjamzito anafahamika.

Kwa nini jamii isijiulize, mtu aliyekuwa mjamzito katika siku za karibuni, ghafla anaonekana hana ujauzito wala mtoto? Mfano, kwa tukio kama hilo la Ruangwa, aliyetupa mtoto kwenye choo cha shule, kwa vyovyote ni mwanajamii katika maeneo ya mji huo.

Kama jamii itakaa kimya juu ya uhalifu huu, hali hiyo inaweza kuchangia ongezeko la utupaji wa watoto wasio na hatia. Jamii ikishiriki, itasaidia polisi kutokomeza ukatili huu. twessige@yahoo.com

Naamka asubuhi,  sioni kilongalonga, 
Napapasa kitandani,  hamadi hiki hapa,  

foto
Mwandishi: Stellah Nyemenohi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi