loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JICHO LANGU: Kamata kamata wamachinga, furaha ya mgambo

Wapenzi wa samaki wa baharini waishio maeneo hayo, wanafahamu soko hilo. Ukitaka vibua, jodari, changu, kamba, chewa na kasa , hapo ndipo mahali pake. Hata hivyo nilipofika sokoni hapo, nilishangaa.

Wachuuzi wa kitoweo hicho walikuwa katika wasiwasi mkubwa mithili ya wanaouza bidhaa haramu. Wachuuzi hao walikuwa wakiangaza macho huku na kule.

Nikasikia wakiulizana, ‘hawa jamaa wako wapi’. Mmoja akapasha habari kuwa wako ‘Buguruni Malapa’. Baadhi yao wakaanza kufungasha samaki hao wabichi. Ndipo nikabaini walikuwa wakihofu kukamatwa na mgambo wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.

Nikabaini soko hilo si halali. Licha ya kwamba limekuwepo miaka mingi sana, lakini halitambuliki. Halmashauri ya Manispaa ya Ilala hailitambui. Ndiyo maana imeamua kutuma mgambo wadhibiti biashara hiyo.

Ingawa sikusubiri kushuhudia mgambo walivyotimua wachuuzi hao, kama ilivyozoeleka katika operesheni za namna hiyo, kwa vyovyote vile kulikuwa na purukushani. Mapambano kati ya mgambo na wafanyabiashara ndogo yamegeuka sugu.

Siyo tu katika eneo hilo la Buguruni. Bali katika maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam na hata miji mingine mikubwa. Purukushani baina ya mamlaka na wamachinga zimegeuka kero.

Mara nyingi, mamlaka hulazimika kutumia nguvu nyingi kuondoa wafanyabiashara ndogo ambao hujipatia riziki kwa kuendesha shughuli katika maeneo yasiyo halali ikiwemo barabarani. Usiombe kushuhudia mgambo wakiendesha operesheni hizo.

Wengi huwa wamefura kwa hasira. Baadhi yao hukiuka hata haki za binadamu katika kuendesha operesheni hizo. Hupiga, kudhalilisha, kujeruhi na hata kufanya uharibifu wa mali za wafanyabiashara husika.

Lakini pia, zipo taarifa kwamba katika operesheni hizo, baadhi ya mgambo wasio waaminifu hujinufaisha kwa kupora mali za wafanyabiashara. Katika mazingira ya namna hiyo, vurugu huwa haziepukiki.

Laiti kama hasira na nguvu zitumiwazo na mamlaka kutimua wafanyabiashara hao, zingekuwa zikitumika kuzuia kurejea kwenye maeneo yasiyoruhusiwa! Tatizo hili lisingekuwa sugu. Mamlaka zimeshindwa kutekeleza dhana ya ‘Kuzuia ni bora kuliko kutibu’.

Badala yake, zimekuwa na nguvu ya soda. Huendesha operesheni kwa msimu. Kisha huenda likizo kwa muda usiojulikana kabla ya kushitukiza tena wakati maeneo yakiwa yameshafurika wafanyabiashara jambo ambalo ni hatari.

Hali hiyo hushawishi na kuaminisha jamii juu ya dhana kwamba wapo watu ambao hunufaika na ukamataji wamachinga mara kwa mara.

Zipo taarifa kwamba, baadhi ya watendaji, hunufaika na uwepo wa wafanyabiashara hao kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kwa kutoza ushuru wa aina mbalimbali.

Utashuhudia watu wenye risiti wakizungukia wafanyabiashara na kutoza ushuru ambao hata hivyo huwa hauelezwi ni wa nini ikizingatiwa maeneo wanayokuwepo siyo halali.

Ili kujiengua na dhana hii, lazima mamlaka husika, zieleze ni kwa nini huamua kukaa na kusubiri wafanyabiashara warejee na kuota mizizi ? Kama ni uzembe basi zikiri wazi zihukumiwe inavyostahili.

Ikumbukwe operesheni husika hugharimu rasilimali fedha na watu kuziendesha. Lazima ishangaze kuona wahusika wakitoa mwanya kwa wafanyabiashara kurejea kwenye maeneo husika na hatimaye kuota mizizi. Mfano mzuri ni katika Jiji la Dar es Salaam.

Zimekuwa zikishuhudiwa operesheni za nguvu zinazofanyika kuondoa wamachinga katika manispaa zote za Kinondoni, Ilala na Temeke. Lakini baada ya muda mfupi, utakuta maeneo hayo hayo yamefurika wafanyabiashara.

Ajabu ni kwamba, watendaji wa halmashauri husika hupita kila siku wakishuhudia shughuli zikiendelea. Tena nyingine huendeshwa karibu kabisa na ofisi za mamlaka husika.

Lakini baadaye, ukishapita muda fulani, inasikika mikakati ikiandaliwa na mamlaka kwa ajili ya kuondoa wamachinga kana kwamba wamezuka ghafla. Tena wakati mwingine, utasikia watendaji wakifanya vikao vinavyogharimu siyo tu muda wa kazi, bali hata fedha.

Isitoshe, rasilimali watu na fedha kwa maana ya posho, hutumika kutekeleza operesheni hizo. Vilevile magari hutumika kubeba waendesha operesheni hiyo.

Kwa mtindo huu, ni kwa nini isijengeke dhana kwamba wapo watu wanaonufaika na ama kurejea kwa wamachinga hao au operesheni za kuwaondoa kwenye maeneo yasiyoruhusiwa? twessige@yahoo.com

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Riadha ...

foto
Mwandishi: Stellah Nyemenohi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi