loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JICHO LANGU: Maumivu ya jino, unaandikiwa kupima malaria

Jicho halikwenda kwenye zahanati hiyo ya serikali kwa ajili ya kuvinjari. La hasha! Bali ni kwa sababu ya kuuguliwa. Lilinasa mambo mengi. Nikakumbuka wimbo uliopigwa na kundi la muziki wa Bongo Fleva la Wagosi wa Kaya.

Wimbo huo si mwingine bali wa ‘Wauguzi’. Ngoja nikumegee mistari kadhaa ya wimbo huo. Baada ya hapo nitakueleza ni kwa nini nilikumbuka wimbo huo. ‘Wauguzi, wauguzi, madaktari na manesi, wauguzi, Taratibu jamani haya, tutaonana wabaya haya.

‘Ninyi wauguzi wa afya ni watu wa muhimu kwa jamii, tatizo baadhi yenu mna kiburi kazini, inabidi mfundishwe ukarimu moyoni. ‘Hamkufundishwa mtukane wagonjwa matusi ya nguoni.

Naanza na manesi, nyie manesi mna nyodo, mnataka mgonjwa awanyenyekee kama watoto… ‘Kaeni mkijua kazi ya nesi ni kama wito. Maisha ni magumu bwana ndiyo maana mmekimbilia unesi.

‘Haikatazi kazi kidogo muwe na interest (maslahi) sindano mnatushindilia mpaka zinaparalaizi mguu… ‘ Hili swali naiuliza wizara ya afya, naomba mnijibu mapema kabla hata sijafa. Kodi zinazolipwa hospitali zinafanya kazi gani, hakuna mafeni watu wanajipepea magazeti…

‘Haiwezekani bwana, huduma tunazichangia mbona hazijainuka. Sometimes (wakati mwingine) madaktari hawaonekani, akija kuonekana pombe imejaa kichwani. Badala ya panadol atakuandikia …sasa unatazama huyu daktari gani?’.

Ngoja nisaidie kuongeza mistari mingine ambayo jicho langu lilibaini kwenye zahanati hiyo ya serikali . Limebaini utekelezaji wa sera ya afya juu ya utoaji huduma bure kwa mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano, umebaki kwenye karatasi.

Huduma ya bure inayopatikana ni kusikilizwa na daktari, tena wakati mwingine mgonjwa anasikilizwa na daktari mwenye kisirani, asiye na upendo wala imani. Ukishaandikiwa kufanyiwa vipimo na majibu yakatoka, sana sana dawa utakayopata bure ni Panadol.

Hizo nyingine utaambiwa kajitegemee kwa kununua kwenye maduka ya dawa. Siyo mara ya kwanza kwa jicho langu kushuhudia hali hii. ‘Hakuna dawa’ umegeuka wimbo usiokuwa na mwisho kwenye zahanati nyingi , tena ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

Pamoja na watoto kuwekwa kwenye kundi la wanaopata tiba bure, inapofika suala la dawa, tofauti na Panadol, jibu ni ‘nenda kanunue kwenye duka la dawa’. Jibu hili huwakumba pia wanaotibiwa kwa bima.

Suala la kujiuliza, mgawo wa dawa na vifaa tiba hutolewa wakati gani kama kila anayekwenda kwenye zahanati za serikali huambiwa hakuna dawa isipokuwa Panadol?

Au dawa zinazopofikishwa kwenye zahanati ndio hugeuzwa biashara kwa watu kwenye maduka ya dawa? Hakika Wagosi wa Kaya wako sahihi kuhoji juu ya kodi tunazochangia kwa kusema ‘Haiwezekani bwana, huduma tunazichangia mbona hazijainuka’.

Licha ya ukosefu wa dawa, hoja ya Wagosi wa Kaya juu ya aina ya madaktari, pia ina mashiko. Wapo madaktari na wauguzi ambao hawana wito isipokuwa wanafanya kazi hiyo ili mradi tonge liende kinywani.

Wengine hata kwa mwonekano wao wanajibainisha kuwa walipotea njia kuingia kwenye taaluma hiyo. Mfano ni daktari ambaye jicho langu lilimuangaza nilipokwenda kwenye zahanati hiyo kupata huduma.

Sitakosea kumhukumu kwamba hakupaswa kufanya kazi hiyo bali angepewa kazi nyingine hususani ya kuuza sura. Daktari gani , tena mwanaume anayetumia mkorogo?

Ana umri wa makamo, lakini amejichubua ngozi, ni mweupe pee kasoro maeneo sugu kama viwiko na vidole, ndivyo vinamsaliti na kutambulisha kwamba ana weupe wa kununua.

Nilipomuona, nikakumbuka namna ambavyo wataalamu wa masuala ya afya, ikiwemo Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) wamekuwa wakisisitiza jamii kuachana na matumizi ya kemikali kubadili ngozi .

Nikajiuliza, je huyu daktari imemtokea kwa bahati mbaya au ni kwa makusudi? Jibu analo mwenyewe. Lakini ukweli ubaki kwamba, daktari huyu hana ubavu wa kushauri mtu juu ya afya ya ngozi hususani aliyeathirika kwa kujichubua.

Ukiacha suala hilo la kujichubua ambalo ni lake binafsi, kwenye huduma, daktari huyo pia haoneshi kabisa kama ana wito na kazi hiyo. Ukifika tu mlangoni, kabla hata ya kukaa, unapokewa kwa kuulizwa tatizo.

Kabla hujaongea, tayari ameshakuandikia vipimo vya malaria na haja ndogo. Usishangae una maumivu ya jino ukaandikiwa kupima malaria! Daktari akishaandika vipimo, huna nafasi tena ya kuelezea historia ya ugonjwa.

Huyu ndiye daktari aliyepewa dhamana ya kusikiliza na kutoa tiba sahihi kwa mgonjwa. Kwake saikolojia ya mgonjwa kaiweka kando, badala yake anatoa huduma ‘kiafande’.

Kinachosikitisha ni kwamba jamii imechukulia kero hizo kwenye zahanati, vituo na hata hospitali za umma kuwa ni sehemu ya maisha yao. Wamekubali kupatiwa huduma katika mazingira hayo magumu. Hakika hii ni hatari kwa sekta nyeti kama hii ya afya.

twessige@yahoo.com

Waziri Mkuu Mstaafu, ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi