loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JICHO LANGU: Mtoto mchanga na disko toto!

Wanaadhimisha kufufuka kwa Bwana wao Yesu Kristo. Kusulubiwa, kufa, kuzikwa na kisha kufufuka siku ya tatu, ni ukombozi mkubwa kwa Wakristo. Hivyo hii ni sikukuu kubwa kwao.

Ukubwa wa siku ya leo, unaanzia kwenye nyumba za ibada hadi majumbani. Nyumba za ibada, zimefurika tofauti na Jumapili za kawaida.

Inawezekana mwingine tangu mwaka uanze hakuwahi kukanyaga kanisani. Lakini ikifika Pasaka au Krismasi, anakuwa miongoni mwa washiriki wa ibada.

Inapofika suala la mahudhurio kanisani kuwa makubwa kupita siku za kawaida, hapo wengi hujiuliza: Hawa waumini wote siku za kawaida huwa wamejificha wapi?. Bila shaka swali hili, wahusika wana majibu yake.

Si jukumu langu kulijibu. Maana naweza kujikuta nakwaza wengi. Nikijaribu kujibu, inawezekana nikahukumu kwa kusema watu wa namna hiyo wanafuata mkumbo tu.

Pia nachelea katika majibu nisijekusema watu wa namna hiyo wanakwenda kuonesha mavazi. Sitaki kujibu kwani naweza kujikuta nikiwaambia watu wa namna hiyo wanakwenda kwenye ibada kuweka miadi.

Vile vile naweza kuwakwaza kwa kusema ni wasindikizaji wa ‘waumini kamili’. Jambo moja ninaloweza kusema, ni kwamba wao pia huhitaji upako na baraka za siku hii ambayo hutawaliwa na shamrashamra za kila aina.

Shamrashamra hizo ni pamoja na nyimbo, maigizo, shangwe na vigelegele. Vile vile ibada zimepambwa kwa mahubiri yanayohimiza kuadhimisha siku hii kwa kutenda mema.

Huambiwa kula, kunywa na kuvaa si chochote si lolote; Isipokuwa roho. Nikiacha nyumba za ibada, katika nyumba za waumini, Pasaka inajidhihirisha katika mlo, mavazi na hata mapambo.

Pilau ndicho chakula kikuu cha siku kwa asilimia kubwa ya watu. Mitaani nako, jicho langu linaangaza kumbi za starehe, hususani baa, ambazo pia zimefurika watu wanaojinasibu kuwa wanasherehekea Pasaka.

Pia naambiwa nyumba za wageni, hujaa ‘washerehekeaji’. Sina hakika kama nyumba hizo hujaa wageni kama ilivyo lengo lake, au hujaa ‘wageni wenyeji’? Wahusika wanalo jibu.

Sina haja ya kuingilia mambo binafsi ya watu. Pia nabaini uwepo wa kumbi zinazojinasibu kupiga muziki kwa ajili ya watoto maarufu kama disko toto. Disko toto limekuwa maarufu tangu zamani.

Siyo tu kwa Pasaka, bali hata sikukuu nyingine za kidini; hususani za dini mbili (Waislamu na Wakristo) zilizo maarufu nchini. Bahati mbaya, baadhi ya wazazi na walezi hukwepa wajibu wa usimamizi wa usalama wa watoto.

Zipo familia ambazo huamua kukaa pamoja. Lakini nyingine, baba na mama huenda kivyao na watoto husherehekea kivyao mitaani. Baadhi ya wazazi na walezi, huwaachia watoto wajiongoze bila kujali umri wala mazingira waliyomo.

Licha ya suala la usalama wa watoto kuwa nyeti, jambo la kushangaza ni kuona watoto chini ya umri wa miaka mitano, wakiwa ama peke yao au na mwangalizi ambaye pia ni mtoto.

Unakuta mtoto huyo wa miaka mitatu akiwa na mwenzake wa miaka sita, wakiongozana kwenda kwenye disko toto. Hivi kweli kwa umri huu, usalama upo? Laiti kama lingekuwa disko toto kama ilivyo jina lake!

Lakini tatizo linakuja, ndani yake, wamo pia vijana wakubwa ambao inadaiwa baadhi hudiriki hata kuingiza vileo. Hii huhitaji kuingia ndani ya ukumbi kushuhudia, bali ukipita nje ya kumbi husika, utabaini aina ya disko toto linalochezwa.

Mara nyingi wahusika wa kumbi hizi, wametanguliza fedha kuliko malengo ya kutoa burudani kwa walengwa ambao ni watoto. Ndiyo maana Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imepiga marufuku disko toto baada ya kubaini kumbi mbalimbali hazina sifa zinazokidhi viwango vya usalama wa watoto.

Ingawa kila mwaka kumekuwepo matamko ya polisi kukataza madisko haya, utekelezaji wake ni mdogo. Ni jukumu la wazazi na walezi kufuatilia usalama wa watoto wao wakati wa sikukuu kama hizi.

Wazazi na walezi wanapaswa wakumbuke majanga yaliyowahi kutokea kwenye kumbi hizo za disko toto na kugharimu maisha ya watoto. Itakumbukwa tukio mojawapo ambalo watoto wawili walikufa kwa kukanyagana katika ukumbi mmoja jijini Dar es Salaam.

Pia itakumbukwa vifo vingine viliwahi kutokea mkoani Tabora baada ya watoto kusongamana na kukosa hewa katika ukumbi wa disko toto. Siyo tu kwa disko toto, bali pia ufukweni na barabarani.

Si haki na ni uzembe wa aina yake, kukuta mtoto mchanga akiwa amebebwa na watoto wenzake wakiingia disko toto.

Pamoja na haki ya kusherehekea, kufurahi na kuburudika waliyo nayo watoto, wazazi wabebe jukumu la kusimamia kuhakikisha wanakuwa na waangalizi watu wazima kuepuka Pasaka kugeuzwa kuwa kumbukumbu ya maafa. twessige@yahoo.com

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Riadha ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi