loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JICHO LANGU: Wanajimaliza kwa mkorogo wa jiki

Katika kipindi kilichoelimisha juu ya vipodozi hatari, kwenye televisheni ya TBC 1, niliona jinsi mkorogo unavyotengenezwa mitaani. Ngoja sasa nieleze kile ambacho jicho langu lilishuhudia. Mtengenezaji wa mkorogo hakuficha.

Alikutwa maeneo ya Buguruni, jijini Dar es Salaam. Hakuwa na wasiwasi wala hofu ya kuonesha namna anavyochanganya krimu, losheni, sabuni na kemikali nyingine hatari kwa ajili ya kupata mkorogo husika.

Alichukua krimu kadhaa zikiwemo zilizopigwa marufuku; zenye viambata vya sumu vya hydroquinone na mercury. Akaminya kwenye kifaa cha kukorogea. Mama huyo pia alichukua sabuni kadhaa; miongoni mwa ninayokumbuka ni Rico.

Ambayo pia ilipigwa marufuku na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania ( TFDA) kwa sababu ina viambata vyenye sumu. Aliendelea na uchanganyaji.

Nilipigwa butwaa alipochukua kemikali ya kuondoa madoa kwenye nguo; maarufu kama Jiki na kuimimina kwenye mkorogo wake. Akatoa maelezo kwamba, jiki ni kemikali inayosaidia kuondoa madoa kwenye nguo,hivyo kutokana na kazi hiyo, anaiongeza kwenye mkorogo wa kujipaka kwenye ngozi ili isaidie kuondoa madoa kwenye ngozi.

Mpaka hapo upo wewe mtumiaji wa mkorogo? Alizidi kunistaajabisha pale alipochukua vidonge vya kutibu malaria vya ALU pamoja na vidonge vya kuongeza Vitamini. Alivitwanga kwenye kinu, halafu unga wake akauongeza kwenye mkorogo. Baada ya kumaliza kukoroga, akamimina kwenye kopo dogo ambalo kwa mujibu wake, huuzia wateja wake kwa Sh 10,000. Wakaoneshwa wateja wanaonunua kipodozi hicho kwa lengo la kuondokana na weusi wa ngozi. Aliyeandaa kipindi hicho, hakuishia kwa watengeneza mkorogo wa ngozi. Bali pia akawonesha wanaotengeneza ‘dawa’ za nywele. Katika kipindi hicho, ilioneshwa saluni moja iliyoko Buguruni ambako mmiliki wa saluni hiyo anatengeneza dawa feki kwa kutumia kemikali mbalimbali na kuwekea wateja wake. Pamoja na vitu vingine alivyochanganya, nilishtuka kuona anaweka sabuni ya unga pamoja na asidi na kuvichemsha. Hata hivyo hakuficha ukweli juu ya ‘dawa’ hiyo kwa kusema inasifika kwa kubabua ngozi. Kutokana na sifa hiyo ya kuunguza na kuleta maumivu, wameibatiza jina la ‘Uchungu wa mwana…’. Baada ya jicho langu kushuhudia haya yote, nikaanza kutafakari. Nikabaini lipo kundi kubwa la watu wasio na uelewa hata kidogo juu ya madhara ya kemikali na vipodozi vinavyodhuru mwili. Watu hawa hawana taarifa yoyote juu ya hadhari zinazotolewa na mamlaka mbalimbali juu ya madhara ya kemikali hususani zenye viambata vya sumu. Ndiyo maana hawaoni hata hofu ya kujionesha hadharani kwenye televisheni wakitengeneza na kuuza mikorogo kama hiyo ambayo ni hatari kwa mwili wa binadamu. Lakini pia lipo kundi lingine ambalo licha ya kuelewa, tena wakiwemo wasomi, wameamua kujibandika majina ya ‘Sijali’. Hawajali chochote zaidi ya urembo. Kwa mtazamo wao kujipodoa ndiyo kila kitu. Kwa gharama yoyote, wanataka dhamira yao ya kuwa weupe itimie. Wanaamini kuchubua ngozi, kwa maana ya kubadilika kutoka rangi nyeusi kwenda nyeupe ndiyo mpango mzima. Hawaamini katika kubaki na ngozi ya asili. Katika kundi hili wanawake ndiyo wengi na wamejikuta wakishabikia ‘weupe wa kutengeneza’. Ingawa wapo baadhi ya wanaume waliojiingiza katika kundi hili na jamii inawashangaa zaidi. Japo kundi hili linaelewa madhara ya kujichubua, wao huona sawa. Hawajali madhara yaliyo mbele yao ikiwemo kuzeeka mapema na hata uwezekano wa kupata saratani ya ngozi. Wanachojali ni kuona leo wanapendeza, wanang’aa na kuwavutia wale wanaopendelea rangi nyeupe. Kesho ya madhara hawataki kuisikia. Hujiliwaza kwamba kama ni saratani, hata wasiotumia vipodozi wameathirika na ugonjwa huo. Hata hivyo, mamlaka zinazohusika kuelimisha na kudhibiti matumizi mabaya ya kemikali, zisikate tamaa. Ziendelee kutoa elimu juu ya matumizi salama ya vipodozi. Ziingie hata mitaani, ziongee ana kwa ana na jamii. Jamii nayo izingatie ushauri wa wataalamu katika matumizi ya vipodozi. Mamlaka zihadharishe juu ya utengenezaji wa vipodozi kienyeji. Lakini pia, zihimize vipodozi asilia. Bila kufanya hivyo, jamii itaendelea kujimaliza kwa mikorogo ya jiki. twessige@yahoo.com

Naamka asubuhi,  sioni kilongalonga, 
Napapasa kitandani,  hamadi hiki hapa,  

foto
Mwandishi: Stellah Nyemenohi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi