loader
Picha

JICHO: Mazingira ya shule zetu yanamjali mtoto wa kike?

Makongamano, midahalo na semina zimetumika, lengo likiwa ni kuangalia namna ya kutatua changamoto zinazomkabili mtoto wa kike. Kabla jicho langu halijaangaza ujumbe mbalimbali uliotolewa katika kuadhimisha siku hii, ni vyema nikumegee jinsi ambavyo nchini Uganda, Rais Yoweri Museveni aliadhimisha.

Rais Museveni alimteua mtoto mwenye umri wa miaka 11 kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Uganda kwa siku moja. Mtoto huyo, Elizabeth Atukunda wa darasa la sita katika shule ya msingi Kampala Parents, alikaimu majukumu ya IGP, Kale Kayihura.

Elizabeth alikabidhiwa ripoti ya utendaji kutoka kwa mkuu huyo wa polisi kisha akakagua gwaride. Baada ya kumalizika maadhimisho, uteuzi huo ulitenguliwa na nafasi kuchukuliwa tena na Kayihura. Tukio hili ambalo linaweza kuchukuliwa kama igizo, si la kubeza.

Limeonesha thamani ya siku hii nchini humo. Lakini pia siku hiyo, Oktoba 11, hapa nchini iliadhimishwa kwa njia tofauti. Kitaifa ilikuwa wilayani Tarime. Hotuba za watu wa kada mbalimbali zilihimiza utatuzi wa changamoto zinazokatisha ndoto za watoto wa kike kufikia malengo yao.

Mimba za utotoni, ukeketaji, ubakaji na miundombinu hafifu kama vile ukosefu wa vyoo na maji shuleni, yakawa miongoni mwa mambo yaliyomulikwa kuwa vikwazo kwa mtoto wa kike. Kuhusu mimba za utotoni, zikapazwa sauti nyingi dhidi ya wanaume wakware wanaowarubuni watoto na kufanya nao vitendo vya ngono.

Mbunge wa Viti Maalumu, Mama Salma Kikwete ni miongoni mwa waliotoa sauti kukemea wanaume wa namna hiyo. Akawasihi watoto wa kike kutambua thamani yao. Uchungu wa mama Kikwete aliyehudhuria maadhimisho mkoani Pwani, ulizingatia hali ya mkoa huo ulio katika orodha ya mikoa 10 yenye tatizo la mimba za utotoni.

Kuhusu ulinzi na usalama wa mtoto, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametoa miezi sita kwa shule zote za msingi na sekondari kuanzisha madawati ya ulinzi na usalama wa watoto. Agizo hilo la Waziri Ummy alilitoa wilayani Tarime kwenye maadhimisho ya kitaifa.

Lengo ni kuhakikisha watoto wanakuwa salama na wanapata sehemu ya kueleza changamoto na matatizo yanayowakabili. Kwa kuzingatia changamoto hizo kwa mtoto wa kike, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF), Maniza Zamani akawasihi viongozi wa kimila na dini kuangalia na kuwasaidia watoto wa kike.

Ikiachwa wadau waliowasemea watoto, pia watoto wenyewe walipata fursa ya kuanisha matatizo yanayoathiri ustawi wao kijamii na kitaaluma. Kwa mfano, mkoani Shinyanga katika maadhimisho ya kimkoa, watoto walitaja changamoto zinazowakabili ni mila potofu, kubakwa na kuozwa ili wawe chanzo cha mapato cha familia.

Katika risala ya watoto hao iliyosomwa na Rosemary Richard, pia wakaomba kila shule itengewe vyumba maalumu kwa ajili ya kujisitiri wanapokuwa katika hedhi. Ombi hili likanikumbusha suala zima la mazingira rafiki kwa mtoto aliye katika hedhi.

Kumekuwa na sauti nyingi za wadau zinazohimiza watoto wa kike hususani wanaotoka familia zenye kipato cha kawaida, kuwezeshwa kupata taulo bora za kike. Tujiulize, Je, ni shule ngapi zina maji ya kutosha kiasi cha wanafunzi walio kwenye hedhi kubaki katika hali ya usafi tangu asubuhi hadi jioni?

Je, wanafunzi wanaotumia vitambaa, wanapata wapi nafasi ya kuvifua na kuanika wawapo shuleni? Haya ni sehemu ya mazingira yanayohitaji kuboreshwa kwa ustawi wa kijamii na kitaaluma kwa mtoto wa kike awapo shuleni. twessige@yahoo.com

JUZI iliibuka taarifa katika mitandao ya kijamii juu ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi