loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

JK aahidi kuisukuma NHC kujenga nyumba Chemba lakini…

Alitoa agizo hilo juzi wakati akiwa katika ziara ya kutembelea wilaya hiyo mpya ambapo pia alifungua jengo la ofisi ya mkuu wa wilaya na kusalimiana na wananchi.

Rais Kikwete alisema iwapo halmashauri hiyo itatoa viwanja nyumba zitajengwa na NHC na watumishi kuondokana na tatizo la ukosefu wa nyumba.

“Tengeni viwanja, wapeni NHC watajenga nyumba, wafanyakazi watapata nyumba haraka hawataendelea kuishi Kondoa au kwenye nyumba ambazo hazilingani na wao,” alisema.

Alisema wakishatenga eneo hilo atafanya kazi za kuwasisitiza NHC ili waweze kujenga nyumba haraka ili watumishi hao wapate nyumba za kuishi.

Alisema Chemba ni miongoni mwa wilaya 19 zilizoundwa na mahitaji yake ni mengi, lakini serikali itafanya jitihada kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Alisema Serikali itaendelea kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji jitihada kuhakikisha mahitaji muhimu yanapatikana haraka. Pia aliutaka uongozi wa halmashauri hiyo kuongeza juhudi kwani ufaulu uko chini sana ambao ni asilimia 19.

Alisema wataendelea kusaidia suala la upatikanaji wa walimu na kuboresha maisha yao na sasa fedha zimetengwa kwa ajili ya mkakati wa kujenga nyumba za walimu.

Naye Mbunge wa Chemba ambayo awali ilijulikana kama Kondoa Kusini, Juma Nkamia alisema kijiografia kabla wilaya hiyo haijagawanywa ilikuwa kubwa kuliko Mkoa wa Kilimanjaro.

Alisema katika kipindi cha uongozi wa Rais Kikwete ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imetekelezwa kwa asilimia kubwa, hali iliyofanya huduma mbalimbali kuboreshwa.

Alisema baada ya Serikali kutenga kiasi cha Sh bilioni tatu za kufufua na kusambaza maji kutoka chanzo cha Ntomoko tatizo la maji katika vijiji vingi litakuwa historia.

Mbunge huyo alisema katika vijiji vingi miradi ya maji inaendelea na vijiji zaidi ya 30 vitapata umeme awamu ya kwanza ya Mradi wa Umeme Vijijini (REA).

Alisema changamoto zilizopo ni makao makuu ya wilaya kuwa na kisima kimoja ambacho hakitoshi na hakipo katika ubora unaohitajika. Alisema kukamilika kwa bwawa la Farkwa kutasaidia pia kusambaza maji mjini Chemba na baadhi ya vijiji vya wilaya hiyo.

Alisema katika Kijiji cha Machiga na vijiji vya Pamamba na Itolo pipa la maji limekuwa likiuzwa Sh 10,000 hali inayofanya wananchi kutumia muda na gharama kubwa kutafuta maji. Pia alitaka serikali kupatia ufumbuzi suala la mgogoro wa ardhi mpakani mwa wilaya hiyo na Kiteto ambao mara nyingi huzuka wakati wa kilimo.

Wakati huo huo, Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe amesema Serikali inafanya jitihada ili kuhakikisha Wilaya Mpya ya Chemba mkoani Dodoma inakuwa na vyanzo vya uhakika vya maji.

Alisema matunda ya juhudi hizo ni pamoja na miradi ya maji katika wilaya hiyo mpya kwenda vizuri na mradi wa Ntomoko unakaribia kukamilika.

Alisema Wizara ya Maji imetoa Sh bilioni tatu kwa ajili ya kuvipatia maji vijiji vingi vya Wilaya ya Chemba na Kondoa ambapo mradi huo unatarajia kuzinduliwa kati ya Desemba mwaka huu au Januari mwakani.

Alisema katika mradi wa vijiji 10 na mradi wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) miradi mingi imefikia asilimia 90 kukamilika. Alisema serikali pia kuanzia wiki ijayo inafanya maandalizi ya uchimbaji wa visima viwili kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa maji Chemba Mjini.

Akizungumzia ujenzi wa bwawa la Farkwa alisema mhandisi mshauri anafanya kazi ya usanifu. “Kazi inayofanyika ni usanifu wa mazingira na Benki ya Maendeleo ya Afrika wameonesha nia tukimaliza kazi ya usanifu watazungumza na sisi,” alisema.

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi