loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JK aungwe mkono kutimiza malengo

Tayari Rais Kikwete ameweka wazi kwamba yeye atakuwa Rais wa mwisho, kuongoza nchi masikini na ajaye atakuwa mmoja wa marais wa nchi tajiri.

Malengo yake haya yatatimia, kama Watanzania wote kwa nia moja, watamsaidia kutimiza malengo haya anayoyabainisha. Hii ni kazi kubwa, ambayo haikuja kwa siku moja.

Rais Kikwete amefanya juhudi kubwa katika utawala wake, kwa kuweka mikakati ya utajiri huo, ikiwa ni pamoja na kutumia wataalamu na watafiti, kuhakikisha rasilimali zilizopo hapa nchini, zinawanufaisha Watanzania wote.

Kwa mara ya pili sasa, Rais Kikwete amenukuliwa akinadi suala zima la kumwachia rais ajaye utajiri wa nchi, jambo ambalo linaleta faraja kwa Watanzania ambao kwa muda mrefu wamekaa katika lindi la umasikini wa kupata wastani wa mlo mmoja kwa siku.

Akiwa nchini Marekani hivi karibuni, Rais Kikwete alisema atakuwa Rais wa mwisho wa Tanzania masikini, huku akisisitiza kwamba muda wake uliobaki Ikulu, utakuwa ni wa kumwandalia mazingira mazuri rais ajaye.

Na juzi akiwa mkoani Morogoro, wakati akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara ya lami ya kutoka Magole hadi Turiani, Rais alisisitiza juu ya hilo, huku akisema kwamba alipokuwa akiingia madarakani, aliahidi kwamba nchi nzima itapitika kwa lami, na hilo limewezekana.

Rais alisema barabara zilizokuwa na lami kabla ya Uhuru mwaka 1961, zilikuwa zile tu ambazo Wakoloni walikuwa na faida nazo. Alitoa mfano wa barabara hizo kuwa ni ya kutoka Morogoro hadi Dar es Salaam na Tanga hadi Dar es Salaam.

Alisema maeneo hayo yalikuwa na mashamba ya mkonge. Alisema barabara zingine zilijengwa mahali ambako wakoloni waliishi. Alisema baada ya uhuru barabara nyingi zilijengwa, na nyingi zaidi katika kipindi cha uongozi ulioanza mwaka 2005.

Rais Kikwete alisema wapo waliobeza ahadi zake za kutaka kuunganisha nchi kwa barabara za lami. Lakini, alisema watu hao sasa wameona ukweli wa ahadi zake.

Hivyo, inabidi pia tusishangae watu walioanza kujitokeza sasa na kubeza kauli yake, anaposema yeye ni Rais wa mwisho wa Tanzania masikini. Ukweli unajidhihirisha kwa kuangalia viashiria vya utajiri anaousema Rais.

Kuwepo kwa gesi na maendeleo ya ujenzi wa njia ya mabomba ya gesi hiyo yalipofikia, vinatosha kutoa picha kamili kwamba Rais ajaye atakuwa na mahali pazuri pa kuanzia. Kila Mtanzania anafarijika na hatua iliyopo sasa.

Ni vizuri kukumbuka kwamba maendeleo ya mtu au nchi, hayaji kwa siku moja. Ni lazima iwepo mikakati ya makusudi, na hili ndilo tunaloliona sasa.

Nchi zote tajiri duniani, zikiwamo zinazotegemea mafuta, zilianza kwa kuweka mikakati kuanzia upimaji na ugunduzi wa maeneo yenye mafuta hayo na jinsi ya kuchimba.

Baada ya kuweka wazi mikakati hiyo, nchi hizo sasa ni tajiri kwa kutegemea rasilimali zilizopo ardhini, jambo hilo ndilo analolifanya Rais Kikwete.

Kama kuna anayepinga au kubeza kauli za Rais, basi mtu huyo ana lake jambo na Watanzania wa sasa wanaelewa, wanapima na kujua ukweli.

Ni wajibu wa kila mmoja wetu, kuanzia mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa na wilaya, makatibu kata na vijiji na wananchi wenyewe, kumsaidia Rais kutimiza lengo lake, kwani mafanikio ya utawala wake ni faida ya Watanzania wote.

Maonesho ya 44 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba, ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi