loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JK- Soko la mpunga, mahindi litapatikana

Pamoja na kuwahakikishia kuwepo kwa soko hilo, pia Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kuanzia mwaka huu imetenga fedha za kununua mpunga tani 10,000, ikiwa ni hatua ya awali.

Rais Kikwete alisema hayo wakati wa mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mwaya kata ya Mwaya wilayani Ulanga, baada ya kuwasili juzi kuanza ziara ya wiki moja mkoani Morogoro.

Alisema kilio cha wakulima cha ukosefu wa soko, kimechangiwa na uingizaji wa mchele mwingi kutoka nje ya nchi na uzalishaji wa mpunga katika mikoa mingi, umekuwa wa kiwango cha juu miaka ya karibuni, hivyo kusababisha uhaba wa soko la ndani.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, kutokana na changamoto hiyo, Serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutafuta soko la nje.

Alisema aliwatuma mawaziri wake kwenda Sudan Kusini kutafuta soko la mpunga na matunda yake ni mazuri.

“Uzalishaji umeongezeka sana, tunajaribu kutafuta soko la mchele ...nimewatuma mawaziri kwenda Sudan Kusini kutafuta soko kwa vile wenzetu wana njaa, tumefanya mazungumzo ya kuona namna ya kuwasaidia kuwauzia mchele, pia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula, licha ya kununua mahindi tu hata mchele watanunua,” alisema Rais Kikwete.

Mbali na kuzungumzia soko la mazao hayo, Rais alisema Mkoa wa Morogoro aliuteua kuwa miongoni mwa mikoa inayounda ghala la Taifa la Chakula, kutokana na kuwa na mabonde mengi yenye rutuba na mvua za kutosha na Wilaya ya Kilombero na Ulanga ni za uzalishaji wa mpunga, utakaotosheleza taifa na ziada kuuzwa nje.

Alisema katika mpango wa kilimo cha umwagiliaji, lengo ni kufikisha hekta 100,000 za wakulima wadogo za umwagiliaji na kuendelea hadi kufikia kati ya hekta 200,000 hadi 350,000.

Alisema kinachofanyika na Serikali ni kujenga miundombinu ya maji ya umwagiliaji kwa kuwasogezea wakulima, ili wayavute hadi mashambani mwao. Kutokana na mpango huo, alisema anataka kuona mkoa huo unakuwa ghala kweli na Serikali itawekeza katika ujenzi wa maghala vijijini.

“ Mahitaji ni makubwa ya mchele na mahindi kwa ajili ya kusaidia nchi zenye njaa barani Afrika,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, ambaye ni Mbunge wa Ulanga Mashariki, aliwasilisha kero za wananchi kuhusu kukosekana kwa soko la mazao yao.

Pia, alitaja changamoto nyingine kuwa ni uvamizi wa wanyama kutoka Hifadhi ya Taifa ya Selous kwa vile asilimia 75 ya jimbo hilo, limezungukwa na hifadhi hiyo.

Alimpongeza Rais Kikwete kwa kusimamia utekelezaji wa ahadi mbalimbali, alizozitoa wakati wa kampeni za uchanguzi wa 2005 kwa asilimia 90.

KAMPUNI ya uchimbaji ...

foto
Mwandishi: John Nditi, Ulanga

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi