loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Josho la mkoloni kivutio Mpwapwa

Wakazi wa Mpwapwa ni mchanganyiko wa makabila ya Wagogo, Wakaguru, Wahehe na makabila mengine madogo madogo. Ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 7,379 imegawanyika katika tarafa nne, kata 30, vijiji 84 na vitongoji 490. Miongoni mwa vivutio vilivyo katika Wilaya ya Mpwapwa ni josho la kwanza kujengwa Afrika Mashariki na Wajerumani mwaka 1905 ambalo limeendelea kutumika mpaka sasa.

Kwa mujibu wa Askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Mpwapwa, Simon Chiwanga, Wajerumani waliiona Mpwapwa kama eneo la kuwekeza kijamii na kiuchumi na ili kupata nyama nzuri na salama walianzisha kituo cha utafiti wa mifugo na kujenga josho.

Hata unapoliangalia josho hilo utagundua lilijengwa kwa ujuzi wa hali ya juu ambapo humfanya ng’ombe asitumie nguvu bali awe anateleza. Kwa jinsi josho hilo lilivyojengwa, baada ya ng’ombe kupita kwenye maji yenye dawa kuna sehemu ya kumkaushia. Hata majosho mengine yaliyojengwa miaka ya 1980 hayana ubora mkubwa ukilinganisha na josho hilo lililojengwa na Wajerumani.

Inaelezwa kwamba kudumu kwa muda mrefu kwa josho hilo kumechangiwa na ujenzi imara. Licha ya kujengwa kwa matofali ya kuchoma lakini uimara wake uko pale pale na sasa ni zaidi ya miaka 109 tangu kujengwa kwake.

Unapoongea na wenyeji wa maeneo hayo wanasema ujenzi waliokuwa wakifanya Wajerumani haulingani na ujenzi unaoendelea sasa kwani inaonekana walitumia utaalamu mkubwa, kulingana na hali ya mazingira ya maeneo husika na walidhamiria kujenga kitu cha kudumu kwa miaka mingi.

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (Taliri), Dk Daniel Komwihangilo anasema taasisi hiyo ilianzishwa na Wajerumani mwaka 1905 wakati huo ikiwa kama kliniki ya kutibu magonjwa ya mifugo na ndipo josho hilo likajengwa.

“Wajerumani hawakuacha kumbukumbu nyingi isipokuwa majengo kadhaa na josho la kwanza hapa Afrika Mashariki na Kati ambalo lilijengwa mwaka 1905 na hadi sasa bado linatumika,” anasema. Anasema tangu wakati huo taasisi hiyo imekuwa kitovu cha utafiti wa mifugo kitaifa na kimataifa ambapo mwaka 2005 iliadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake.

Dk Kamwihangilo anasema taasisi hiyo ipo kwenye ukanda wa ukame lakini milima inayozunguka taasisi hiyo inafanya hali ya hewa kuwa nzuri huku wastani wa mvua kwa mwaka ukiwa ni milimita 660 ingawa kiasi cha mvua na mtawanyiko wake hubadilika kati ya mwaka na mwaka.

Aidha anasema karibu asilimia 90 ya mvua hunyesha kati ya Desemba na Aprili na mara nyingi kipindi kifupi cha ukame hutokea mwezi Februari. Anasema maeneo mengi ya taasisi yana udongo mchanganyiko wa kichanga tifutifu na mengine hususan sehemu za milimani ni mchanganyiko wa mfinyanzi na kichanga chepesi.

Anasema udongo wa eneo hilo una upungufu wa nitrogen na phosphorous na una kiwango cha juu cha potassium. Kwa kiasi kikubwa uoto wa asili una aina mbalimali za nyasi, vichaka na miti aina nyingi za asili ikiwemo vichaka na miti aina ya acacia, cassia, grewia na commiphora kwa lugha za kitaalamu.

Anafafanua kuwa Taliri inajumuisha vituo vya Mpwapwa, Mabuki, Naliendele, Kongwa, Tanga, Uyole na West Kilimanjaro ambavyo vipo katika maeneo tofauti na maalum ya kiikolojia kuwezesha tafiti mbalimbali za uzalishaji endelevu wa mifugo. Anasema umuhimu wa utafiti unaonekana katika kuzalisha aina bora ya mifugo, aina mbalimbali za nyasi na miti-malisho na vyakula vingine vya mifugo.

Aidha anasema utafiti unabainisha ni kwa namna gani wanyama na ndege wanaofugwa wanastahili kutunzwa ili walete tija kwa mfugaji mwenyewe na taifa kwa ujumla. “Utafiti katika nchi yetu unazingatia lengo la taifa katika kujitosheleza kwa chakula na kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kufuatana na Dira ya Maendeleo ya Taifa,” anasema.

Anasema utekelezaji wa kazi mbalimbali za utafiti wa uzalishaji na uendelezaji wa mifugo unategemea moja kwa moja upatikanaji wa fedha kutoka serikalini kupitia Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

Pia utafiti wa uzalishaji na uendelezaji wa mifugo unafanyika vyuoni na hata vijijini kwenye mazingira ya wafugaji kwa kuhusisha wataalam wa fani mbalimbali wakiwemo wale wa uzalishaji wa koo za mifugo na aina za malisho, lishe ya mifugo, watafiti wa malisho na nyanda za malisho na pia wale wa sayansi ya jamii.

Maeneo yaliyotiliwa mkazo ni pamoja na uzalishaji na uendelezaji wa wanyama wanaocheua kama ng’ombe, mbuzi, kondoo, wanyama wasiocheua kama kuku na nguruwe na uendelezaji wa malisho sambamba na tafiti za lishe na ubora. Kaimu Mkurugenzi huyo anazitaja changamoto zinazokabili taasisi hiyo kuwa ni uvamizi wa maeneo ya taasisi unaofanywa na wananchi wanaoishi karibu na mashamba yao.

Anasema wananchi huyavamia wakitaka kulima, kuchunga na hata kujenga nyumba, hali ambayo hutishia usalama, lishe na afya ya mifugo ikiwemo pia usalama wa watumishi wa taasisi pale ambapo baadhi ya migogoro inapoelekea kwenye ugomvi. Anasema Taliri Mpwapwa imeshindwa kutumia eneo lake la Kiboriani kikamilifu, hali inayosababisha kusitishwa kwa tafiti zinazolenga uzalishaji wa mifugo na malisho katika nyanda za juu.

Anasema kutokana na kutotumika kwa shamba hilo taasisi inashindwa kuhimili matatizo makubwa ya utunzaji wa ng’ombe yanayotokana na upungufu wa malisho hasa wakati wa kiangazi. Pia anasema mfumo wa umiliki wa ardhi usiotilia mkazo uboreshaji wa nyanda za malisho unasababisha kukosekana kwa dhamira ya kuendeleza maeneo hayo kwa kupanda nyasi au mikunde bora inayopendekezwa.

Anasema taasisi hiyo imezungukwa na milima ambayo ni muhimu sana kwa vyanzo vya maji na uoto wa asili ambavyo ni muhimu, si kwa taasisi tu bali hata kwa maeneo ya mji na vijiji vinavyozunguka taasisi. Pamoja na kuwepo kituo cha utafiti wa mifugo katika wilaya hiyo bado mifugo mingi ni ya kienyeji ambayo haina uzalishaji wenye tija, hali inayofanya wafugaji kushindwa kufaidika na utajiri wa mifugo waliyonayo.

Kaimu Ofisa Mifugo wa Wilaya ya Mpwapwa, Herment Tumaini anasema ufugaji unaofanyika katika wilaya hiyo ni huria na kiasi kikubwa ni wa asili. Anasema wilaya inakadiriwa kuwa na ng’ombe 179,737, mbuzi 148,317, kondoo 56,343, nguruwe 3,102, mbwa 9064, punda 3,262 na kuku 204,923 na pia inakadiriwa kuwa mifugo inachangia asilimia 45 ya pato la wilaya.

Anasema uzalishaji wa maziwa kwa wastani unakadiriwa kuwa lita moja kwa siku kwa ng’ombe wa kienyeji japo kwa hali ya kawaida ng’ombe anayelishwa na kutunza vyema anatakiwa kuzalisha takriban lita sita kwa siku. Mtaalam huyo anasema ubora wa mifugo ni wa wastani kutokana na miundombinu michache kwa ajili ya kuzuia kuenea kwa magonjwa ya mifugo.

Pia anasema magonjwa yanayoshambulia na kuzuru afya ya mifugo yanapunguza uzalishaji na ubora wa nyama na maziwa. Akizungumzia suala la chanjo anasema Serikali imeendelea kupambana na magonjwa mbalimbali ya mifugo pamoja na kuchukua tahadhari juu ya magonjwa ya mlipuko ambapo wilaya iliweza kudhibiti ugonjwa wa bonde la ufa (RVF) uliotokea nchini mwaka 2007 na magonjwa mengine ya mifugo kwa kuipatia chanjo na kuiogesha.

Aidha ng’ombe wapatao 199,866, kondoo 37,833, mbuzi 85,023, mbwa 14,841 na kuku 239,756 walipatiwa chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali katika kipindi cha 2006 hadi 2013. Tumaini anasema ng’ombe 222,109, kondoo 60,824, mbwa 9,398 waliogeshwa kwa ajili ya kuwakinga dhidi ya magonjwa yaenezwayo na kupe katika kipindi cha 2006 hadi 2013.

“Mifugo iliyo mingi ni ya kienyeji ambayo haina uzalishaji wenye tija hivyo idara ya mifugo kwa kushirikiana na taasisi ya Taliri imefanikiwa kusambaza madume bora 22 na majike 21 katika vijiji saba kwa ajili ya uboreshaji wa ng’ombe wa asili,” anasema. Vijiji hivyo ni Gulwe, Kibakwe, Godegode, Chogola, Winza na Makose.

Pia Majike yamesambazwa katika vijiji vitano vya Gulwe, Winza, Makose, Godegode na Chogola. Anasema lengo ni kuongeza nyama na maziwa ya asili kutoka lita mbili hadi lita 10 za maziwa kwa siku na nyama kutoka kilo 150 hadi kilo 250 kwa muda wa miaka miwili.

Akielezea mafanikio alisema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita wamefanikiwa kuzalisha ndama 1260, kupandisha kiwango cha maziwa kutoka lita mbili hadi sita kwa siku na nyama kutoka kilo 150 hadi kilo 200 katika kijiji cha Chipogoro, na mkulima ameweza kufaidika na mradi wa kuongeza kipato na lishe kwenye kaya.

TANZANIA imeridhia mikataba na matamko mbalimbali ya kimataifa yanayotoa haki ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi