loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JUMA MBIZO: Muziki ulimfanya atupwe jela miaka saba

Safari ya Mbizo katika muziki wa dansi ilianza muda mrefu na ni miongoni mwa walioanzisha bendi ya muziki wa dansi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ya Anga Anga. Hata hivyo, pamoja na kufanya mambo mengi katika kuendeleza muziki wa Tanzania kuanzia ule wa dansi, taarab na hadi mabonanza ya muziki na michezo, Mbizo alijikuta akifungwa jela miaka saba kutokana na masuala hayo ya muziki.

Kuratibu bendi:

Mbizo kwa njia moja au nyingine ameshiriki kuanzisha, kuratibu au hata kuongoza baadhi ya bendi za muziki na zile za taarab huku zingine ziking’ara na zingine kuibuka na kufa mara zinapoanzishwa. Baadhi ya bendi alizoshiriki kuzianzisha ni Anga Anga, ambayo ni bendi ya JWTZ walianzisha wakiwa masomoni China mwaka 1975, ambapo wanafunzi wa kila nchi walitakiwa kuanzisha bendi au vikundi vya sanaa.

“Tulipokuwa katika masomo ya kijeshi nchini China wanafunzi wa kila nchi walitakiwa kuanzisha kikundi chao cha muziki au ngoma ili kutoa burudani pale chuoni na sisi tulianzisha Anga Anga na huo ndio ukawa mwanzo wa bendi hiyo hadi sasa,” anasema Mbizo.

Anasema, bendi hiyo walianzisha pamoja na Zacharia Hans Pope ambaye kwa sasa ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, wakati huo walisoma wote China. Mbizo pia alishiriki kuanzisha bendi za MK Group, MK Beats na MK Sound, ambapo bendi mbili za kwanza yeye (Mbizo alikuwa akiziongoza huku MK Sound aliianzisha kwa ajili ya kuwa na waimbaji Wakongo.

Katika bendi hiyo alikuwemo Nyoshi El Saadat, Noseke, Wilii, Katozi, Bakunde, ambao waliendesha bendi hiyo huku zile mbili za kwanza zikawa zinaundwa na Watanzania. Anasema, MK Sound baadae ikawa chini ya Asha Baraka na baadae ilipata mkataba wa kwenda kutumbuiza pamoja na Bozi Boziana Botswana na nchi zingine zilizopo kusini mwa Jangwa la Sahara.

Anasema, safari ya Bozi Boziana ilikuwa ikiishia Nairobi, Kenya na baadhi wa wanamuziki wa MK Sound ambao walikuwa wakimsaidia mwanamuziki huyo waligoma kurudi Tanzania na kung’ang’ania kubaki Nairobi. Pia alishiriki kuanzisha bendi ya Ngorongoro Heroes iliyokuwa na maskani yake katika ukumbi wa Bahama Mama, Kimara Dar es Salaam.

Katika miaka ya hivi karibuni, ndiye mwanzilishi wa kundi la taarab la Jahazi pamoja na Mashauzi Classic, ambayo yanatamba kwa sasa kwa upande wa muziki huo.

Bonanza la michezo:

Mbizo ndiye aliyeanzisha bonanza la soka la Old is Gold, ambalo lilikuja kuzaa timu ya Tanzania Stars iliyoundwa na wachezaji wengi waliowahi kuzichezea Yanga na Simba. Timu hiyo baadae ilikuja kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Kombe la Washindi, sasa Kombe la Shirikisho, na kuifunga Batter Bullet ya Malawi kabla ya kuondolewa na Mamelodi Sun Down ya Afrika Kusini.

Mbizo ndiye mwanamichezo wa kwanza kuanzisha bonanza la michezo lililowashirikisha wachezaji wa zamani wa Simba na Yanga waliowahi kuichezea timu ya taifa ya Tanzania. Anasema tamasha hilo lilifanyikia kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku mgeni rasmi akiwa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.

Baadae Uganda waliandaa bonanza la Afrika Mashariki na kuzialika timu za Kenya na Tanzania, huku Tanzania ikifikia katika fainali ambayo timu hiyo ya Tanzania ilishindwa kuibuka na ushindi na kuambulia nafasi ya pili.

Kufungwa jela:

Pamoja na mazuri yote aliyoyafanya kuuendeleza muziki, Mbizo alijikuta akihukumiwa kwenda jela miaka saba baada ya kukutwa na hatia ya kuwazuia wanamuziki wa bendi ya Empire Bakuba iliyokuwa chini ya Kabasele Yampanya, ‘Pepe Kale’ (marehemu). Ilikuwaje hadi alijikuta akitupwa jela miaka hiyo saba?

Mbizo anasema, wakati huo alikuwa akifanya kazi katika hoteli moja jijini Dar es Salaam huku akiwa mjumbe wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA). Miaka ya 90, bendi ya Empire Bakuba ilipokuja nchini kutokana na jitihada za Mbizo, bendi hiyo ilifikia Friends Corner na baada ya maonesho kadhaa ya muziki ilitakiwa kuondoka, lakini bahati mbaya waliyoileta walikuwa hawajakamilisha malipo ya malazi hotelini hapo.

Mwenye hoteli alibaini kuwa kundi hilo la muziki likiwa na nyota wake lilikuwa linaondoka kurudi Kongo (DRC) ambako wiki inayofuata walikuwa na shughuli ya mtoto wa aliyekuwa rais wa nchini hiyo, Mobutu Seseseko, hivyo aliamua kulizuia gari lililobeba wanamuziki hao.

Mbizo anaendelea kusema kuwa, gari hilo la wanamuziki wa Empire Bakuba chini ya Pepe Kalle liliendelea kuzuiliwa na kusababisha kuchelewa ndege huku kukiwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya nyota wake kama Bileku Mpasi. Sakata hilo lilitua ubalozi wa Kongo na suala hilo likawa zito, hatimaye likatua katika vyombo vya sheria na hatimaye mahakamani, ambako Mbizo ndiye alikuwa mtuhumiwa badala ya bosi wake aliyemtupia mzigo Mbizo.

Hukumu ilisomwa katika mahakama ya Kivukoni na Mbizo alipatikana na hatia ya kuingilia kazi ya idara ya Uhamiaji na kumtupa gereza la Ukonga kwa kifungo cha miaka saba. Baada ya kutumikia kifungo cha miezi sita jela, Mbizo alikata rufaa na hatimaye Mahakama Kuu ilimwachia huru na kurudi uraiani.

Changamoto za kifungo:

Mbizo anasema, pamoja na kufungwa jela lakini hakuacha shughuli za muziki kwani anaona ilikuwa kama moja ya changamoto katika kazi yake hiyo anayoipenda sana. Anasema, kila kazi ina changamoto zake na kwake kifungo ni changamoto katika kazi yake hiyo na kilimfanya kuzidi kuipenda kazi yake hiyo.

“Kila kazi ina changamoto zake na hii yangu ya muziki kile kifungo ndio moja ya changamoto na wala haikunikatisha tamaa hadi sasa bado ni mdau wa muziki,” anasema Mbizo katika mahojiano na mwandishi wa makala haya hivi karibuni.

Kuhama Makundi:

Kawaida Mbizo amekuwa sio mtu wa kukaa muda mrefu katika kundi moja au mahali pamoja na inatokana na kutakiwa na makundi mengi. Anasema, endapo kama atakaa kwa muda mrefu katika kundi moja, basi atashindwa kupata muda wa kuyaendeleza makundi mengine na kufanya watu kumuona kama mtu asiyetulia mahali pamoja.

“Kuhamahama kwangu kuna sababu kubwa sana, kama nisingekuwa nafanya hivyo basi ningekosa muda wa kuyaendeleza makundi mengine ya muziki,” anajitetea Mbizo sababu za kutodumu kwa muda mrefu mahali pamoja.

MKUU wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Godwin ...

foto
Mwandishi: Cosmas Mlekani

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi