loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kadi nyekundu ilivyopunguza vifo vya wazazi

Wakati ikiwa na umuhimu mkubwa kwenye viwanja vya michezo, kadi nyekundu imegeukia suala la vifo vya wajawazito na watoto wachanga ambapo kituo cha afya Nguruka wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma imeamua kutumia kadi hiyo kwa mtindo wa aina yake. Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya cha Nguruka, Stanford Chamgeni, katika mahojiano na gazeti hili anasema kuwa imeitwa kadi nyekundu kulingana na rangi ambayo kadi hiyo imetumika kuitengenezea lakini haina uhusiano na kadi ile ya uwanjani.

Chamgeni anasema katika kukabiliana na vifo vya wajawazito na watoto wachanga, wameona wabuni kadi hiyo ambayo itakuwa inatumiwa na wajawazito wakati wa kuanza kuhudhuria kliniki hadi anapojifungua.

Mganga huyo Mfawidhi anasema kwa sasa kadi hizo nyekundu zimekuwa zikitolewa kwa wenyeviti wa vijiji ambao huwakabidhi wajawazito na kutoa maelekezo kwamba kila anapoenda kliniki ahakikishe anakwenda na kadi hiyo.

Akiwa kliniki, kadi hiyo pia huwekwa saini na mhudumu wa afya katika kliniki ya baba, mama na mtoto ambao ukaguzi hufanyika kuonesha kama kadi hiyo inafanya kazi inavyopaswa na hiyo ni kutokana na usimamizi wa viongozi wa serikali za vijiji.

Msimamizi wa huduma za baba, mama na mtoto katika kituo hicho, Florence Katalambula, anasema mjamzito anapopewa kadi hiyo maana yake yuko kwenye hatari na anapaswa kupata huduma hospitali au kituo cha afya hadi atakapojifungua.

Katalambula anasema kwa sasa kesi nyingi za operesheni na vifo kutoka vijijini zimeanza kupungua kutokana na matumizi ya kadi nyekundu na elimu wanayopewa.

Anasema kadi nyekundu wanayopewa pia huwatia hofu na kuacha uvivu wa kuhudhuria kituo cha afya wakati wote wa ujauzito hadi kujifungua.

Akizungumzia chimbuko la matumizi ya kadi hiyo Chamgeni anasema ilitokana na kufikiria mbinu ya kukabiliana na vifo vya wajawazito na watoto wachanga kutokana na uzembe wa kufika kliniki hasa kwa baadhi ya akina mama ambao ujauzito wao unagundulika kuwa na matatizo.

Anasema kabla ya kufikia uamuzi huo waliitisha kikao cha viongozi wa kada mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini ili kujadili suala hilo.

Anasema baada ya mkutano huo, kwa pamoja bila kujadili itikadi za vyama au dini walilibeba suala hilo na kulipeleka kwenye mikutano ya vijiji ya kata za jirani na kituo cha afya cha Nguruka.

Zaidi ya vijiji vitano kutoka zaidi ya kata tatu za tarafa ya Nguruka zinategemea kupata huduma za afya katika kituo hicho cha afya cha Nguruka ambapo takwimu zinaonesha kuwa karibu watu 94,833 wanapata matibabu katika kituo hicho cha afya.

“Kwa sasa kumekuwa na mafanikio makubwa katika matumizi ya kadi hiyo, kwani kampeni zilizofanyika zimewezesha kuwa na ongezeko kubwa la wajawazito kuwahi kliniki wanapopata ujauzito, lakini pia kuwahi kituo cha afya wakati wa kujifungua,” anasema Chamgeni.

Akizungumzia uanzishwaji wa kadi hizo nyekundu, Mkunga Mfawidhi wa kituo hicho, Beatrice Mtesigwa, anasema imetoa hamasa kubwa kwa wanawake kujitokeza na kuhudhuria kwenye vituo vya afya badala ya kwenda kwa wakunga wa jadi.

Anasema uwepo wa kadi nyekundu ulienda sambamba na kufanyiwa kwa ukarabati wa kituo hicho cha afya na kujengwa kwa chumba cha upasuaji mdogo kulikofanywa kwa ufadhili wa Shirika la World Lung Foundation ambapo watumishi wa kituo hicho walipatiwa pia elimu ya kufanya upasuaji mdogo.

Sambamba na hilo, anasema kuwa Shirika la World Lung Foundation limesaidia pia vifaa mbalimbali, ikiwemo kitanda cha kujifungulia wajawazito na mambo ambayo sambamba na kadi nyekundu yamechangia kuongeza hamasa kwa wajawazito kupata huduma katika kituo hicho.

“Kwa sasa vifo vimepungua sana kwa sababu miaka mitatu minne nyuma kulikuwa na idadi kubwa ya vifo vya wajawazito na watoto wachanga wanaokufa kwa uzazi pingamizi kukiwa na wastani wa vifo 10 kwa mwezi ambapo kwa takwimu za kuanzia mwaka 2012 hadi kufikia mwezi Juni ni vifo vya kina mama saba vilivyotokea,” anasema.

Pamoja na uhamasishaji huo na uboreshaji unaofanyika bado vifo vipo kwa baadhi ya akina mama kutokana na kuchelewa kufika kituo cha afya kwa ajili ya kujifungua, lakini wengine wanachelewa hata kuanza kliniki hadi wanapokuwa wamepata matatizo.

Wakizungumzia uwepo wa hamasa kupitia kadi nyekundu na uboreshaji wa kituo hicho baadhi ya akina mama waliofika kujifungua kituoni hapo, wamesema kwa sasa hamasa kwa jamii kujifungua kwenye kituo cha afya ni kubwa kuliko kwenda kwa wakunga wa jadi.

Esther Filbety na Paskazia Libenus, wakazi wa kijiji cha Nyangabo, tarafa ya Nguruka ambao walijifungua kwa kufanyiwa upasuaji wanasema kuwa uboreshaji na ujenzi wa chumba cha upasuaji imewapa faraja wajawazito wengi kujitokeza na kuhudhuria kituo cha afya kwa ajili ya kujifungua, lakini tatizo la kukosekana kwa damu kunapokuwa na dharura bado imekuwa changamoto kubwa kwao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji cha Nguruka, Yakubu Nzigamiye, amesema kadi nyekundu imekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza hamasa kwa mama wajawazito kuhudhuria kliniki lakini pia kuwahi wakati wa kujifungua.

Nzigamiye anasema kuwa kadi nyekundu imekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza kama si kuondoa kabisa uwepo wa vifo vya wajawazito na watoto wachanga katika kujifungua.

Mwenyekiti huyo anasema kuwa licha ya mafanikio hayo bado tatizo la upatikanaji wa damu ni tatizo, kwani anasema kuwa kunapokuwa na dharura ya kuhitajika kwa damu inabidi ndugu na jamaa watafutwe kwa ajili ya kutoa damu na hakuna vifaa kwa ajili ya kuhifadhia damu hadi itolewe mkoani Tabora.

Mwenyekiti huyo anasema kuwa tatizo la damu linaweza kuchangia kurudisha nyuma juhudi zao za kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto kwani wakati mwingine damu inaposhindwa kupatikana kwa haraka mgonjwa anaweza kufariki dunia.

Akizungumza maboresho makubwa yaliyofanywa na Shirika la World Lung Foundation kwenye kituo cha afya cha Nguruka, Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Beatrice Mtesigwa, anasema kuwa wakati kukiwa na idadi kubwa ya wajawazito wanaofika kituoni hapo kujifungua na kuanza kliniki mapema bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya uchache wa watumishi na hivyo kulazimika kufanya kazi kwa saa nyingi hasa katika wodi ya wazazi.

Baada ya kuonesha mafanikio katika kupunguza vifo vya wajawazito kwenye tarafa ya Nguruka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nguruka, Nicholous Kombe anasema kuwa mpango wa halmashauri yake ni kupeleka mpango huo katika maeneo mengine.

Kombe anasema kuwa viongozi wa vijiji na viongozi wa dini wamekuwa msaada mkubwa katika kufanikisha mpango huo na kwamba wanatarajia pia kwa siku za karibuni kuona namna ambavyo mpango huo wa kadi nyekundu utaweza kutekelezwa katika kata za Uvinza na Ilagara ili kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga.

Akieleza kampeni za kupunguza vifo vya wajawazito na watoto mkoani Kigoma, Mkuu wa mkoa huo, Issa Machibya analishukuru Shirika la World Lung Foundation kwa msaada mkubwa wa uboreshaji wa huduma za afya hasa katika kampeni ya kuboresha huduma za uzazi na kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga.

Machibya anasema kuwa ujenzi wa vyumba vya upasuaji katika vituo saba vya afya mkoani Kigoma na utoaji wa vifaa mbalimbali kulikofanywa na shirika hilo kumekuwa msaada katika kufanikisha malengo ya mkoa katika kudhibiti vifo vya wajawazito na watoto wachanga.

Mapema hivi karibuni, Waziri wa Afya, Dk Seif Rashid alisema kumekuwa na mafanikio katika mkakati wa kupunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua ambapo takwimu za karibu zinaonesha vifo hivyo zimepungua kutoka vifo 840 kwa akina mama 100,000 na kufikia vifo 400 kwa wajawazito idadi hiyo.

TANZANIA na dunia nzima kwa sasa ...

foto
Mwandishi: Fadhili Abdallah

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi