loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kalala Junior ndani ya Bongo fleva

Ni bendi iliyovuta mashabiki wengi kwa wakati mmoja, kiasi cha kutishia kumbi za bendi zingine kuchukua nafasi zao. Yote hiyo ni kazi nzuri iliyokuwa ikitengenezwa na wanamuziki watatu waliounda kundi hilo akiwemo Kalala Junior, Khalid Chokoraa na Jose Mara (Mtoto wa Kimara Temboni).

Mpasuko mkubwa ukaja kutokea baada ya mmoja wao, Kalala Junior alipoamua kurudi katika bendi yake ya zamani, African Stars ‘Twanga Pepeta’ aliyotokea kabla ya kuanzisha Mapacha Watatu. Kurudi kwake Twanga Pepeta, Agosti mwaka jana, aliamua kutengeneza wimbo maalumu wa kuonesha kwa nini amerudi na nini anataka kufanya na kuamua wimbo huo kuupa jina la Nyumbani ni Nyumbani.

Wimbo ambao ulifanya vizuri kiasi cha uongozi wa bendi hiyo maarufu nchini, kuamua kuipa jina la albamu yake ya 10 kwa jina la Nyumbani ni Nyumbani. “Nilihama Mapacha Watatu na kurudi katika bendi yangu sababu ya mshahara kuwa mdogo, hivyo kwa sasa sioni sababu ya kuondoka tena na hata kama nikiondoka nitarudi hapa hapa,” anasema Kalala Junior.

Anasema kwa sasa ameandaa staili mpya ya uimbaji kwa Twanga Pepeta ambayo inaitwa Cheza Nalinga. Staili hiyo ambayo inapatikana mwisho wa wimbo au katikati maarufu kama kurapu, inakuwa kama kionjo cha wimbo. Hivyo anasema anatarajia kuiongezea ujuzi zaidi ili kuja kutumika katika albamu ijayo ya Twanga Pepeta, ambayo itakuwa ya 11.

“Kwa wale watu wanaokuja kuangalia matamasha yetu ya ‘live’, huwa wanaijua staili hiyo ya uimbaji kwa kuwa ni maarufu sana,” anabainisha mwimbaji huyo. Anasema tayari ameshaanza kuitambulisha staili hiyo katika majukwaa na watu wamekuwa wakiimba anapoanza kuimba, jambo ambalo linaonesha kwamba inakubalika kwa wapenzi wa muziki huo.

“Watu wameanza kuikubali staili hiyo mpya, hivyo nahitaji kuiboresha na kuiweka kwenye albamu ijayo ya bendi yake,” anasema Kalala Junior ambaye alifafanua kuwa kwa sasa amejifunza kupiga vifaa vyote vya muziki ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kimuziki. Anasema ni muhimu kwa mwanamuziki pia kuvijua vifaa vya muziki ili aimbe vizuri bila ya kumtegemea mtayarishaji ‘prodyuza’ ambao wamekuwa wakilalamika kila siku.

“Ujue kama utakuwa ukivijua vizuri vifaa vya muziki na upigaji wake, basi hata kuimba na kwenda na mdundo haitakusumbua sana,” anaeleza. Aidha, mwimbaji huyo ameamua kujiingiza rasmi katika muziki wa Bongo Fleva. Kalala Junior amesema kujiunga kwake katika muziki wa Bongo fleva, ni kutaka kuingiza staili mpya ya rhumba katika muziki huo. “Ingawa naimba muziki wa dansi, lakini nagundua kuna kitu kinakosekana kwenye muziki wa Bongo fleva,” anasema.

Anasema hivyo kuamua kujiingiza kwenye muziki huo ni kutaka kuonesha ladha tofauti yenye asili kama ya dansi katika muziki wa Bongo fleva. Kalala Junior anaendelea kusema kwamba tayari ameshaanza mikakati ya kuandaa albamu ya muziki wa Bongo fleva ambayo pia kutakuwa na mitindo tofauti kama Rhumba na Bolingo.

“Nimeona ni bora katika albamu hiyo niweze kutengeneza hivyo vitu vipya kisha niwaachie Watanzania wachague wenyewe,” anasema na kuongeza kuwa hiyo itakuwa albamu yake ya pili, baada ya ile ya kwanza ambayo aliamua kurudia nyimbo zote za baba yake mzazi, Komando Hamza Kalala.

Albamu hiyo aliamua kuifanya kama albamu yake ya kwanza, na hii ya pili ndiyo yupo kwenye maandalizi ya kuikamilisha ambayo ni nje ya bendi yake ya Twanga Pepeta.

“Hii itakuwa albamu yangu ambayo haitahusiana na bendi yangu ya Twanga,” anaendelea kusisitiza. Anasema wimbo wa kwanza katika albamu yake ya Bongo Fleva, tayari umeshakuwa tayari huku akihitaji kumshirikisha mmoja wapo katika ya Ommy Dimpoz na Ali Kiba. “Nahitaji kumshirikisha mmoja wa wasanii wa Bongo Fleva, kati ya Kiba au Dimpoz sababu ndiyo ninaowakubali sana,” anasisitiza.

Kuhusu mkataba wake na kazi zake za nje, anasema mkataba haumbani kutofanya kazi zake za nje isipokuwa ni kwa makubaliano maalumu. Hivyo anaweza kuimba muziki wa Bongo fleva na kupata umaarufu na kwenda kufanya matamasha nje, bila ya kizuizi chochote.

Kufanya hivyo anasema anaruhusiwa ilimradi atoe taarifa kwa uongozi ambao wenyewe ndiyo utatoa ridhaa ya yeye kwenda kufanya kazi hiyo. “Uongozi wanachohitaji ni taarifa ya kwamba nitafanya tamasha sehemu fulani na baada ya hapo nitaweza kufanya kazi yangu,” anafafanua na kubainisha kuwa kwa sasa ana mkataba ambao unaruhusu kama mtu akivunja makubaliano waliyoweka, basi humlipa mwenzake kwa kukiuka makubaliano hayo.

Anasema sasa hana mpango wa malumbano na mtu isipokuwa anaangalia maslahi zaidi kwenye muziki. Hata hivyo, nyota huyo anasema muziki alianza akiwa na bendi ya Bantu Group iliyokuwa ikimilikiwa na mpiga gitaa la solo mashuhuri nchini na mwimbaji Hamza Kalala ambaye pia ndiye baba yake mzazi.

Hiyo ilikuwa bendi yake ya kwanza kuimba na kuifanyia kazi katika miaka ya 2000. Aliamua kujiunga na bendi hiyo baada ya miaka michache kumaliza elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari ya Makongo, Dar es Salaam na baadaye kumsaidia baba yake kuandaa nyimbo kali kama Ngozi ya kitimoto na baadaye albamu ya Tutabanana hapa hapa.

Mwaka 2002, alihamia Bambino Sound ikiwa chini ya Banza Stone mkoani Arusha, wakati huo baba yake akiwa kama meneja na baada ya hapo akahamia bendi tofauti zikiwemo TOT Plus, Mchinga Sound, Mchinga Generation, Twanga Chipolopolo na zingine.

SEKTA ya ubunifu (sanaa) na uchumi ...

foto
Mwandishi: Mohamed Mussa

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi