loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kama Mzazi: Watoto si kuku wa kienyeji

Kwa sisi vijana wa zamani tulikuwa tunaufahamu msemo huo kwa kumaanisha kwamba iwapo mtoto hatapata malezi mazuri tangu akiwa utotoni, uwezekano wa kumbadilisha kuwa na tabia nzuri akiwa mkubwa ni mdogo.

Hapa nataka kuwakumbusha wazazi wenzangu hususan wazazi wapya kwamba wakati wa kuwapatia watoto wetu malezi bora katika maisha yao ni pale wanapokuwa wameshaanza kupata ufahamu wa kuweza kuongea na kutambua mambo mbalimbali.

Mtoto hujifunza kutokana na mazingira na maelekezo anayopewa na wazazi au walezi wake, wakiwemo walimu na jamii kwa ujumla wake.

Namna moja ya kujua kwamba mtoto yuko katika mtiririko mzuri wa malezi ni pale wanapofika wageni nyumbani au wakiwa kwenye matembezi na wazazi au walezi wao.

Katika mazingira haya, utagundua au kupata kionesha njia kwamba mtoto yuko katika mstari sahihi wa malezi. Kiashiria cha msingi ni pale mtoto anaposalimia yeye mwenyewe au anapokumbushwa na wazazi wake kusalimia wakubwa anaowaona katika mazingira hayo.

Mtoto aliyelelewa katika misingi na maadili mazuri, atasalimia au anapokumbushwa kufanya hivyo mara moja atasalimia. Lakini ni kweli pia kwamba kwa watoto ambao hawakuelekezwa au kufundishwa kufanya hivyo wanaweza kukataa katakata kusalimia wakubwa hata kama ni kwa kutishiwa fimbo au adhabu nyingine.

Huwa ni aibu kubwa kwa wazazi makini kupatwa na dhahama ya aina hii, kwamba mtoto wako hasalimii wakubwa anaowaona. Huwa siyo sifa kwa wazazi bali ni aibu na ni dalili ya kushindwa kumpatia malezi mtoto wao.

Lakini pia kutokana na mtindo wa maisha wa siku hizi hususani kwa wazazi wa mijini kuwa na mikikimikii ya kusaka maisha, wazazi au walezi hukosa muda wa kukaa na watoto wao, hivyo watoto wakiwa bado wadogo tu wa kwenda shule za chekechea huwa jeuri, hukataa kutimiza maelekezo sahihi au kuyakubali maonyo kutoka kwa wazazi au walezi wao.

Hali inakuwa mbaya zaidi wakati mzazi husika anapoelezwa na wenzake juu ya tabia ya mtoto wake na yeye kutochukua hatua za kurekebisha kwa kigezo chochote kile.

Kwa mfano mtoto anachezea maji ya bomba na kukatazwa akikataa na mzazi akamwacha basi atazoea. Siku nyingine anatukana wenzake au hata watu wanaomzidi umri ukamwacha.

Mtoto wa aina hii ndivyo anavyoanza kuota usugu wa tabia mbaya ambazo hatimaye ataishia kuwa hivyo katika jamii. Ndiyo maana wahenga wanasema ‘Samaki mkunje angali mbichi.’

Sote ni mashuhuda kwamba samaki akiwa mkavu huwezi kumkunja kwani lazima atavunjika. Hali ni kama hiyo kwa watoto wanaopewa malezi mabovu na wazazi au walezi wao.

Kukabiliana na hili wazazi hawana budi kuanza nao mapema watoto wao kwa kuwapatia maelekezo, maonyo, ushauri, mila na desturi nzuri katika jamii zetu mbalimbali ili nao waweze kuwa watu wenye mtazamo sahihi wa kitanzania na dunia katika maisha yao ya ukubwani. Tusiwaache watoto waishi kama kuku wa kienyeji. Ni wajibu wetu kuwaongoza.

NATAKA niwe mkweli kwa nafsi yangu kuwa, hata kama tungekuwa ...

foto
Mwandishi: Nicodemus Ikonko

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi