loader
Picha

Kampuni hizi mfano bora, heshima EAC

Wakurugenzi wa kampuni hizo, Hamis Mikate wa Ensol na Franz Kottulisnky wa RVE, waliwaambia wanahabari katika taarifa yao kuwa kampuni hizo, zilipata tuzo na kuiwakilisha Tanzania katika Jukwaa la Uwekezaji Umeme Vijijini, liitwalo ‘Alliance for Rural Electrification (ARE) Investment Forum’, lililofanyika nchini Italia Machi 13- 15, mwaka huu.

Ilibainishwa kuwa jukwaa hilo, liliwashirikisha wawakilishi wa kampuni na taasisi kutoka nchi mbalimbali za Afrika, Asia, Amerika na Ulaya na lilifanyika katika Kisiwa cha Sicily, ambako jukwaa lilizitambua na kuzipa tuzo kampuni zilizotoa mchango maalumu, kuendeleza sekta ya umeme vijijini katika nchi zao kwa ubunifu na mawazo endelevu ya biashara.

Katika jukwaa hilo, Mkurugenzi wa Miradi wa Ensol, Prosper Magali alichaguliwa kuwa miongoni mwa wajumbe tisa wa Bodi ya Jukwaa hilo la Kimataifa, wanaoiwakilisha ARE duniani kote, wakitoka katika nchi mbalimbali, akiwa Mtanzania na Mwafrika pekee.

Jukwaa lililenga kujadili mwenendo na sera za kimataifa, zinazohusu nishati safi ili kuangalia namna bora ya kuunganisha sera hizo na jamii vijijini katika nchi zinazoendelea na kuhakikisha jamii zinakua kiuchumi kupitia miradi ya umeme vijijni.

Katika makundi saba ya tuzo hizo za ARE Mwaka 2018, Rift Valley Energy (RVE) ilishinda na kupata tuzo katika Kundi la nne la ‘Sekta Binafsi Katika Nchi Zinazoendelea’ kupitia Mradi wa Mwenga Hydro, uliowezesha kuzalisha umeme wa maji wa megawati 4, kuunganisha katika gridi ya taifa na kuusambaza katika mtandao wa kilomita 300 maeneo ya Mufindi na Kihansi, unaowezesha nyumba 3,000 kupata nishati hiyo.

Ensol Tanzania Limited iliijengea heshima Tanzania na hata Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kuibuka kidedea katika Kundi la 6 la ‘Miradi Bora ya Umeme Vijijini’, kupitia mradi wake kijijini Mpale katika Milima ya Usambara wilayani Korogwe mkoani Tanga.

Huu unatoa na kusambaza umeme wa kilowati 48 kutokana na mionzi ya jua, ukihudumia nyumba 250 zenye wakazi wapatao 3,000, hali inayowanufaisha kibiashara na kwa uzalishaji mali.

Mikate wa Ensol anasema Ensol iliweza kushirikiana na wadau wa ndani na wa kimataifa kufikisha kwa mara ya kwanza umeme kwa zaidi ya wakazi 3,000 wa kijiji hicho na maeneo yanayokizunguka.

Majaji walifurahishwa na ubunifu na matumizi ya teknolojia, yanayowezesha malipo kupitia simu za mkononi, yanayowarahisishia wateja kupata huduma bora zaidi na kwa wakati.

Kimsingi, kufanikiwa kwa kampuni hizo za Kitanzania, kutekeleza miradi hiyo dhidi ya kampuni zilizoomba toka sehemu mbalimbali barani Afrika, Asia na Amerika na kwingineko, kunaonesha kuwa ushiriki wa sekta binafsi katika uendelezaji wa sekta ya umeme vijijini nchini Tanzania, unatambulika kimataifa, kama mfano bora wa kuigwa.

Hapana shaka kuwa ushiriki wa kampuni hizo katika miradi ya umeme vijijini, umewezesha kushirikisha maeneo ya vijijini nchini Tanzania, kupata umeme na kushiriki kikamilifu kulisaidia taifa kuelekea uchumi wa viwanda.

Ndiyo maana ninasema Ensol na Rift Valley Energy ni mfano bora kuisaidia Tanzania, kuingia uchumi wa viwanda kwa uhakika wa umeme.

MSIMU wa sikukuu za mwisho wa mwaka umewadia. Siku ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi