loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kanisa la Mkunazini urithi maridhawa Z’bar

Eneo lililopo kanisa hilo ndipo palikuwa kitovu cha biashara ya utumwa. Watumwa walinadiwa mahala hapo na kuuzwa kwa mawakala ambao walipelekwa nchi mbalimbali duniani. Inasadikiwa kuwa zaidi ya watumwa milioni 20 kutoka Afrika waliuzwa katika nchi mbali mbali za Ulaya pamoja na Marekani kati ya mwaka 1450 hadi 1880.

Kanisa la Anglikana lilijengwa na kupata baraka zote kutoka kwa Sultani Sayyid Barghash aliyetawala visiwa hivyo toka mwaka 1870- hadi 1888. Sultan Barghash alitoa kibali na sehemu ya kiwanja kama zawadi kwa ajili ya ujenzi wa kanisa hilo.

Zanzibar imeingizwa katika orodha ya nchi zenye urithi wa kimataifa kutokana na vigezo vya usanifu wa majengo ya kale likiwemo Kanisa la Anglikana lililojengwa mwaka 1873-1877 kwa ustadi na usanifu wa hali ya juu.

Akizungumza katika sherehe za utiaji saini wa ukarabati mkubwa wa jengo la Kanisa la Mkunazini ambazo zilihudhuriwa na Balozi wa Jumuiya ya Ulaya EU nchini, Waziri wa Habari Utangazaji Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk alisema historia ya Zanzibar imebebwa na Kanisa la Mkunazini ambalo linaonesha uvumilivu wa watu kuabudu na kuheshimu dini za watu tofauti tangu enzi hizo.

Alisema Zanzibar ni visiwa vyenye mchanganyiko wa watu mbalimbali wenye kuamini na kuabudu dini tofauti kwa muda mrefu ambapo historia inaonesha kwamba ujenzi wa kanisa ulipata baraka zote kutoka kwa kiongozi wa wakati huo ambaye ni Sultani kutoka Oman.

Mbarouk anasema Kanisa la Anglikana la Mkunazini limebeba historia ya Zanzibar na kuchangia kwa kiasi kikubwa kupigwa vita biashara ya utumwa. “Zanzibar inatajwa enzi na karne kuwa visiwa vyenye uvumilivu mkubwa wa dini na imani za watu katika misingi ya kuheshimiana... Utamaduni huo tunatakiwa kuudumisha,” anasema Waziri Mbarouk.

Jumuiya ya Ulaya imekubali kutoa fedha kulifanyia ukarabati mkubwa Kanisa la Mkunazini ambalo lipo katika hali ya uchakavu huku baadhi ya kuta zake zikiwa zimeanza kupasuka na kuweka nyufa. Balozi wa Jumuiya ya Ulaya nchini, Filibe Sebriga, anasema wameamua kulifanyia ukarabati Kanisa la Mkunazini kwa sababu limebeba historia kubwa inayotokana na mchango wa kanisa hilo kama chombo cha dini na biashara ya utumwa.

Anasema kanisa hilo linadhihirisha jinsi wananchi wa Zanzibar walivyokomaa na kuwa na uvumilivu wa imani tofauti za dini kwa miaka mingi. “Jumuiya ya Ulaya imeamua kulifanyia ukarabati mkubwa Kanisa la Mkunazini kutokana na mchango wake mkubwa kwa Zanzibar katika historia na usanifu wa majengo ya makumbusho,” anasema.

Balozi amewataka Wazanzibari kuiga mfano huo wa kuheshimu dini za watu mbalimbali ili kuepuka vitendo vya chuki na uhasama. Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Anglikana la Zanzibar, Askofu Michael Hafidh, anasema wamefurahishwa na taasisi za kimataifa ikiwemo Jumuiya ya Ulaya kukubali ombi la kulifanyia ukarabati jengo hilo la kale.

Anasema Kanisa la Anglikana Mkunazini linaonesha uvumilivu wa kidini uliopo nchini ambao ni wa kupigiwa mfano katika nchi nyingi duniani. “Kanisa hili ni alama ya Zanzibar kama nchi yenye uvumilivu wa kidini... Waislamu wapo kwa asilimia 90 lakini wafuasi wengine wa dini nao wapo na wanaheshimiwa muda wote,” anasema.

Anasema kukamilika kwa ukarabati wa kanisa hilo kwa kiasi kikubwa kutaimarisha mapato ya kanisa hilo yanayotokana na wageni wanaotembelea jengo hilo la kale kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Historia inaonesha kwamba kanisa hilo lilijengwa na askofu kutoka Uingereza aliyejulikana kwa jina la Edward Steere.

Kutokana na ukweli kwamba eneo na baraka za ujenzi wa kanisa hilo vilitolewa na Sultani Barghash, kunamfanya Askofu Michael Hafidh kusema: “Kumbe misingi ya kuongoza na kufuata utawala bora wa kuheshimu imani za watu ulianza tangu enzi za utawala wa kisultani katika miaka hiyo mingi iliyopita. Ni vyema Wazanzibari wakaendelea kuheshimu misingi hiyo.”

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe, Issa Makarani Sarboko, anasema Kanisa hilo ni kielelezo cha urithi wa majengo ya kale duniani kote. Anasema kanisa hilo ni sehemu muhimu ya historia ya Zanzibar inayotokana na urithi wa majengo ya kale duniani pamoja na historia ya utumwa ambapo Zanzibar ilikuwa kituo kikuu cha biashara hiyo iliyopigwa marufuku baadaye.

“Historia ya Zanzibar imetangazwa kwa kiasi kikubwa na Kanisa la Mkunazini ambalo ndiyo kitovu cha biashara ya utumwa,” anasema.

Kanisa linatajwa kuchangia kupigwa marufuku kwa biashara ya utumwa Zanzibar na baadaye duniani kote kwa juhudi binafsi zilizofanywa na mvumbuzi David Livingstone. Katika mwaka 1857 Dk Livingstone ambaye ni mmisionari kutoka Uingereza alifanya ushawishi katika Bunge la Uingereza kupiga marufuku biashara ya utumwa baada ya kuona madhara yake wakati alipokuwepo Zanzibar.

Muswada wa kupiga marufuku biashara ya utumwa uliwasilishwa bungeni mwaka 1833 na hatimaye mwaka 1834 Augosti 1 Bunge la Uingereza lilipiga marufuku rasmi biashara ya utumwa. Kanisa la Mkunazini linatembelewa na watalii wengi kutoka nchi mbalimbali ambao hujionea hali halisi ya historia iliopo hapo ikiwemo ya biashara ya utumwa.

Mmoja ya watembezaji watalii katika Kanisa hilo Michael John anasema katika msimu wa utalii hupokea zaidi ya watalii 50,000 kwa mwaka ambao hutaka kujua historia ya kanisa hilo na uhusiano wa biashara ya utumwa. ‘Watalii wengi wanavutiwa na kutembelea eneo la kanisa zaidi ili kujua historia ya Kanisa na uhusiano uliopo baina ya kanisa na biashara ya utumwa,” anasema.

Hilo ndiyo kanisa la Anglikana la Mkunazini ambalo ni kanisa la kwanza kujengwa Zanzibar likipata kibali kutoka kwa utawala wa kisultani wa Oman.

TANGU mwishoni mwaka jana 2020, ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi