loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Karibu tena Phiri, tuheshimu mikataba ya makocha

Logarusic alifutwa kazi Jumapili iliyopita, baada ya wakuu wa Simba kueleza kutoridhishwa na mwenendo wake katika kuinoa timu hiyo, ikiwamo pia suala la nidhamu kudaiwa kuchangia kufukuzwa huko.

Siku chache baada ya kumfukuza kocha huyo ambaye alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja uliosainiwa takriban mwezi sasa, Simba ilimtangaza Phiri kushika mikoba hiyo na akatua nchini Jumatano wiki hii.

Kutua kwake Simba kunamfanya arudi kwa vijana hao wa Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo, Dar es Salaam kwa mara ya tatu sasa. Awali, tungependa kumpongeza kwa kuteuliwa kwake kuinoa timu hiyo kwa mara nyingine, hilo likithibitisha imani waliyonayo viongozi wa Simba kwake.

Si hao tu, hata mashabiki wa Simba pia wameonesha imani kwake hasa ikikumbukwa kwamba katika msimu wa 2009-10 aliiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara bila kupoteza mechi yoyote.

Kwa hiyo, hakuna shaka kwamba huyu ni mtu anayeifahamu vizuri Simba, hivyo anao uwezo mkubwa wa kusimamia maendeleo yake ya kiufundi na kuwapa raha mashabiki wake ambao msimu uliopita, haukuwa mzuri kwao.

Lakini wakati Phiri akitua na kupewa mkataba wa mwaka mmoja, ni lazima tuweke rekodi sahihi kwamba klabu kongwe hasa za Simba na Yanga zinaanza kujenga mazoea ya tabia ya kufukuza kocha wakiwa wamedumu nao kwa muda mfupi.

Ukiondoa Logarusic aliyetimuliwa baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja ambao aliutumikia kwa takriban mwezi, Simba iliwahi kuwafukuza wazalendo Abdallah Kibadeni na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo.

Hao nao walipewa kazi baada ya kufukuzwa kwa makocha wengine wageni wakiwamo Patrick Liewig aliyefukuzwa kama ilivyokuwa kwa Milovan Cirkovic.

Kwa Yanga, wapenzi wa soka wameshuhudia kufukuzwa katika siku za karibuni kwa makocha kama Ernie Brandts, Tom Sentiefit, Dusan Kondic, Kostadin Papic na wengine, ambao mikataba yao haikufika mwisho.

Tabia hii kwa kweli haijengi mazingira mazuri ya kuwa na uendelevu wa timu katika masuala ya ufundi na inachangia timu kufanya vibaya.

Ni vizuri timu za Yanga na Simba zikajifunza kwa timu ya Azam FC na hata Mtibwa Sugar ya Morogoro, ambazo zimekuwa na utaratibu wa kuheshimu mikataba ya makocha wao na hata maendeleo yao yanavutia sababu ya kukaa muda mrefu na makocha.

Ni imani yetu kuwa Phiri na hata kwa upande wa Yanga, kocha mpya, Marcio Maximo, mikataba yao itaheshimiwa na kupewa fursa ya kuzinoa timu kwa uhuru ili kuleta maendeleo badala ya kuvuruga programu zao na hata kurudisha nyuma maendeleo.

Kwani ni ukweli uliojengeka, kuwa na kocha kwa muda mrefu, kusaidia kujenga timu imara na mifano inaonekana kwa wenzetu waliopiga hatua kubwa kisoka hasa England ambako mashabiki wengi wa soka wanafutilia soka yake.

Tujifunze huko kwa sababu wenzetu wanamudu kukaa na makocha kwa miaka mingi ikiwamo kuanzia 10 hadi 23, na mafanikio yanaonekana, badala ya kufukuza kocha kwa sababu tu ameshindwa katika mechi ya kirafiki ya bonanza.

RIPOTI ya 15 kuhusu uchumi wa Tanzania ya ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi