loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kasoro kila kona Uchaguzi Mkuu BFT

Kasoro kila kona Uchaguzi Mkuu BFT

Kufanyika kwa uchaguzi kunaiwezesha BFT kuwa na baadhi ya sura mpya, huku nafasi ya ukatibu mkuu ikiendelea kushikiliwa na Makore Mashaga ambaye katika uongozi uliopita ni kama alikuwa akiliongoza shirikisho hilo peke yake. Baadhi ya viongozi walijiuzulu hata kabla ya kumalizika kwa kipindi chao cha uongozi na hivyo kumfanya Mashaga kuhangaika na BFT yeye mwenyewe.

Waliochaguliwa:

Katika uchaguzi huo uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Wakala wa Uongozi na Maendeleo ya Elimu (ADEM), na kusimamiwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), BFT ilishindwa kumpata rais wake. Nafasi ya Rais ambayo katika uongozi uliopita ilikuwa ikishikiliwa na mwanadada Joan Minja, ilishindwa kumpata mrithi baada ya mgombea pekee, Andrew Kuyeyana kushindwa kupata kura nyingi za Ndiyo.

Mpinzani wa Kuyeyana, Mutta Rwakatale alienguliwa katika mchujo wa BMT uliofanyika muda mfupi kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo, ambao ulijaa dosari kibao za kiutawala na kiutendaji. Kuyeyana licha ya kutokuwa na mpinzani katika kinyang’anyiro hicho cha urais, alijikuta akiambulia kura 11 za Ndiyo huku 14 zikimkataa na kufanya kuikosa nafasi hiyo muhimu.

Hata hivyo, kitendo cha kumuengua Rwakatale kuwania nafasi hiyo nusura kisababishe vurugu baada ya baadhi ya wajumbe kutokubaliana nacho wakidai kuwa BMT walifanya hivyo ili kuhakikisha Rwakatale hagombei na wao kumuweka mgombea wao.

BFT sasa itakuwa chini ya Makamu wa Rais, Lukelo Wililo aliyepata kura za Ndiyo 19 wakati Katibu Mkuu ataendelea kuwa Makore Mashaga aliyeshinda kiti hicho kwa kura 17 za Ndiyo na tano za Hapana licha ya kutokuwepo katika uchaguzi huo.

Mhazini sasa ni Chad Jonathan Kapandantava aliyeondoka na kura 21 huku tatu tu zikisema Hapana katika uchaguzi huo uliohudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa BMT, Henry Lihaya, Richard Mganga na Nelson Chacha.

Wajumbe wa Kamati ya Utendaji waliochaguliwa na kura zao katika mabano ni Said Omary Gogopoa na Restuta Bula (18), Asha Vonatis (15), Zuwena Kipingu na Leopord Kayunga (14), Salehe Mwinyiheri (13), Juma Bugingo (11), Anthony Mwang’onda (10) na Salum Viduka (9).

Uchaguzi wenyewe:

Uchaguzi huo ulioahirishwa kwa karibu mara mbili, ulionekana tangu mwanzo kuwa ungejaa ubabaishaji baada ya BFT wenyewe kutokuwa na mpangilio mzuri kuanzia mahali ambako wangefikia wajumbe wao, ukumbi, makabrasha na mambo mengine kibao.

BFT haikuwa na fedha ya kuwaandalia malazi wajumbe wake kiasi cha kufanya mgombea mmoja kuamua kuwafadhili wajumbe hao katika hoteli yake kitu ambacho sio kizuri katika uchaguzi kwani nafasi hiyo inaweza kutumika vibaya. Haina tofauti na takrima. Mbali na kasoro hizo hata taarifa za fedha, Rasimu ya Katiba na taarifa zingine zilipatikana pale pale ukumbini badala ya wajumbe kupewa siku kadhaa kabla ili kuzipitia mapema.

Kupatiwa taarifa mapema kungewawezesha wajumbe kutoa michango yao ya mawazo au kufanya marekebisho muhimu katika rasimu yao ya Katiba ya BFT, ambayo hata hivyo haikujadiliwa baada ya wajumbe kuipinga hadi pale itakapotafsiriwa.

Uongozi uliomaliza muda wake BFT haukuwahi kuitisha Mkutano Mkuu kwa kipindi chote cha miaka minne walichokuwa madarakani, kitu ambacho ni kinyume cha Katiba yao ambayo inawataka kufanya mkutano huo mara moja kwa mwaka.

Mbali na kufanya marekebisho ya Katiba yao, lakini bado ilikuwa na upungufu mwingi, kitu ambacho kinaacha maswali mengi kuliko majibu ya mahali ambako BFT walifanya marekebisho hayo. Taarifa ya fedha nayo ilijaa ubabaishaji mkubwa kiasi cha kufanya Rais aliyekuwa anamaliza muda wake, Minja kuipinga ambayo iliyoandaliwa na katibu wake, Mashaga, lakini haikupitishwa na Kamati ya Utendaji.

Kingine BFT walitakiwa kujipanga ili kuhakikisha wajumbe wa Mkutano Mkuu wanaandaliwa chakula badala ya kuwaacha wagombea ndio kuandaa msosi kwa wapiga kura, kitu ambacho kinaweza kuchukuliwa kama `rushwa’ kwa wapiga kura.

Kwa upande wa BMT:

Baraza la Michezo la Taifa (BMT), liliusimamia uchaguzi huu kwa mujibu wa Katiba ya BFT, lakini nao hawakujipanga vizuri kwani kulikuwa na kasoro nyingi katika usimamizi wao huo.Pamoja na kufanya jambo zuri la kuzuia uchaguzi huo kufanyikia katika hoteli ya mmoja wa wagombea, lakini bado walichemka kwa kufanya usaili muda mfupi kabla ya uchaguzi wenyewe kitu ambacho kiliwafanya kutokuwa makini sana au kutowapa wahojiwa muda wa kutosha wa kujieleza.

Ilitakiwa BMT lazima itoe muda wa wagombea waliochujwa katika usaili kukata rufaa na kutoa nafasi kwa wengine kuwapinga wale waliopitishwa kugombea kama wana vizuizi, lakini hilo lilishindikana sababu ya kufanya usaili siku hiyo hiyo ya uchaguzi. Kuendesha usaili siku hiyo hiyo ya uchaguzi ilisababisha kuleta malumbano makali na baadhi ya wajumbe ambao walipinga kitendo cha BMT kumuengua Rwakatale kuwania kiti hicho cha urais.

Pia BMT walionekana kutojipanga vizuri kwani awali walitaka wapiga kura kutumia kalamu za risasi katika kuchagua jina la mgombea, kitu ambacho kilipingwa na wajumbe na kufanya BMT kubadili utaratibu na wajumbe kutumia kalamu za wino. Hata hakukuwa na maboksi ya kupigia kura na badala yake kura zilikuwa zikiwekwa katika bahasha wakati wangeweza kuweka utaratibu mzuri wa kutumia vifaa vya plastiki ambavyo huonesha ndani.

Pamoja na kasoro zote, uchaguzi umemalizika na kinachotakiwa sasa ni kwa viongozi wapya kukaa chini na kuhakikisha wanauendeleza mchezo huo wa ndondi na kuacha kabisa ubabaishaji uliofanywa na waliopita.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Cosmas Mlekani

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi