loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Katavi wanavyochangamkia ufugaji wa nyuki kisasa

Mkoa wa Katavi, licha kujaaliwa utajiri mwingi wa maliasili ikiwemo wanyama pori, madini ya aina mbalimbali na ardhi yenye rutuba ifaayo kwa kilimo, pia una hekta nyingi za misitu ya aina mbalimbali ikiwemo miombo.

Misitu hii inafaa sana kwa shughuli za ufugaji wa nyuki. Umuhimu wa ufugaji nyuki haupo katika kupata masega na asali pekee, lakini wadudu hawa wanasaidia sana kuboresha chamvua ambayo ni muhimu katika kuboresha mbegu.

Ndio kusema uchavushaji unasaidia kuweka sawa mbegu ziwe za kwenye mapori au katika mashamba ya binadamu kama alizeti ambayo yanashauriwa kuwa karibu kutokana na mahitaji ya nyuki.

Kwa takwimu za hivi karibuni, Tanzania ina makundi makubwa ya nyuki, ambayo kwa pamoja yana uwezo wa kuzalisha tani 138,000 za asali na tani 10,000 za nta kwa mwaka.

Lakini hii ni endapo nyuki hawa watafugwa kisasa. Hata hivyo, licha ya kujaaliwa utajiri huo wa kuwa na nyuki na misitu mingi, bado Tanzania inazalisha tani 9,000 tu za asali zenye thamani ya Sh bilioni 27 na tani 600 za nta zinazokadiriwa kuingiza Sh bilioni tatu tu.

Hebu piga mahesabu namna tulivyo nyuma kwa kuzalisha 'vijitani' 9,000 wakati tungeweza kuzalisha tani zaidi laki moja kwa mwaka!

Kwa takwimu hizo, hakuna ubishi kwamba hamasa inahitajika kutolewa pmoja na mitaji kwa wakulima kupitia mkakati maalum utakaowekwa ili kuhakikisha wananchi wengi wanachangamkia fursa hii adhimu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, mbali na kuwaongezea wakulima na wafugaji kipato, ufugaji wa nyuki ni ajira kwa vijana pia.

Takwimu zinaonesha kwamba nchi ya Ethiopia inayoongoza katika Bara la Afrika kwa kuzalisha asali kwa wingi huku ikishika nafasi ya nane katika dunia, inazalisha tani 39,000 tu za asali kwa mwaka na kwa mahesabu ya hapo juu Tanzania tukidhamiria tuna uwezo wa kuipita maradufu.

Mtoto wa Mkulima, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amenukuliwa mara kadhaa akihimiza wananchi wakiwemo vijana kuchangamkia ufugaji wa nyuki kwa kujiunga katika vikundi vya uzalishaji ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Pia amekuwa akirudia kauli yake mara kadhaa akiwahimiza wakulima mmoja mmoja au waliojiunga katika vikundi vya uzalishaji, hususani vijana kufuga nyuki kwa njia ya kisasa kwa kuwa na mizinga ya kisasa ya nyuki ambayo mfugaji hahitaji mtaji mkubwa na kwamba mfugaji anaweza kuanza na mizinga mitatu ya kisasa na ikampa mafanikio.

Pinda amekuwa pia akiwahakikishia wafugaji wa nyuki kuwa masoko ya uhakika yapo katika nchi za Ulaya, Marekani na Mashariki ya mbali. Waziri Mkuu kila anapopata fursa ya kuwepo kijijini kwake alikozaliwa, pale Kibaoni wilayani Mlele katika Mkoa wa Katavi hachoki kuwahimiza wakulima kuchangamkia fursa hii ya ufugaji nyuki.

Mwaka jana nilibahatika kufika kijijini Kibaoni na kushuhudia baadhi ya mashamba yake anayofuga nyuki kwa njia ya kisasa ambapo kijijini hapo na kwingine yamegeuka kuwa mashamba darasa. Wakazi wa kijiji cha Kibaoni walinidokeza kwamba Waziri Mkuu amekuwa chachu ya kubadili maisha yao kupitia ufugaji nyuki, si katika kijijini Kibaoni pekee bali hadi Inyonga ambayo sasa ni makao makuu ya Wilaya ya Mlele.

“Kwa sasa vijana wengi hapa wilayani Mlele wameanza kuchangamkia ufugaji wa kisasa wa nyuki baada ya Waziri Mkuu kutuonesha njia. Wengi wetu tumeachana na ule ufugaji wa kizamani tulipokuwa tukitumia mizinga iliyotengenezwa kwa magome ya miti," anasema Moshi Mwigulu, mkazi wa kijiji cha Usevya kilicho kilomita chache kutoka kijijini Kibaoni.

"Miaka ya nyuma haikuwa rahisi kuona mtu akiwa na mizinga mingi na ilikuwa ni nadra kuona mtu anamiliki mizinga ya kizamani zaidi ya 100 lakini kwa sasa kuna vijana, tena wa umri mdogo wanamiliki mamia ya mizinga ya nyuki," anathibitisha Damian Chapewa kutoka wilayani Mlele.

Kwa mujibu wa Chapewa, kwa sasa yeye binafsi ana mizinga ya kisasa 50 inayompa zaidi ya lita 200 kwa mwaka na anauza asali yeye mwenyewe. Ndoto yake ni kufikisha mizinga ya kisasa zaidi ya 100 ili aweze kupata lita zaidi ya 400 kwa mwaka.

“Ujue ufugaji huu wa kisasa ni mzuri kwa kuwa pamoja na kuondoa hatari ambayo watu walikuwa wakiizungumza katika ufugaji na urinaji asali kwa kutumia njia zile za kizamani, ufugaji huu pia unasaidia sana kukabiliana na maadui wa nyuki ambao awali walikuwa wanasumbua katika ufugaji wa kienyeji.

"Nyuki nao wana maadui wao kama vile mvua, mchwa, upepo mkali, moto, jua la moja kwa moja na kelele za mara kwa mara,” anasema Chapewa.

Kwa kuunga mkono jitihada hizo za Waziri Mkuu, hivi karibuni, Shirika lisilo la Kiserikali la Usevya Development Society (Udeso), lilitengeza mizinga ya kisasa ya nyuki ipatayo 270 yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 17.

Mkurugenzi wa Udeso, Eden Wanyimba shirika lake litasambaza mizinga hiyo kwa vikundi saba vya uzalishaji vilivyopo wilayani Mlele ili kuviwezesha kuongeza uzalishaji wa asali iliyo bora katika harakati za kuwaongezea kipato wananchi.

Wanyimba anasema licha ya kuboresha elimu, kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, na kudhibiti maambukizi ya Ukimwi, Udeseo pia inajihusisha kikamilifu na uhifadhi wa mazingira.

“Hakika Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameonesha njia ya ufugaji nyuki, mie nikiri kuwa iwapo ufugaji huu utapata hamasa ya kutosha sina shaka wakazi wengi mkoani hapa watajihusisha nao na hakika maisha yao yatabadilika na kuwa bora zaidi kwani ufugaji huu wa nyuki hauhitaji mtaji mkubwa wa kutisha wala kutumia muda mwingi katika kuwashughulikia. Ni ufugaji ambao hauna palizi wala kutumia mbolea," anasema Wanyimba.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Kanali Ngemela Lubinga, anasema Serikali wilaya humo imejizatiti katika kuwaelimisha wakulima kuhusu ufugaji wa kisasa wa nyuki ikiwemo utumiaji wa mizinga ya kisasa ya nyuki na njia bora ya kuongeza ubora wa asali.

Kwa sasa Wilaya ya Mlele yenye ukubwa wa kilomita za mraba 28,000 ndio maarufu kwa ufugaji wa nyuki katika Mkoa wa Katavi.

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya ...

foto
Mwandishi: Peti Siyame

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi