loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Katiba mpya inahitaji mchango chanya wa waandishi wa habari

Lakini, kutokana na mawazo mchanganyiko ya wanajamii, wakati mwingine kupatikana kwa katiba si jambo jepesi kutokana na mitazamo tofauti ya wanajamii na hasa kunapojitokeza baadhi ya watu kutanguliza maslahi ya makundi yao mbele. Kwa mujibu wa Montesquieu Cohler (1989) na wengineo, vyombo vya habari huchukuliwa pia kama mhimili wa nne wa dola usioonekana baada ya serikali, bunge na mahakama.

Vyombo vya habari vimekuwa pia vikichukuliwa kama asasi za kiraia katika kukuza demokrasia na kuwakilisha matarajio na maslahi ya haki za kiraia.

Kwa mujibu wa mwanazuoni McQuail (2005) katika nadharia yake ya utengenezaji wa uhalisia, vyombo vya habari huchagua, hutathmini na kutoa vipaumbele kwa matukio ya aina fulani, watu fulani, vionjo fulani na fikra za aina fulani na kuvishadadia sana hadi vikageuka kuwa uhalisia wa maisha ya kila siku.

Huu uchaguaji, utathmini na ushadidiaji wa nini kiandikwe au kijadiliwe huitwa upangaji wa ajenda (agenda setting). Kama ajenda ni nzuri inakuwa na faida kwa jamii na kama ni mbaya basi jamii inateketea. Naye Fourie (2001) anabainisha kuwa hata upande ambao wanahabari huchagua kuuangazia zaidi katika matukio, ni kielelezo cha mbeleko ya uchambuzi na itikadi vinavyotumika kutengeneza uhalisia.

Fourie anadai kuwa vyombo vya habari vinaweza kutengeneza aina fulani ya mtazamo wa jamii na baadaye wasomaji, wasikilizaji na watazamaji wakaamini kwamba huo ukweli na ndio mtazamo wa jamii kwa ujumla hata kama wakati mwingine si kweli.

Wanahabari ni sehemu muhimu sana ya jamii yetu, ambao wana jukumu la kuelimisha na kutoa habari kwa umma kuhusiana na masuala mbalimbali yanayoendelea ndani na nje ya nchi, ambayo yanagusa maslahi ya wananchi yakiwemo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Hivi sasa nchi yetu ipo katika mchakato muhimu sana wa kuandaa katiba ya nchi itakayoamua mustakabali wa taifa letu na maendeleo ya wananchi kwa ujumla kwa miaka mingine mingi. Katiba inayotafutwa ni ambayo itasigana kiasi na ya sasa kwa maana ya kutilia maanani mabadiliko yanayotokea nchini mwetu na duniani kote, kujibu kero za sasa na pengine za baadaye kwani inatazamiwa itumike miaka 100 ama zaidi ijayo.

Kinachofahamika ni kwamba suala la kutengeneza katiba mpya si jambo rahisi rahisi kama ilivyodokezwa hapo juu. Ni jambo linalozungukwa na mitazamo tofauti ikiwemo ya wenye nia njema, wenye nia mbaya, wachoyo, waadilifu na kadhalika na hivyo wanahabari wanatakiwa kuwa watulivu, kuacha ushabiki na uwezekano wa kuwa mawakala wa mtu au kikundi fulani cha watu wenye uchu wa madaraka ama maslahi binafsi.

Hatua hii ni nyeti na muhimu sana kwa sababu maamuzi yake yakiwa mabaya yanaweza kuusambaratisha mchakato mzima wa kutunga Katiba. Kusambaratika kwa mchakato wa katiba kutokana na misuguano mikali ya kiimani, kiitikadi na kimsimamo baina ya wajumbe wa Bunge Maalumu ambako kunaweza kulitumbukiza taifa katika mgogoro hatarishi wa kisiasa na ni jambo ambalo halipaswi kushaabikiwa na waandishi wa habari.

Kitendo cha mwananchi au kundi la watu fulani kutamani au kupanga kuusambaratisha mchakato mzima wa kutunga katiba mpya ambayo imeshaligharimu taifa muda na raslimali nyingi katika hatua ya Bunge Maalumu ni sawa na uchuro kwa taifa. Aidha wanahabari wanatakiwa kutanguliza uzalendo, maadili, weledi na uwajibikaji katika nafasi yetu ya kuwafikia wananchi ili kuhakikisha masuala yenye maana kwa maendeleo yanawafikia walengwa na pia kukubaliana na nguvu ya wengi linapokuja suala la maamuzi.

Kimsingi mijadala yenye weledi katika ngazi zote za jamii itategemea sana uwepo wa wanahabari wenye ujuzi katika ngazi mbalimbali na sehemu sahihi katika jamii zetu.

Hivyo basi tujikite sote kwa pamoja katika kujenga uelewa sahihi juu ya huu mchakato katika kuwapatia wananchi maendeleo yao na kudumisha umoja na amani iliyopo ikiwa ni pamoja na kuwa na uelewa sahihi wa Katiba ya nchi. Kwamba katiba inatakiwa kubeba nini hasa na pia kuangalia nguvu ya hoja ya walio wengi.

Aidha wanahabari nikiwemo mimi, tuna jukumu kubwa la kutoa taarifa sahihi kwa maslahi ya taifa letu kuhusiana na yote yanayoendelea katika mchakato unaoendelea hivi sasa bungeni wa kupata Katiba Mpya Sambamba na hilo tunatakiwa tutumie taaluma na weledi wetu kwa kufanya kazi itakayoimarisha nchi yetu, mshikamano wetu, umoja wetu, upendo miongoni mwetu na amani iliyojengwa kwa zaidi ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Uhuru wa Tanzania Bara na Mapinduzi Matukufu ya Zanzaibar.

Kamwe tusikubali kutumika kwa ajili ya kuisambaratisha nchi, jambo ambalo halitakuwa na maslahi yoyote kwa taifa kwani bado Tanzania ni nchi moja yenye serikali mbili yaani ya Muungano na ile ya Zanzibar. Tuongozwe na dira inayosema kwamba neema ya amani tulio nayo sasa tutagundua utamu na umuhimu wake endapo siku moja tutakuwa sababu ya kuchangia kusambaratika kwake na Mungu apishilie mbali.

Tukumbuke kuwa Taifa la Tanzania limezaliwa kutoka kwenye tumbo la mapambano ya Ukombozi. Dira ya ukombozi ndiyo iliyowaongoza wapigania uhuru barani Afrika kudai haki ya kujitawala, haki ambayo ilipatikana lakini baadaye mataifa haya yakajikuta katika mbinyo wa kujitanua kiuchumi kutoka kwa waliokuwa wakoloni.

Dira ya ukombozi ndiyo iliyoongoza Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 na ndiyo iliyozaa itikadi ya Umoja Afrika na dira hiyo hiyo ndiyo iliyozaa wazo la kuunda Muungano wa Tanzania na pia ikazaa Azimio la Arusha na vingine vingi. Hivyo mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita ni matunda ya utekelezaji wa dira hiyo ya ukombozi.

Hivyo wanahabari, wajumbe wa Bunge Maalum, na wananchi kwa ujumla tunatakiwa kutambua kwamba misuguano mikali iliyopo sasa ni hatarishi kisiasa na kiusalama kama kila upaande utaendelea kung’ang’ana kivyake. Lakini tutambue kuwa katiba inayopiganiwa siyo mwarobaini au kikombe cha babu kinachotibu kila ugonjwa bali ni moja ya nyenzo za mapambano ya ukombozi ambayo utunzi wake unatakiwa kuzingatia historia ya nchi yetu na hali halisi ya sasa.

Lengo la mchakato wa Katiba ni kuhakikisha kwamba Tanzania inapata katiba ambayo ni bora itakayoshughulikia changamoto na kuweka mazingira ambayo yatamrahisishia maendeleo mwananchi kwa haraka. Na kimsingi, Bunge la Katiba halijadili kuhusu muundo wa serikali mbili au tatu pekee kwa sababu kuna mambo mengi kwenye rasimu ya katiba yanatakiwa kujadiliwa.

Isitoshe, kwa mtazamo wangu, muundo wowote utakaoukabalika si hoja kubwa isipokuwa unabeba nini na kukabiliana na mapungufu gani yaliyopo sasa. Kwa mtazamo wangu, hata muundo wa sasa wa serikali mbili ulioboreshwa ungeweza kutupeleka tunakotaka kama ndio hoja ya wengi walioko bungeni.

Kuzifanya tofauti za kiimani, itikadi na kimsimamo zilizopo kuwa mtaji wa kisiasa au mradi wa kuiyumbisha nchi kisiasa ni kujihujumu sisi wenyewe. Tunaporudi katika Bunge la Katiba kwa mara nyingine ni vyema habari zinazoandikwa katika vyombo vya habari mbalimbali hapa nchini zikasaidia kuimarisha na kujenga misingi ya umoja, mshikamano, upendo, amani, uwajibikaji na kulinda Muungano wa Tanzania na si vinginevyo.

Hiyo ndiyo inayopaswa kuwa ajenda ya waandishi wa habari kwa sasa wakati nchi ikielekea katika kurejea kwenye mchakato wa kukamilisha rasimu ya pili ya Katiba ili tupate katiba mpya.

KATIKA makala mbili zilizopita tumeangalia manufaa ambayo wanavijiji wamepata kutokana ...

foto
Mwandishi: Benjamin Sawe

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi