loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Katika hili la bei za umeme heko Tanesco

Msimamo wa Tanesco ambao unahimiza wazalishaji kupunguza bei ya kuuza umeme wao, ni msimamo unaoonesha kukomaa kwa uwajibikaji wa shirika hilo kwa umma.

Tunasema hivyo kwa kuwa tayari bei ya umeme ni kubwa na juhudi za serikali zimehamishiwa kupunguza makali hayo kwa kutumia rasilimali zetu zilizopo.

Ni tegemeo la serikali kwamba baada ya kupata gesi na makaa ya mawe kuchimbwa bei ya umeme nchini itapungua, lakini wafuaji hawa wa umeme kupitia makaa ya mawe wao wanaonesha kitu kingine kabisa, kwamba umeme huo ni ghali.

Wakati inajulikana wazi kwamba umeme wa makaa ni rahisi kutokana na ukweli wa namna rasilimali hizo zinavyokuwa karibu na maeneo ya kufua umeme, kitendo cha mawakala wa NDC kutaka bei kubwa haiwezi kuvumilika na wala Wachina kutaka senti 12 si sawasawa!

Na ndio maana sisi tunaungana na Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuwataka wahusika kukaa chini na kukokotoa upya kwani sisi si wapya wa kutumia nishati hii ambako duniani kote ina bei rahisi.

Ukiangalia maelezo ya katibu mkuu kwa kadhia zote mbili, umeme wa NDC na ule wa Wachina wa Ludewa unachoweza kukisoma kwa haraka ni juhudi za wafanyabiashara na wawekezaji kutunyonya na kujipatia faida kubwa huku sisi tukiumia.

Hivi inaingiaje akilini watu kutaka kuiuzia umeme Tanesco uniti moja kwa senti 12 za Marekani wakati wao wenyewe kwao wanaouziana umeme wa mkaa dola za Marekani senti 5?

Hatuwezi kwa namna yoyote ile kukubaliana na watu wanaotaka umeme uwe ghali hapa nchini kwani utakuwa mwanzo wa kuleta mfumuko wa bei kwa bidhaa mbalimbali.

Tunasifu ushujaa wa Shirika la Umeme (Tanesco), wa kukataa mkataba wa kununua umeme wa makaa ya mawe kwa gharama kubwa kutoka Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC), kwani tunaamini wangelikubali wangevuruga mpango wa kupunguza gharama ya umeme kwa wananchi.

Aidha tunampongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi ambaye amesisitiza mazungumzo na haja ya kupunguza zaidi bei ya umeme ili wananchi wote wafaidike na raslimali zilizopo.

Kwetu sisi msimamo huu wa Tanesco, tunaona kwamba ni salamu tosha ya watanzania kuwezeshwa kutumia utajiri wao kupunguza ukali wa maisha na si kuwafaidisha wachache na wao kuumia.

Tunapenda kuamini maneno ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kuwa bei ya umeme iliyopo kwa sasa ni kwa muda tu na itashuka baada ya ujenzi wa bomba la gesi kukamilika, hivyo kitendo chochote kitakachofanywa na wenye dhamana zao kuzuia kuendelea kunyonywa kwa Watanzania katika sekta ya nishati tutakiunga mkono.

Maonesho ya 44 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba, ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi