loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kauli ya Askofu itufumbue macho

Kauli hiyo aliyoitoa juzi wakati wa kuchangia fedha za kukamilisha ujenzi wa Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Kondoa, ililenga kuwakumbusha Watanzania, wajibu walionao kwa Rais, ambaye ndiye kiongozi mkuu wa nchi na huo, ndio ukweli.

Kwa mujibu wa Askofu Isuja, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, akitoa mwongozo na ushauri katika mada mbalimbali kwa wananchi wake, ni hekima na busara zinazomwongoza kwa kuwa ushauri huo unatoka kwa Mungu.

Askofu akasema Rais kwa wadhifa wake, mara zote anatumia hekima katika kutenda na kuamua mambo mbalimbali yahusuyo nchi ikiwemo suala la malumbano yanayoendelea sasa kote nchini kuhusu mchakato wa kupata Katiba mpya.

Kwake yeye kama Askofu mstaafu, tena kiongozi wa kiroho, anasema hafurahishwi na jinsi makundi mbalimbali ya Watanzania wanavyolumbana na kubeza hata miongozo inayotolewa na Rais Kikwete.

Tunanukuu alichosisitiza Askofu: “Imekuwa ni tabia kwa Watanzania kubeza na kudharau mashauri yake pasipokujua kuwa yeye ameteuliwa na Mungu kuwaongoza Watanzania”.

Akasisitiza kwamba ili nchi iwe na amani na upendo bila kugombana, Watanzania hawanabudi kuitegemea sana busara na hekima ya Mungu ili kusiwe na kutumbukia katika mizozo itakayohatarisha amani.

Ni katika hilo akaliasa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kujipima kama wanatumia hekima katika kujadili na kuwapatia Watanzania Katiba mpya.

Alisema kutofautiana kifikra si kosa, ila pawepo na busara katika kuridhiana na kufikia hitimisho ambalo matokeo yake ni kuleta amani, umoja na ustahimilivu kwa Watanzania wote na si kama inavyoonekana hivi sasa.

Tunaamini, kauli ya Askofu hainabudi kuchukuliwa kwa uzito mkubwa kwa kuwa, kabla ya rasimu hii kupelekwa bungeni, kulikuwepo na maneno ya hapa na pale kutoka kwa viongozi wa siasa, hasa vyama vya upinzani kudai kwamba hawatendewi haki katika chaguzi mbalimbali kwa vile Katiba iliyopo imepitwa na wakati.

Wakawa wanadai kwamba haiendani na mfumo wa vyama vingi vya siasa kwa vile, ina mtazamo wa chama kimoja cha siasa, hivyo ingekuwa vyema ibadilishwe na kukidhi haja ya mfumo uliopo sasa wa vyama vingi.

Lakini la kushangaza, hao hao viongozi waliokuwa wakihitaji Katiba tena kwa udi na uvumba, wamekuwa vinara wa kuhakikisha katiba hiyo ama inacheleweshwa pasipokuwa na hoja za msingi tena kwa kususa vikao halali au isipatikane kabisa.

Katika misingi ya demokrasia ambapo kila mtu anawajibika kuhakikisha analinda maslahi ya walio wengi, hatukutarajia viongozi wa siasa ambao ndio hao hao waliotaka Katiba, leo hii wanakuwa vikwazo kwa jambo dogo ambalo kimsingi linaweza kupatiwa ufumbuzi kwa maridhiano baada ya kujadiliana kwa pamoja na kupata muafaka.

Tunahitaji viongozi wanaowajali wananchi, wanaoheshimu mamlaka zilizopo madarakani na hasa kwa ngazi ya juu kabisa ya Rais wa nchi ambaye mbali na kuwa mtawala, lakini ushauri wake ni wa busara na hekima kwa ajili ya watu wake, ambao haunabudi kuheshimiwa badala ya kukaa vijiweni na kubeza.

RIPOTI ya 15 kuhusu uchumi wa Tanzania ya ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi