loader
Picha

KAULI YA MDADISI: UCSAF ilivyofanikiwa kuua benki za ardhini vijijini

Hii ni baada ya Serikali kubaini kuwa, teknolojia ya mawasiliano ya simu za mkononi, imejikita zaidi mijini na kuyaacha maeneo yaliyo pembezoni na yasiyo na mvuto wa kibiashara hasahasa, vijijini na kuwafanya watu wa huko, wazidi kuachwa nyuma kimaendeleo.

Kauli ya Mdadisi ilizuru maeneo mbalimbali kuona minara ya UCSAF ilivyobadili maisha wa watu hususani suala la benki yaani utumaji, upokeaji, utunzaji na ukopaji wa fedha kupitia simu za mkononi huko vijijini.

Katika Kijiji cha Singita, Jimbo la Solwa mkoani Shinyanga, Margaret Mwenda, anasema yeye ni mmoja wa wanakijiji waliopata ukombozi wa usalama wa pesa zao, baada ya UCSAF kusambaza minara ya simu katika vijiji vilivyoachwa na kampuni za simu kwa kukosa mvuto kibiashara.

Hata taasisi za kifedha zikiwamo benki, nazo zimeyakwepa maeneo hayo. Matokeo yake, huduma za kuhifadhi pesa mahali na njia salama zilikuwa kitendawili na kuwalazimisha wengi kuchimbia pesa ardhini, au kuziweka chini ya godoro ili kuzihifadhi, au kutembea nazo mfukoni.

Anapozungumza na makala haya kijijini kwake, Magreth anasema yeye ni miongoni mwa wanaonufaika na kushangilia mpango wa serikali kupitia UCSAF kufadhili uwekaji wa minara ya simu vijijini na hivyo, kuepukana na benki za ardhini anazosema ni hatari.

“Wakati kijiji chetu hakijawa na simu, nilikuwa nikifanya biashara zangu, faida ninayopata ninaitunza kuchimbia na kuficha chini au kwenye godoro au sehemu nyingine nje ya nyumba ili siku nikipata nafasi, nimpelekee mama anitunzie,” anasema Margaret, mfanyabiashara ya mgahawa (mamantilie) kijijini kwake.

Anasema tofauti na utunzaji wake wa pesa siku za nyuma kwa kuficha kwenye kishimo nyumbani hadi anapozileka kwa wazazi wake kijijini Mwamala, mwendo wa nusu saa toka nyumbani kwake, ujio wa simu za mkononi baada ya kuwekwa minara ya simu kijijini hapo, umemwezesha kutunza pesa zake kwa usalama katika simu.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho (Singita), Julius Kasenga anasema utunzaji wa pesa kupitia simu za mkononi kijijini hapo, umepunguza vilio vya kuibiwa pesa njiani au nyumbani, pesa kuharibika au kuliwa na mchwa na pia, umepunguza matumizi mabaya ya watu kutokana na kutembea na pesa mifukoni.

“Hata yale magomvi ya watu kwenye familia kudai wameibiana, yamepungua na pengine kuisha kabisa. Kwa kweli hii simu zimeleta usalama hapa kijijini maana unapata huduma za benki hapo hapo ulipo, na wakati wowote,” anasema Mwenyekiti huyo.

Deogratius Chubwa ambaye ni kiongozi wa Timu ya Masoko wilayani Kasulu katika Mkoa wa Kigoma wa kampuni ya Vodacom, anasema licha ya kuwapo changamoto ndogondogo za kiufundi, utunzaji, upokeaji na utumaji pesa kupitia simu umekuwa ukombozi na usalama dhidi ya wizi na ujambazi kwani hata simu ya mtu ikipotea, pesa hubaki salama mradi tu, mtu atunze namba ya siri.

Kayanda Thobius wa Kata ya Kumsenga wilayani Kasulu, anasema uwepo wa minara ya UCSAF umeongeza idadi ya watumiaji wa simu wanaotuma, kupokea na kutunza pesa kupitia simu za mkononi na hivyo, kuufanya uwakala wa MPesa kumpa kipato kinachoendesha maisha yake na familia.

“Hizi M-Pesa (anamaanisha simu za mkononi), zimenipa heshima kubwa maana hii ndiyo benki pekee ya watu wa vijijini wanayoipata muda wowote; kwa muda mfupi na karibu. Unajua watu wanaipenda kwa kuwa ni benki inayotunza, kutuma, au kupokea hata shilingi 200. Hii minara imetusaidia,” anasema Kayanda.

Maria Tunu wa Kijiji cha Mahembe Kigoma anasema minara hiyo imewafungulia milango watu wa vijijini kupata mikopo ya fedha na kuirejesha, bila masharti magumu. “Hata mimi ninaweza kukopa, bila kuambiwa niweke kiwanja au leseni (dhamana) au hofu ya kuuziwa vitu vyangu ndiyo maana ninazishukuru hizi simu kwa kuleta benki; tunaweka pesa salama, na tunakopa bila masharti magumu, mradi tu, uwe mwaminifu,” anasema Maria.

Mwingine anayethibitisha ukombozi wa UCSAF kuwezesha maeneo ya vijijini kupata mawasiliano ya simu na hivyo kutumia simu za mkononi kuhifadhi fedha zao salama ni Ngasa Kapongo, mkulima na mfugaji kijijini Lagana katika Wilaya ya Kishapu Shinyanga.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nsimbo wilayani Kaliua, Fatuma Juma huku akizitaja M-Pesa, HaloPesa, TigoPesa na AitelMoney anasema, “Simu zimetuwezesha kukopa na kurejesha tofauti na zamani, ambapo kama siyo ndugu yako kukukopesha, huna pa kukimbilia.”

JUZI iliibuka taarifa katika mitandao ya kijamii juu ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi