loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kenya wanapenda kazi yangu kuliko Tanzania- Msechu

Kenya wanapenda kazi yangu kuliko Tanzania- Msechu

Ni msanii aliyepata umaarufu kutokana na mashindano ya kusaka vipaji ya Bongo Star Search, (BSS) mwaka 2009 akiwa ni mshiriki kutoka mkoa wenye vipaji vingi vya muziki, Kigoma. Alizaliwa miaka 26 iliyopita mkoani humo katika familia ya watoto wanne, na yeye akiwa ni wa pili. Wazazi wake ni wenyeji wa kijiji cha Kifula, Ugweno Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Sababu kubwa ya kutokea Kigoma, ni kwa sababu baba yake alikuwa akiishi kule kikazi, hivyo wao wamezaliwa ndani ya mkoa huo. Ni msanii anayejivunia kutoka familia ya wanamuziki wa kwaya, kuanzia baba yake mzazi, mama yake, dada, kaka na hata babu yake aliwahi kuwa mwimbaji wa kwaya miaka ya zamani.

Kitendo cha kuacha kwaya na kujiingiza katika muziki wa kizazi kipya hakikufurahisha baadhi ya wanandugu, ingawa ndiko mapenzi yake yalikoegemea. Muziki ulikuwa katika damu yake kiasi kwamba baada ya kumaliza elimu yake ya sekondari mwaka 2009, mwaka huo huo akashiriki kwenye mashindano ya BSS ili kujaribu kuendeleza kipaji chake.

Kutokana na kukubalika haraka, wakati huo alipata nafasi ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza na hivyo kupata matumaini ya kutimiza ndoto zake. Kwa watu waliokuwa wakifuatilia mashindano hayo, hakika wanamtambua vizuri kwani alikuwa ana uwezo wa kucheza na kuimba. Bila kujali umbo lake nene, ni mwepesi katika kucheza.

Mashindano hayo yalimpa umaarufu mkubwa, kwani alikuwa akiwafurahisha mashabiki wake na kuwaburudisha vilivyo hasa inapofika zamu yake ya kuimba, hata kama ulikuwa umenuna utajikuta unacheka mwenyewe kutokana na manjonjo yake ya kucheza. Umahiri wake wa kuimba ulimfanya kupata kura nyingi na hivyo kufanikiwa kushika nafasi ya pili wakati huo, ingawa matumaini yake makubwa alitamani kuchukua nafasi ya kwanza.

Hata hivyo, kushika nafasi hiyo hakukupoteza matumaini yake ya kuendelea na muziki bado alikuwa na nia hivyo mwaka 2010 alijaribu bahati yake tena kwa kushiriki kwenye mashindano ya Tusker Project Fame iliyokuwa ikiwashirikisha wasanii wa muziki kutoka nchi za Afrika Mashariki.

Katika mashindano hayo, Msechu aliendelea kujenga jina lake na kukubalika ukanda wa Afrika Mashariki kwani alipata mashabiki wapya waliokuwa wakimpigia kura. Alifanikiwa kushika nafasi ya pili, nyuma ya Paschal Cassina aliyeshika namba moja, na hivyo kumsaidia kusogea mbele katika kupiga hatua nyingine kimuziki.

Mbinu ambazo alikuwa akizitumia alipokuwa kwenye mashindano ya kwanza alitumia tena kwenye ya Tusker. Mwaka 2011 Msechu alirudi tena Tusker Project Fame kugombea nafasi tatu za juu zilizoshirikisha mastaa wa mashindano hayo yaliyopita na kuzidi kutakatisha jina lake kwa mara nyingine ambapo alishika nafasi ya tatu.

“Kwa kweli nashukuru Mungu mashindano yote hayo yaliniimarisha na kunifanya nijulikane na kukubalika haraka kwa mashabiki wa ukanda wa Afrika Mashariki, leo hii najivunia na hilo,” anasema. Tangu ameanza muziki wake kwa kipindi kifupi tayari amefanikiwa kutoa nyimbo saba.

Lakini zinazovuma zaidi na kumpa chati katika muziki wa Afrika Mashariki ni Hasira Hasara, Majaribu, Unaniumiza roho, Relax na Kumbe. Anasema amekuwa akipata mialiko ya kupiga shoo katika nchi za Kenya, Tanzania, Uganda na sehemu nyingine. Zaidi anawakubali mashabiki wa Kenya kwa kuunga mkono muziki wake kwa asilimia kubwa kuliko Tanzania.

“Nawashukuru Kenya wamekuwa wakiniunga mkono kwa asilimia kubwa ukitofautisha na hapa nyumbani, nimefanya shoo nyingi huko, hata ninapoenda kupiga shoo watu ni wengi, nafurahi na nawaomba kuendelea na moyo huo huo,” anasema Msechu ambaye kwa sasa ana mchumba na mtoto mmoja wa kike aitwaye Laureen.

Msechu anasema hajatoa albamu na mpango utakuwepo kuanzia mwakani ambapo anatarajia pia kuanza mwaka mpya na nyimbo nzuri zitakazowaburudisha mashabiki wake.

Msanii huyo ana malengo makubwa ya kuboresha muziki wake na mojawapo ni kuhakikisha kuwa akialikwa katika shoo anapiga muziki wa ‘live’ . “Hili ni lengo langu la kwanza na tayari nimeanza mchakato wa kuimba ‘live’ kwenye shoo zangu, lengo ni kuhakikisha naimba kimataifa zaidi, na najifunza mengi,” anasema Msechu.

Lengo la msanii huyo sio kwamba anasubiri hadi anunue vyombo vyake, bali yuko tayari kuazima kwa wenzake ili kufanya kazi nzuri na kujijengea heshima. Anasema ikiwa atafanikiwa baadaye atanunua vyombo vyake ili kurahisisha kazi zake. Jambo ambalo anajivunia kwa sasa anasema anaendelea na ujenzi wa nyumba yake na tayari ana usafiri.

Lakini kwake anaona hivyo ni vitu vya kawaida, zaidi amelenga kuboresha muziki wake ili uzidi kufanya vizuri kila siku. Licha ya mafanikio kidogo aliyopata tangu ameanza muziki huo, anasema changamoto kubwa anayokutana nayo ni pale ambapo amekuwa maarufu kwani ana kazi kubwa ya kujichunga.

“Kuwa staa ni kazi inabidi ujichunge usije ukafanya mambo ya ajabu, jamii inakutazama, unatakiwa uwe makini kweli, wakati mwingine watu wanaweza kukufikiria hivi kumbe sivyo,” anasema. Anasema jamii wakati mwingine hufikiri staa ni mtu mwenye maisha mazuri kumbe inaweza ikawa ni tofauti.

Msechu anasema ili msanii aweze kutimiza ndoto zake za kuwa msanii mkubwa wa kimataifa ni kubadilika na kufanya muziki mzuri. Msanii huyo siku za karibuni aliwahi kuzungumzia suala la kuungwa mkono, na kuelezea utofauti wa Tanzania na Kenya. Anasema Kenya iko mstari wa mbele kuwapa nafasi wanamuziki chipukizi ukilinganisha na nyumbani hapa.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi