loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kibali cha kuomba mitaani !

Hata hivyo, si wote wanaosherehekea mavuno. Wapo baadhi wanaoendelea kulia njaa. Wakati wenzao wakivuja jasho vijijini kwa kulima, wao hukimbilia mijini kuomba. Wakati wenzao wakivuna, wao wanaendelea kuzunguka mitaani na bakuli wakiomba fedha na chakula.

Utawakuta barabarani, kwenye baa, stendi za magari na hata majumbani wakiomba. Watoto kwa wakubwa, wanaume kwa wanawake, wamegeuza kuombaomba ajira ya kudumu. Wapo wenye ulemavu hususani wa kutoona ingawa baadhi wanadaiwa kuwa na wa bandia.

Baadhi wameamua kutumia vibali maalumu; tena vyenye mhuri wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kurasimisha kuomba mitaani. Nimeshuhudia mwanamke akiwa na kibali husika akijinadi kuwa na ugonjwa wa kifafa.

Akiwa amevalia vazi maridadi la kitenge huku akionekana ni mwenye nguvu na siha njema, mama huyo hashughuliki kujieleza kwa mdomo.

Baada ya kufika kwenye meza yenye wateja waliokuwa wakijipatia chakula, alitoa barua enye mhuri wa Serikali ikimwelezea ana ugonjwa wa kifafa. Ilielekeza, atakapohitaji msaada apewe bila usumbufu.

Miongoni mwa mambo niliyobaini kwa huyo mama ni kwamba, ukitaka kuporomoshewa maneno, anza kumhoji undani wa maisha yake. Utajuta kuzaliwa! Cha msingi akikuonesha hiyo barua, kama una nia na hutaki maneno, basi ingia mfukoni mwako mtolee kuanzia Sh 500 na kuendelea halafu mwache aende zake.

Lakini ukijitia kiherehere cha kuanza kumhoji, ‘unaishi wapi, unaishi na nani, kwa nini unaomba wakati una nguvu’, utajuta pale utakapoporomoshewa laana na matusi ; tena kwa sauti mbele ya kadamnasi. Jambo ambalo nimekuwa nikijiuliza, ni je, vibali hivyo vya kuomba omba, ni kweli hutolewa na ofisi hiyo ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma?

Najiuliza zaidi, je, kuomba ni ajira inayotambulika kiasi cha kupewa kibali? Je, kama ni kweli mama huyo ana kifafa, ofisi hiyo ya Serikali haina msaada endelevu kwa watu kama hao zaidi ya kuruhusu kuomba mtaani?

Nimeendelea kujiuliza, je urahisi na hatari iko wapi kwa mwenye kifafa; kati ya kuzunguka mitaani kuomba au kulima shambani au kuendesha biashara ndogondogo? Katika kujaribu kujijibu maswali haya, nikaja na majibu kwamba uko uwezekano wa baadhi ya watu kughushi nyaraka za Serikali ikiwemo mihuri kuonesha kuwa wamehalalishwa kufanya vitendo hivyo.

Hata hivyo pamoja na majibu hayo ya kujaribu kutetea ofisi ya Mkuu wa Wilaya, najiuliza tena, kama kibali hicho hakijawahi kutolewa, kwa nini ombaomba hao wasikamatwe?

Ukiacha ukweli kwamba watu hao wanaoomba huonesha vibali husika kwa uwazi, mkono wa Serikali ni mrefu kiasi kwamba ni nadra ofisi ya Mkuu wa Wilaya kutumika isivyo halali bila wahusika kubainika. Bila kujali kama ombaomba hao wamepewa vibali au wameghushi, ukweli ubaki kwamba juhudi za makusudi zinahitajika kudhibiti kuomba mtaani. Nafahamu ni vigumu mji wowote kukosa ombaomba. Maana hata kwenye nchi zilizoendelea, watu hao wapo lakini si kwa kiwango cha juu kama ilivyo mjini Dodoma. Kasoro ninayoona, ni baadhi ya wanaoomba kuonesha kana kwamba Serikali inabariki vitendo hivyo kutokana na uwepo wa vibali kama hivyo.

Hata kama mtu ana ulemavu unaohitaji msaada, si sahihi kumhalalishia kwamba kuomba ndiyo tegemeo la maisha yake. Badala yake, aoneshwe njia ya kuendesha maisha yake bila kudhalilisha utu wake kwa kuomba mitaani. Laiti kama lingekuwa tatizo la dharura linalohitaji msaada wa haraka, kidogo ningeweza kukubali japo kwa shingo upande.

Lakini kwa tatizo kama vile ugonjwa wa kifafa, sioni mantiki kwa kiongozi wa aina yoyote kukubali kwamba kuomba mitaani ndiyo suluhu.

Matumizi ya nyaraka hizi zenye mihuri ya Serikali, kuomba mitaani, kunadhalilisha siyo tu mamlaka inayohusika, bali taifa machoni pa wageni.

Kama kweli ofisi ya Serikali imeshiriki kuidhinisha vibali hivi, ni vyema ikawasaka na kubatilisha vibali hivyo; kisha zitafutwe njia nyingine za kusaidia wenye mahitaji ya kweli. Ikiwa mamlaka hazijawahi kutoa vibali husika, ni wakati mwafaka kusaka wote wanaotumia nyaraka zenye mihuri inayodaiwa kuwa ya Serikali, hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao. twessige@yahoo.com

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Riadha ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi