loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kigodoro kinavyochochea mimba kwa wanafunzi Kisarawe

"Wanapoenda kwenye ngoma usiku, mambo wanayofanya huko ni makubwa, wanalewa, wanafanya ufuska na kupata ujauzito huko kwenye ngoma. Kwa mtoto wa kike ina athari kubwa zaidi huku kwa mtoto wa kiume athari zinajitokeza mwishoni kwani hawezi kufanya vizuri masomo yake," anasema Mohamed Kilinga.

Kilinga ni mwenyeji wa kijiji cha Kibuta na ni mtendaji wa kata hiyo, kazi ambayo ameifanya sasa kwa muda wa miaka 16. Anasema katika uhai wa ajira yake, ameshuhudia ngoma namna zinavyoathiri sekta ya elimu katika kata hiyo. Anasema wasichana wengi ambao wamepata ujauzito wakiwa shuleni, chanzo kikubwa ni ngoma.

"Sisi tuliwahi kwenda kumkurupusha msichana ambaye aliachishwa shule na akawekwa ndani na mzazi wake ili amcheze mwali, tulipewa taarifa na walimu.

"Nilichukua mgambo wa kata tukaenda hadi nyumbani kwa huyo mzazi, tukamkamata na kumkurupusha binti yake na kumpeleka shuleni maana alikuwa kidato cha nne na alikuwa anakaribia kufanya mtihani," anasema Kilinga.

Kilinga anasema katika kata yake amepiga marufuku wanafunzi wa darasa la saba na wale wa kidato cha nne kuwekwa ndani wakati wanakabiliwa na mitihani.

Anasema utekelezaji wa jambo hilo umekuwa jepesi maana wanashughulika na wazazi, ambao kwa sasa wanaogopa kuswekwa ndani.

Anasema wanashauri zaidi wasichana wanaosoma shule, wachezwe ngoma wakati wa likizo ili kutoa fursa kwa binti huyo kuhudhuria shule na kupata haki yake ya elimu. Anashauri kuwa Serikali ingepiga marufuku ngoma hiyo ichezwe mwisho saa 12 jioni na sio kukesha kama ilivyo sasa.

"Kama ingekuwa inaishia saa 12 hizi athari kwa watoto wa kike zingepungua maana wangeona aibu kulewa mchana na kufanya ufuska huo."

Mkuu wa Shule ya Sekondari Kibuta, Mussa Juma, anasema wanafunzi wake ni miongoni mwa wanafunzi ambao wamekatishwa masomo kutokana na athari za kigodoro.

Anasema ngoma hii inayokesha kwa siku mbili ni hatari kwa ustawi wa elimu wilayani Kisarawe, kwani hakuna kizuizi watu wazima, vijana, wanafunzi wote wanaenda kokote inakopigwa.

"Ngoma inapigwa pembeni kunauzwa bangi na gongo, vyote hivi vinauzwa hadharani...ili ucheze vizuri hiyo ngoma ni lazima ulewe," anasema Juma.

Juma anaongeza kuwa ni kwenye ngoma hiyo wanafunzi wengi wanapata ujauzito maana wanajikuta wakati wanacheza wanalewa na hatimaye kwenda kufanya ngono na mwanaume.

Ngoma hiyo inapigwa wakati wote kwa mwaka mzima isipokuwa wakati wa mfungo wa mwezi wa Ramadhani tu ambao Juma anasema katika kipindi hicho ngoma hiyo haipigwi kutokana na wakazi wengi wilayani humo kuwa wafuasi wa dini ya Kiislamu.

Anasema yeye shuleni kwake, amewatangazia wazazi kuwa ni marufuku kuwacheza wanafunzi wakati wa masomo, hivyo amezungumza na wazazi kuwa wafanye shughuli hiyo wakati wa likizo.

"Ni jambo gumu kulisimamia, lakini kwa kiasi fulani nashukuru kwamba, wakati wa likizo wanafunzi wake wengi wanachezwa... utaona tu msichana anarudi kutoka likzo kabadilika, ameshakua mtu mzima hapo unajua tu kuwa huyu keshachezwa," anasema Juma.

Juma anashauri pia kuwa kwa kuwa ni ngumu kuzisimamisha mila hizo, ni bora jamii ikaelimishwa ili ngoma hizo ziwe zinachezwa mchana hadi saa 12 kuliko kukesha kwa siku mbili au tatu, kwani athari zake kwa jamii ni kubwa zaidi.

Baraka Athumani ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Kibuta, anasema Vanga ni ngoma inayopenda sana kijijini hapa na yeye anakiri kuwa huwa anahudhuria kwenye ngoma hiyo ambayo siku hizi imekuwa maarufu kama kigodoro.

"Kwetu ilishapigwa wakati dada alipokuwa anatoka kwenye umwali, aliwekwa ndani kwa miezi mitatu wakati huo wanasoma shule ya msingi," anasema Baraka.

Ali Rajabu anasema dada yake ambaye ni mwanafunzi wa sekondari aliwekwa ndani kwa wiki mbili na kigodoro kilipigwa kwa siku mbili nyumbani kwao.

"Ni kweli pale watu wanakunywa sana pombe na hata bangi inauzwa." Aisha Mohamed, mwanafunzi wa sekondari ya Kibuta akizungumzia suala hilo la ngoma anasema yeye aliwekwa ndani lakini wakati wa likizo.

"Mimi baba yangu ni mwelewa nilichezwa wakati tukiwa likizo na hivyo sikuachishwa masomo."

Anakiri kuwa kuna wanafunzi wenzake wengi tu ambao wanachezwa wakati shule zinaendelea " Hilo ni suala la uamuzi wa mzazi mwenyewe, binti huna sauti wewe ni mtu wa kuambiwa tu kwamba unawekwa ndani na hakuna kubisha."

Alipoulizwa kama yeye ameshahudhuria ngoma tofauti na ile aliyochezwa, anakiri kuwa ni kweli huwa anaenda, lakini zaidi mchana kwani usiku baba yake anamkataza asiende huko kutokana na matendo machafu yanayoendelea hasa wakati wa usiku.

"Kwa kweli wakati wa usiku vitendo vibaya sana vinafanyika kwenye kigodoro, ndio maana sisi baba haturusu kwenda huko usiku, watu wanafanya ngono hadi kwenye mihogo," anasema.

Afsa Almasi ni mwanafunzi wa sekondari ya Kibuta mkazi wa kijiji cha Mlegele, anakiri kuwa kigodoro kimechangia wanafunzi wengi kupata ujauzito kwa vile huko ndiko wanapata fursa ya kwenda kukutana na wapenzi wao.

"Msichana ukiwa na mpenzi wako, wakati wa kigodoro ndio muda wa kwenda kukutana naye, jambo ambalo linachangia wasichana wengi kupata ujauzito. Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kisarawe, Mohamed Kahundi, akizungumzia anasema ngoma zinazohusudiwa na wananchi hazina uzuri kwani kwa kiasi kikubwa zinaingilia mfumo wa elimu.

Anasema mtoto akienda shule ngoma inavuruga mtiririko wake wa kusoma kwa sababu baadhi ya watoto wanawekwa ndani kwa muda wa mwaka mmoja na ndipo anachezwa ngoma. Anazipinga ngoma hizo kwa maelezo kuwa zinachangia kuharibu maadili kwa watoto, anasema mtoto anafundishwa mambo ya kukaa na mume wakati bado ni mdogo. "Huyo mtoto anachezwa na watu wazima, mambo anayoelekezwa ni makubwa kuliko umri wake."

Kaimu mkurugenzi huyu anasema ngoma zinachangia kuwepo kwa mimba za utotoni, ubakaji kukithiri na kuwepo kwa magomvi kati ya mume na mke.

"Mpiga ngoma wakati mwingine anagoma kupiga ngoma hadi apewe kanga, akipewa ya mke wa mtu ina maana hiyo kanga ni tiketi ya huyo mwanamke kwenda kufanya naye ngono, je mume wake akiona nini kitatokea hapo kama sio ugomvi?

"Na kibaya zaidi huyu mpiga ngoma asipopewa kanga, anagoma kupiga ngoma na watu hawatakubali ni lazima apewe hiyo kanga, anaweza kupewa ya binti ambaye hana mume na mwishowe ataenda kufanya ngono na mpiga ngoma akipata ujauzito ndio maana unakuta watoto wengi humu hawana baba," anasema Kahundi.

Kutokana na athari za ngoma hizo kwa elimu, Kahundi anasema halmashauri imepiga marufuku kucheza ngoma wasichana walioko shule ya msingi hadi pale watakapohitimu masomo yao.

Anaongeza kuwa kwa wale ambao wako sekondari wanashauri wasichana hao wachezwe wakati wa likizo.

Anasema pia kuwa halmashauri iko kwenye mchakato wa kutunga sheria ndogo za kupiga marufuku ngoma hizo, kwa maelezo kuwa zimeonesha kutokuwa na manufaa kwa jamii ya watu wa Kisarawe, badala yake zinazidi kudidimiza elimu na kusababisha kuzaliwa watoto wasio na baba.

"Hizi ngoma za vigodoro ni chafu kwa kweli ni heri zipigwe marufuku, hii itasaidia vijana wetu kujikita zaidi kwenye elimu," anasema Kahundi.

TAMKO la Kimataifa Kuhusu Haki za Binadamu (UDHR 1948), Mkataba ...

foto
Mwandishi: Shadrack Sagati

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi