loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kigodoro kinavyochochea mimba kwa wanafunzi

Jina kigodoro kwa mujibu wa baadhi ya watu ni kutokana na ukweli kwamba watu hukesha kwenye muziki ama ngoma ambao hugeuka kuwa 'godoro' lao! Umaarufu wake unatokana na kupendwa sana na watu, hususan vijana.

Ngoma hizo huko nyuma zilikuwa na majina kama mdundiko, charanga, vanga, mchiriku ama disko la usiku lakini mchanganyiko huu unapokesha ndio siku hizi umebatizwa jina la kigodoro.

Kisarawe ni moja ya sehemu ambako ngoma ama madisko ya kukesha (rusha roho) hufanyika sana. Takriban kila mwisho wa wiki kuna sehemu kuna kigodoro na hususan ngoma zinazotokana na mila za kumtoa mwali.

Mwali ni binti ambaye amevunja ungo, hivyo anawekwa ndani ambako anafundwa mambo mbalimbali, hususan yanayohusu majukumu ya kulea familia endapo atabahatika kuolewa na siku anapotolewa nje huwa ni sherehe inayoambatana na ngoma.

Ngoma hizi pia mara nyingi hutanguliwa na mikesha ya siku kadhaa. Hata kwenye harusi, ngoma hii inapigwa na inawavuta mamia ya watu wa rika zote kuanzia watoto, vijana na hata watu wazima.

Licha ya kuwa uchezaji wake wakati mwingine unakiuka maadili ya kitanzania, lakini ukweli ni kwamba ni ngoma inayochezwa mbele ya watu wa rika zote.

Godfrey Ambele, mtendaji wa kata ya Kisarawe, anasema ngoma ya vanga katika wilaya ya Kisarawe ni kitu ambacho kinathaminiwa sana kuliko hata elimu, hasa kwa vijana.

"Hivi vigodoro kwa kweli imekuwa tatizo kubwa na inachangia elimu wilayani kwetu hapa kuzidi kushuka kwa sababu hata watoto wa shule wanaruhusiwa kwenda mbali na kuwa uchezaji wake hauna maadili," anasema Ambele.

Ambele anasema zamani ngoma ya vanga kama kuna 'shughuli' mahala, ilikuwa inapigwa kwa wiki nzima lakini siku hizi serikali imepiga marufuku badala yake inachezwa kuanzia Ijumaa hadi Jumapili.

"Huko ni kucheza na kulea na matendo mengine machafu kama ya ngono," anasema Ambele na kuongeza kuwa "Shughuli inapokuwa vijijini, kutokana na umaarufu wake, baadhi ya wanandugu wanasafiri kutoka Dar es Salaam kuja kukesha kwa kucheza ngoma hiyo."

Anasema Serikali ya wilaya ya Kisarawe baada ya kuona athari za ngoma ni kubwa katika maendeleo ya elimu, ilipiga marufuku ngoma hizo, lakini wananchi walikuja juu kwa kusaidiwa na maofisa utamaduni kuwa kufanya hivyo ni kuua utamaduni wa Kizaramo. Anazidi kufafanua kwamba wananchi walilalamika hadi kwa viongozi wa kisiasa wa wilaya.

"Kama unavyojua wanasiasa ni watu ambao wanasaka kura na wananchi ndio mtaji wao, siasa waliingilia na ngoma hizo zikarejeshwa tena."

Wanchoke Chinchibera ni Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya ambaye anasema ngoma hizo licha ya kuendana na matendo machafu, hata mwali mwenyewe anapowekwa ndani anafundishwa mambo makubwa ambayo yako juu ya umri wake, ikiwa ni pamoja na namna ya kumridhisha mwanaume katika tendo la ndoa.

Anasema msichana anapotoka kwenye kufundwa, anataka kujaribu mambo aliyokuwa anafundishwa na makungwi, jambo ambalo anasema limechangia wasichana wengi kujikuta wanapata ujauzito wakiwa bado shuleni.

"Mtoto wa kike ana umri wa chini ya miaka 16 lakini anafundishwa namna ya kutunza mume, akitoka huko mawazo yamemkaa anataka kujaribu," anasema Chinchibera.

Mwalimu wa sekondari ya Masaki, Benjamin Ngomoka anasema wanafunzi wengi wanaacha shule kutokana na kuthamini kuchezwa ngoma.

"Kesi nyingi tulizo nazo hapa ni msichana kuacha shule na kwenda kuchezwa ngoma." Anatoa mfano wa binti mmoja ambaye alikuwa anajiandaa kufanya mtihani wa 'moku' lakini akawekwa ndani na mzazi wake ambaye aliandika barua shuleni kuwajulisha kuwa mwanafunzi huyo hatohuhudhuria shule kwa mwezi mmoja kwani desturi hazimruhusu kwenda shule wakati kawekwa ndani.

"Huyu binti kwa sasa haji shule na sisi suala hilo tumelipeleka kwa mtendaji wa Kata. Yeye ndiye mwenye kuweza kuchukua hatua," anasema Ngomoka.

Ngomoka anasema safari hii Baraza la Mtihani (Necta) linaunganisha alama za mtihani wa moku kwenye mtihani wa mwisho, hivyo kitendo cha msichana huyo kutofanya mtihani huo tayari anakuwa amejipunguzia alama.

Ngomoka anakiri mila ya kuchezwa ngoma kwa mabinti inapewa nafasi na umuhimu mkubwa na wananchi wa wilaya ya Kisarawe kuliko elimu.

Anasema wazazi wengine wanapeleka hata mwaliko kwa walimu shuleni hapo kuhudhuria ngoma ya kuchezwa binti zao ambao ni wanafunzi.

Anasema wanafunzi wa shule yake wengi wameathirika na suala hilo, na anasema licha ya kuwashauri wawacheze watoto wao wakati wa likizo, lakini imeshindikana na hivyo kujikuta wasichana baadhi wanawekwa ndani kwa wiki mbili au mwezi mmoja na hivyo kukosa masomo.

Mwalimu huyo anasema kwenye ngoma kwenyewe vitendo vingi vinavyofanyika vinahamasisha vitendo vya zinaa, hali ambayo imesababisha kuwepo na maambukizi makubwa ya Ukimwi wakiwemo wanafunzi.

Lakini Abbas Zembwe ambaye ni mwenyekiti wa kijiji cha Masaki, anatetea ngoma kuwa hiyo ni mila na desturi za Wazaramo na kamwe hawawezi kuziacha.

"Ngoma sio sababu ya wanafunzi kupata mimba, maana kinachofundishwa huko sio mambo mabaya bali mambo ya kumjenga msichana," ansema Zembwe.

Anasema kwenye ngoma watoto wanafundishwa maadili ya maisha, nidhamu anayopaswa kuwa nayo mtoto wa kike na wa kiume.

"Sisi wenyewe wakati tumeenda jando tulifundishwa maadili wakati tunatahiriwa." Hata hivyo, anasema ngoma kwa sasa sio jambo la lazima maana kuna familia ambazo hazichezi mabinti zao baada ya kuhisi kuwa zinachangia uvunjaji wa maadili.

"Pamoja na hayo, ngoma haziwezi kuathiri jamii kama zitakatazwa kabisa maana watoto wetu wanafundishwa maadili yote huko shuleni."

Pamoja na ukweli huo, Zembwe anasema sio rahisi kwa jamii ya Kizaramo kuachana na jambo hilo na ndio maana licha ya Serikali kutaka kuzipiga marufuku walikuja juu na akasema kwa sasa zinapigwa kuanzia Ijumaa jioni hadi Jumapili jioni, siku ambazo sio za shule wala za uzalishaji. Hata hivyo, anasema ngoma ya sasa inayoitwa kigodoro kidogo ina mushkeli tofauti na walizocheza wao.

"Hii ngoma ya sasa hivi wanayoita kigodoro kweli ni lazima nikiri kuwa inachangia kuharibu binti zetu hadi wanakuwa malaya."

Anasema kitendo cha ngoma kukesha, ni mahala ambapo huwa kuna pia ulevi wa kupindukia ukifanyika, jambo ambalo linaleta ushawishi wa watu kufanya ngono.

Anasema kwa kuwa ngoma hizo zinahudhuriwa hata na watoto wa shule, wanajikuta wakijifunza vitendo ambavyo si vizuri kwao kulingana na umri na majukumu yao ya shule.

Anapoulizwa kuhusu mmoja wa mwanakijiji wake kuandika barua shuleni ya kumweka ndani binti yake na hivyo kukosa mtihani wa moko, Zembwe anasema:

"Hilo jambo nimelisikia na limenisikitisha, huo ni ujinga wa mzazi mwenyewe."

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kifukumuko kilichoko katika kijiji cha Musimbu, Khalid Chamuwange, anasema kigodoro ni muziki ama ngoma inayohamasisha vitendo vya ngono na kwamba ni jambo ambalo haliwezi kukanushwa.

Anasema watu wanaotoka mjini kwenda kijijini huko kucheza ngoma hiyo, wengi maadili yao sio mazuri na hata wanapokuwa kwenye ngoma uchezaji wao sio wa maadili kwani wakati mwingine wanavua nguo na kubaki uchi. Chamuwange anasema wazazi wanachangia watoto wao kuwa malaya na hivyo anahoji:

"Wewe ni mzazi, mtoto wako yuko shule ya msingi. Kuna haja gani ya kumcheza ngoma na kumfundisha mambo ya kikubwa?" Chamuwange ambaye amezaliwa katika kijiji hicho cha Musimbu anasema, amefuatilia kuona kama ngoma zina faida na amegundua kuwa hasara ni kubwa kuliko faida.

"Mimi hapa sitamcheza binti yangu, hakuna faida yoyote." Anasema unakuta mtu ni maskini, lakini anaamua kumcheza binti yake kwa gharama kubwa na baada ya ngoma hiyo binti anaenda kujaribu aliyofundishwa huko na hatimaye anapata mimba.

Mwenyekiti huyo wa kitongoji anasema pamoja na Serikali kupiga vita ngoma ya kigodoro, lakini jamii wanaipenda ndio maana suala hilo limeshindikana kuachwa licha ya kuwa limechangia kudidimiza elimu wilayani Kisarawe.

Kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa ...

foto
Mwandishi: Shadrack Sagati

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi