loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kijiji kinachoongoza kuwa na watoto pacha

Kijiji hicho kilicho umbali wa kilometa 30, kutoka wilaya ya Malappuram, kina idadi ya watu takribani 2,000 lakini kina pacha 350, na hivyo kuweka rekodi ya kijiji chenye pacha wengi kuwahi kutokea duniani. Maajabu hayo yameshangaza ulimwengu kwani kwa takwimu za mwaka 2008 pekee, wanafamilia 15, walipata pacha.

Hata hivyo wataalamu wa afya wanashangaa hali hiyo na kushindwa kuna sababu za kisayansi. Matukio ya kijiji hicho kwa wanafamilia kujifungua watoto pacha yalianza kutokea miaka kati ya 60 hadi 70. Kwa tafiti za afya duniani zinaonesha kuwa wastani wa watoto pacha kuzaliwa ni pacha sita kwa vizazi hai 1,000.

Lakini katika kijiji cha Kodinhi, hali ni tofauti ambapo kwa kila vizazi hai 1,000 wanazaliwa pacha 42 na hiyo ni kusema kuwa ni zaidi ya asilimia 700 ya wastani wa pacha kuzaliwa duniani.

Hata hivyo, uchunguzi wa kitabibu unaonesha kuwa India kwa ujumla ni miongoni mwa nchi zenye idadi ndogo ya watoto pacha, lakini kijiji hicho kimeshangaza na kuwa karibu na takwimu za kimataifa za maeneo yenye idadi kubwa ya watoto pacha.

Katika kijiji hicho kwa sasa kuna pacha wa rika mbalimbali, ambapo wapo watoto, vijana, watu wazima na wazee na kwamba pacha hao wako katika makundi mawili; pacha wanaofanana na wasiofanana.

Kutokana na wingi wa pacha katika kijiji hicho, ni rahisi kukutana na pacha mmoja dukani na mara unakutana na mwingine sokoni na kushindwa kujua yupi ni yupi. Shuleni ndio wengi kabisa na hata maofisini na hivyo kama ni mgeni unaweza kuchanganyikiwa.

Hata hivyo, wingi wa pacha umekuwa ukileta ugumu kwa walimu shuleni kwa kushindwa kuwatofautisha pacha hao, kwa kuwa wengi wao wanafanana. Jambo hilo pia linawawia vigumu hata wananchi wa kawaida kushindwa kuwatofautisha pacha hao na yapo baadhi ya matukio ambayo yalisababisha kuwachanyanga pacha hao.

Tukio mojawapo ni la kijana mmoja aliyekuwa amemchumbia pacha mmojawapo ila alishindwa kumfahamu siku ilipowadia kwa kuwa wote wanafanana akashindwa kumtambua mchumba wake.

Hata hivyo jopo la madaktari wamejaribu kuchunguza chanzo cha kuzaliwa kwa pacha hao bila mafanikio na kwamba zaidi ya pacha 220 walizaliwa kwenye familia 2,000.

Watafiti kadhaa wameshatembelea kijiji hicho kilichopo kwenye Jimbo la Kerala na kufanya utafiti wao ambapo wameshindwa kubaini chanzo kwani pacha wanaozaliwa kiijijini hapo ni zaidi ya wastani wa mara sita ya kiwango cha pacha wanaozaliwa duniani.

Miongoni mwa madaktari waliofanya utafiti ni pamoja na Dk Krishnan Sribiju , daktari mzalendo wa nchi hiyo ambaye pia ni mtaalam wa masuala ya watoto pacha, amefanya utafiti wake kwa miaka miwili.

Dk Sribiju anasema ingawa katika kijiji hicho pacha hao 220, waliozaliwa kwenye familia 2,000 wameandikishwa kwenye kitabu kijijini hapo lakini idadi ya pacha hao ni zaidi ya hao walioandikishwa.

Hata hivyo, bado wataalamu wanachunguza iwapo matukio ya kuzaliwa kwa pacha hao yanatokana na kinasaba, maumbile, kurithi au sababu za mabadiliko ya hali ya hewa, na kwamba hivyo vyote vimeingizwa katika utafiti ili kubaini kwa nini kijiji hicho wananchi wake wanazaa pacha zaidi.

Cha kushangaza ni kwamba wanawake wanaoolewa kijijini hapo wanaolewa na watu ambao pia nao walizaliwa pacha, hivyo kusababisha muendelezo wa wao kuzaa pacha na kwamba hata wakienda kuolewa nje ya eneo hilo, huzaa pacha! Jambo hilo hivi sasa limeachwa kwa watafiti kubaini chanzo cha pacha hao kimetokana na nini.

Kwa mujibu wa takwimu za kijijini hapo, pacha wazee zaidi kuzaliwa kijijini hapo walizaliwa mwaka 1949. Na kwamba kadri miaka inavyosonga ndivyo idadi ya pacha nayo inazidi kuongezeka. Kuna takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya pacha 79 kijijini hapo wana umri kati ya miaka 0 - 10.

Utafiti uliofanywa kwenye Chuo Kikuu cha Lagos cha Tiba, kilitoa pendekezo kuwa kuna aina ya kemikali iliyopatikana kwa wanawake wa kabila la Igbo-Ora ambayo huenda ikachangia kusababisha kizazi cha pacha.

Lakini kwa matukio ya kijiji cha Kodinhi, utafiti huo unaweza usiwe sababu kwa kuwa hakuna uhusiano baina ya kemikali hiyo na uzazi na kwamba bado matukio ya uzazi wa pacha katika eneo hilo bado ni kitendawili! Wakati watafiti wakikuna vichwa kupata chanzo cha pacha hao, mhamiaji aliyerejea kutoka Ghuba kuja kikijiji hapo T. Abdul Razak (58) anasema hiyo ni siri ambayo Mungu anaijua na matukio hayo ni “Zawadi ya Mungu”.

“Hiyo ni siri ya Mungu hakuna sababu ya kufanya utafiti, ni zawadi kutoka kwa Mungu,” anasema Razak.

Mwaka 2008, takriban pacha 30, ambao ni familia wakiwa baba, mama na watoto waliunda umoja wao kijijini hapo na hilo likawa tukio la kwanza kufanywa likiwa na lengo la kutoa angalizo na kuomba familia hizo kusaidiwa, kwa kuwa wanakabiliwa na matatizo ya elimu na afya, kutokana na wao kuwa na idadi kubwa ya watoto pacha.

Hayo ndio maajabu ya Kijiji cha Kodinhi, ama kweli duniani kuna mambo!

Makala haya yameandaliwa na IKUNDA ERICK kwa msaada wa mtandao.

MWANAHARAKATI mmoja anayejiita Mimi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi