loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kikwete alivyoguswa na walioacha shule Ruvuma

Kuna jambo limenivutia wakati wa ziara ya Rais Kikwete Ruvuma, anajivunia kuwa na mke mwalimu.

“Yule pale mke wangu, yule ni mwalimu,” anasema anapozungumza na wananchi katika Kijiji cha Lumecha wakati akiwa njiani kwenda mjini Namtumbo. Si hivyo tu, Rais Kikwete anawathamini walimu, katika maeneo mbalimbali, baada ya kuzungumza na wananchi, aliwaita wapige picha. “asanteni, nyie watu wazuri, kwaherini, na watoto someni,” anawaaga wananchi wa Lumecha.

Rais anakumbuka agizo kuhusu ujenzi wa maabara katika kila shule ya sekondari na amedhamiria kulitekeleza. “Hili la maabara lipo clear (wazi), Novemba lazima wamalize, anayeshindwa ninaye,” anasema.

Ameagiza viongozi wote wakiwemo wa Halmashauri na madiwani wahakikishe agizo lake linatekelezwa, yeye atapeleka vifaa. Novemba mwaka huu kila shule ya kata iwe na maabara ya physics (fizikia), chemistry (kemia), na biology (biolojia),” ameagiza Rais Kikwete. Wakati anazungumza na viongozi wa Mkoa wa Ruvuma mjini Tunduru, Rais Kikwete anasema “Hili sisemi sana, tutaulizana Novemba.”

Kasi kubwa ya wanafunzi mkoani humo kuacha shule imemkera Rais Kikwete, anataka majibu ya uhakika sababu za kuwepo tatizo hilo, na ameagiza limalizwe haraka. “Elimu, ninyi mkoa huu mna mtihani mkubwa…safari yenu ni ndefu kweli,” anasema. Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa anafahamu changamoto kubwa ya elimu mkoani Ruvuma, na anatambua pia umuhimu wa elimu kwa watoto.

“Nchi hii inaendeshwa kwa mpito, leo tupo sisi, kesho vijana wetu watakuja kutuongoza,” anasema Kawawa. “Nasisitiza ndugu zangu wana Ruvuma, chonde chonde tusimamie watoto wetu waende shule,” anasema. Rais Kikwete anataka majibu kuhusu wanafunzi wanaonza shule za msingi na sekondari lakini hawamalizi, kwamba ni kwa nini hawamalizi, wapo wapi, wanafanya nini, na kwa nini wapo huko.

Kwa mujibu wa Kikwete , jambo la mtoto kutomaliza shule ni baya, ameagiza wanafunzi wanaoacha shule watafutwe mapema waendelee kusoma. Kwa mujibu wa kiongozi huyo mkuu wa nchi, kiwango cha wanafunzi wasiomaliza shule hakikubaliki, tatizo hilo lazima limalizwe haraka.

Rais Kikwete amewaagiza viongozi mkoani Ruvuma wajiulize watafanya nini ili watoto walioacha shule warudi shuleni kuendelea na masomo. Rais anasema, kuna tatizo kubwa la mimba kwa wanafunzi mkoani Ruvuma, na kama shule hazitakuwa na hosteli jambo hilo baya litaendelea.

“Hili na hosteli mlifikirie sana, na hili la school feeding (chakula kwa wanafunzi shuleni)…school feeding program ni muhimu, usiwe uji tu, waongeze lishe,” anasema.

Anasema, kama kasi ya sasa ya wanafunzi kuacha shule itaachwa iendelee, baadaye kutakuwa na tatizo kubwa la kuwa na mpango wa elimu kwa waliokosa. “Kwa nini huyu alipata fursa ya kusoma, akaacha shule halafu sasa mnaanza kuhangaika na mpango wa elimu kwa aliyekosa,” anasema Rais Kikwete mjini Tunduru alipozungumza na viongozi wa Mkoa wa Ruvuma kabla ya kumaliza ziara ya siku saba.

Rais Kikwete amewaagiza viongozi wa mkoa huo, ifikapo Agosti nane mwaka huu, wawe wamewasilisha kwake mpango wa kukabiliana na tatizo la watoto kutomaliza shule. Kwa nyakati tofauti, Rais Kikwete anasema, wanafunzi wengi hawamalizi shule kwa sababu viongozi si makini na kwamba, Serikali haiwezi kuacha hali hiyo iendelee hivyo ni lazima tatizo hilo lipatiwe ufumbuzi haraka.

Amewaeleza mamia ya wananchi wa Namtumbo kuwa, anafahamu kwamba, baadhi ya wanafunzi hawamalizi shule kwa sababu ya kupata mimba, hivyo amewauliza wanaume ni uhodari gani kumpa ujauzito mwanafunzi. Amewataka wanaume wawaache wanafunzi wa kike wasome, wawafuate wakubwa wenzao kwa kuwa kuna wanawake wengi wanaotafuta wanaume.

Kwa mujibu wa Rais, kufanya ngono na mtoto wa kike ni tabia mbaya na si uhodari. “Uhodari wa kuhonga pipi? Tafuta wazee, mzee mwenzako mzungumze ili mpishane maneno…kuna wanaume wa hovyo tu,” anasema.

“Wanawake wapo wengi wanaotafuta wanaume lakini unataka wanafunzi tu…uhodari huu, uhodari wa kuhonga pipi? Mtoto wa shule aachwe asome… ndiyo maana mke wangu ana msemo hapa, Mtoto wa mwenzio ni mwanao,” anasema na kubainisha kuwa mimba kwa wanafunzi zimekithiri mikoa ya Kusini na Pwani.

Mke wa Rais Kikwete, Mama Salma Kikwete anasema, watoto wa kike wanastahili kupata fursa ya kupata elimu badala ya kuozeshwa wakiwa wadogo na amependekeza wanaooa wanafunzi wafungwe jela.“Kumpa mume darasa la tano si wakati wake, kumpa mume kabla ya matokeo si wakati wake.” “Wafungwe hawa, akifungwa mmoja hawatarudia wengine, huku mimba ni nyingi, ni nyingi kupita kiasi,” anasema.

“Ninyi wazee msiwape hawa watoto mimba, mtoto wa mwenzio ni mwanao kama uliyemzaa, ninyi vijana msiwape watoto mimba, kwani dada yako anaweza kuwa mpenzi wako, mwiko, haiwezekani hata kidogo,” alisema Mama Salma. Rais Kikwete ameamuru wanaume waliooa wanafunzi wasakwe washitakiwe mahakamani wajibu mashitaka ya ubakaji na pia ameagiza wasichana wanaopaswa kuwepo shuleni lakini hawapo huko watafutwe warudi kuendelea na masomo.

“Mtoto wa shule hatakiwi kuwa mama wa nyumbani, mtoto wa shule anatakiwa awepo shuleni,” anasema Rais. “Lazima nipate majibu, wapo wapi, kwa nini, lazima mchukue hatua, hao wengine wapo wapi?” Anauliza Rais Kikwete kwenye mkutano wa hadhara mjini Namtumbo wakati akiendelea na ziara mkoani Ruvuma iliyoanza Julai 17 mwaka huu.

Rais anaagiza maofisa elimu shule za msingi na sekondari watoe taarifa kwenye Baraza la Madiwani kuhusu mahudhurio ya wanafunzi na pia walimu watoe ripoti kama hiyo kuhusu wanafunzi waliopo na wasiokuwepo ili hatua zichukuliwe haraka. Anatoa mfano kuwa, wanafunzi 4,509 tu walihitimu darasa la saba wilayani Namtumbo mwaka jana kati ya 7,520 waliokuwa wameanza darasa la kwanza.

Amesema, mwaka 2010, wanafunzi 18,892 walianza masomo ya sekondari mkoani Ruvuma, lakini 9,968 tu ndiyo waliohitimu hivyo kumaanisha kuwa, watoto 8,924 hawakumaliza ambao ni sawa na asilimia 48. “This is bad (jambo hili ni baya), asilimia moja, mbili, tatu, ni kawaida, lakini asilimia 48 haikubaliki,” anasema.

“Viongozi wa mkoa mkae mlizungumze, mkae mlizungumze mkitoka hapa, it is a serious matter, very serious,” anasema Rais Kikwete. Anatoa mfano kuwa, mwaka 2007 watoto 9,900 waliandikishwa kuanza darasa la kwanza wilayani humo lakini 6,482 tu walifanya mtihani wa darasa la saba mwaka 2013 hivyo kumaanisha kuwa, 3418 hawakumaliza shule.

Anasema pia kuwa, kati ya wanafunzi 3,100 walianza kidato cha kwanza katika wilaya hiyo, 1,251 tu walifanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2010, na akauliza, wanafunzi 1849 wamekwenda wapi. “Wamekwenda wapi, inaonekana hili jambo hili halina jawabu…jambo hili hatuwezi kuliacha liendelee na linaendelea kwa sababu viongozi sio makini…ni hodari wa kupeleka wanafunzi darasani lakini si kuhakikisha wanakuwa darasani,” anasema.

Rais ameagiza kuwa, kila baada ya miezi mitatu, walimu watoe taarifa ya mahudhurio ya wanafunzi na amewataka viongozi watimize wajibu wao katika jambo hilo. “Mkiwatafuta mapema watoto hawa watarudi, mmeshindwa kutimiza ipasavyo wajibu wenu wa uongozi,” anasema Rais Kikwete.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, Malengo ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ni kufikia kiwango cha ufaulu cha asilimia 80, lakini Ruvuma wapo kwenye asilimia 38, hivyo ametaka wajitahidi wafike angalau asilimia 60. Rais anasema, inasikitisha kuona kuwa, mikoa iliyo nyuma kimaendeleo ndiyo isiyotilia mkazo suala la elimu na kwamba, kwenye jambo hilo hataki ile dhana ya aliyenacho ataongezewa. Rais umenena, mwenye masikio na asikie.

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Basil Msongo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi