loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kikwete alivyotoka ‘peponi’ kwenda ‘mbinguni’

Mbwembwe za madereva wa bodaboda, shangwe, nderemo na vifijo kabla na baada ya kumpokea katika viwanja vya kituo kipya cha mabasi mjini Mbinga havikuashiria kwamba pale ni mbinguni na huenda kiongozi huyo wa nchi alishangaa aliposikia kuwa Mbinga ni mbinguni, Nyasa ni peponi.

Mamia ya wananchi wengi wao wakiwa wamevaa fulana, khanga, vitenge, kubeba bendera za Tanzania na Marekani, vikundi za zaidi ya 20 vya ngoma za asili, wanafunzi wengi wa shule za msingi na sekondari, na bendi ya muziki wa dansi vilimpa Rais Kikwete mapokezi aliyostahili.

Wakati Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga anawasalimu wananchi na kutamka’ Mbinga, na wakaitikia mbinguni, nilidhani nimesikia vibaya, lakini baadaye nilijiridhisha kwamba, nilichokisikia ndicho kilichotamkwa.

“Mbinguni hawaingii watu wasio na furaha bwana…mbinguni huingii ukiwa na sura kukasirika” anasema DC Ngaga wakati anawashawishi wananchi wachangamke, wafurahi wakati wanamsubiri Rais wao aende kuwasalimu na kukifungua kituo hicho cha mabasi cha kisasa.

Mbunge wa Mbinga Mashariki, Gaudence Kayombo, alirudia kutamka maneno hayo kuwa Mbinga ni mbinguni, na mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi, Kassim Mapili, akasema ‘Mbinga mbinguni oyee!’

Wakati yanatamkwa hayo, Rais Kikwete alikuwa hajafika kwenye eneo hilo, na hata alipowasili saa 5 asubuhi, kuburudishwa kwa ngoma za makabila mbalimbali, kuzunguka kuwasalimu wananchi na kucheza nao, bado alikuwa hafahamu kuwa kumbe alikuwa mbinguni!

Wananchi Mbinga wameonesha ukarimu mkubwa kwa Rais Kikwete, na Mzee Moris, kwa niaba yao, amemkabidhi kiongozi huyo hengo kwa ajili ya kufyekea bustani, na mkewe, Mama Salma amepewa kitenge.

“Na haya unayoyaona hapa yanathibitisha kama kumbe kweli hapa ni mbinguni,” anasema Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu. “Na kule tulipotoka ni peponi,” anasema. “Mheshimiwa Rais katika msafara wako huu na sisi tumebahatika kufika hapa Mbinga mbinguni, si rahisi kufika mbinguni ukiwa hai,” anasema Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.

Waziri Tibaijuka anasema, Mbinga ni mfano wa kuigwa katika masuala ya mipango miji na angependa eneo la kituo kipya cha mabasi mjini humo liwe town square yaani eneo mjini ambalo watu wanapumzika, na kukaa kuzungumza. “Lakini nikifika Dar es Salaam naenda kutoa agizo kila Halmashauri pawe na town square” anasema.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, kupanga miji ni kazi ngumu kama inayofanywa na figo katika mwili wa binadamu, kasisitiza utunzaji mazingira ili Mbinga uwe mji wa kitalii.

“Na mlipokaa kwa kweli Mwenyezi Mungu amewapa mahali pa pekee,” anasema Profesa Tibaijuka na kubainisha kwamba, katika wilaya hiyo hakuna migogoro mingi ya ardhi. “Akina mama mpo? Tunaweza hatuwezi?...wenyewe wa Mbinga wanaita Mbinga City,” anasema.

“Asanteni sana kwa mahudhurio yenu, tumefurahi sana, Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye,” anasema Mama Salma. “Nimekuja mara nyingi lakini leo mmetia fora” anasema Rais Kikwete. Wakati Rais Kikwete anaanza kuzungumza na wananchi saa nane mchana alisema “Wenzetu mna bahati, mna mbingu na pepo”.

Anawapongeza Mbinga kwa kuwa kahawa yao ni moja ya kahawa bora duniani. “Mwenye macho haambiwi tazama, mwenye masikio haambiwi sikia,” anasema baada ya kuwapongeza pia kwa kiwango cha maendeleo walichofikia. Licha ya kusema, Mbinga ni mbinguni, na Nyasa ni Peponi, Mwambungu, anamweleza Rais Kikwete kwamba, ukosefu wa barabara lilikuwa giza kubwa mkoani Ruvuma.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa mkoa, wakati fulani, mtoto wa ndugu yake alihamishiwa Tunduru, wanafamilia walikutana kujadili jambo hilo, na kwamba, walikaa utadhani kulikuwa na msiba.

Anasema, walifanya hivyo kutokana na mtazamo hasi waliokuwanao kutokana na ugumu wa mazingira ya huko wakati huo, lakini sasa wanaodhani kupelekwa Tunduru ni adhabu, wanakosea. Balozi wa China nchini, Lu You Qing, anasema, Songea ni mahali pazuri sana, kuna maliasili za kila aina, mandhari nzuri na watu wakarimu sana, na wana uwezo wa kupata ufumbuzi wa kila aina ya tatizo.

Amesifu sera ya Kilimo Kwanza kuwa imewawezesha wananchi wapate chakula cha kutosha na kubaki na ziada inayouzwa nje. Balozi Qing anatoa changamoto kwa wanaume wafanye kazi kwa bidii ili watoto wao waishi maisha mazuri. Kwa mujibu wa Balozi huyo, China imeweza kupata maendeleo makubwa kiuchumi kwa kuwa iliboresha miundombinu, na kwamba, ili upate maendeleo ya kweli lazima ujenge barabara.

“Chini ya uongozi wa Rais Kikwete sasa kuna barabara kwenda kila mahali,” anasema na kuongoza kuwa, miundombinu hiyo inarahisisha upelekaji mazao sokoni hivyo kuongeza vipato vya wananchi. “Na sasa wananchi tuna Rais mzuri sana, mawaziri wazuri sana, wakuu wa mikoa wazuri sana, na sasa tunapata maendeleo makubwa sana,” anasema.

Mbunge Kayombo anasema, mandhari ya Mbinga ni ya kipekee na kwamba wilaya hiyo imepiga hatua kubwa kimaendeleo. Anatoa mfano kwamba, hivi sasa kuna shule ya kufundisha kuongeza thamani ya madini yakiwemo Safaya, rubi na dhahabu. “Baada ya muda mfupi watu watatoka Chalinze na Dar es Salaam kuja kununua hapa Mbinga,” anasema Kayombo.

Ameshukuru Rais Kikwete kwa kutekeleza ahadi zake kwa wananchi wa Mbinga ikiwa ni pamoja na kufikisha umeme wilayani humo ulioanza kuwaka Septemba 6, 2007. “Na ndiyo inayosababisha Mbinga iwe mbinguni maana mbinguni hakuna giza,” anasema na kubainisha kwamba, sasa barabara si tatizo Mbinga.

“Hapa mambo ya barabara, umeme yalikuwa makubwa sana,” anasema Mbunge huyo na kuongeza kuwa, hivi sasa kata 15 katika Wilaya ya Mbinga yenye wakazi 354,000 zinapata umeme, ofisi ya Mkuu wa Wilaya inakaribia kumalizika kujengwa, Ikulu ndogo imejengwa.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimembariki Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea ...

foto
Mwandishi: Basil Msongo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi