loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kikwete ataka mafataki wasirubuni wanafunzi

Rais amesema kuna wanawake wengi wanaotafuta wanaume, hivyo kufanya ngono na mtoto wa kike ni tabia mbaya na si uhodari.

“Uhodari wa kuhonga pipi? Tafuta mzee mwenzako mzungumze mpishane maneno…kuna wanaume wa hovyo tu,” alisema Kikwete aliposimama kuzungumza na wananchi wa kijiji cha Utwango wakati akiwa njiani kwenda wilayani Namtumbo, kuendelea na ziara yake mkoani Ruvuma.

“Wanawake wapo wengi wanaotafuta wanaume, lakini unataka wanafunzi tu…uhodari huu, uhodari wa kuhonga pipi? Mtoto wa shule aachwe asome,” alisema Rais.

Alibainisha kuwa kuna tatizo kubwa la mimba kwa wanafunzi katika wilaya hiyo, linalosababisha watoto wafukuzwe shule. “Ndiyo maana mke wangu ana msemo hapa, mtoto wa mwenzio ni mwanao.”

Alisema hakuna tatizo la mimba kwa wanafunzi katika mkoa wa Kilimanjaro, ila limekithiri katika mikoa ya Kusini na ya Pwani.

Naye Mke wa Rais Kikwete, Mama Salma Kikwete alisema mjini Namtumbo kuwa watoto wa kike, wanastahili kupata fursa ya kupata elimu, badala ya kuozeshwa wakiwa wadogo.

Alisema hayo alipozungumza na wananchi wa Namtumbo kwenye mkutano wa hadhara baada ya Rais kufungua barabara ya Songea- Namtumbo, na kuweka jiwe la msingi barabara ya Namtumbo- Kilimasera- Matemanga.

“Wafungwe hawa, akifungwa mmoja hawatarudia wengine, huku mimba ni nyingi, ni nyingi kupita kiasi, ninyi wazee msiwape watoto mimba, mtoto wa mwenzio ni mwanao kama uliyemzaa, ninyi vijana msiwape watoto mimba, kwani dada yako hawezi kuwa mpenzi wako, ni mwiko, haiwezekani hata kidogo,” alisema Mama Salma.

Katika mkutano huo, Mama Salma alisema hakuna anayeweza kutibu Upungufu wa Kinga Mwilini (Ukimwi), hivyo wananchi wasidangayike.

“Kutoka asilimia tano nukta moja ya maambukizi, tunataka tufike asilimia ziro nukta ziro, na ziro nukta ziro ni Tanzania bila Ukimwi… Tanzania isiyokuwa na Ukimwi inawezekana,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu alisema janga la Ukimwi bado halina tiba. Alibainisha kuwa kasi ya kuenea kwa virusi vya Ukimwi (VVU) ni kubwa kwa sababu ya ‘nyumba ndogo’ na ‘michepuko’.

IKIWA fomu moja ya kuomba ridhaa ...

foto
Mwandishi: Basil Msongo, Namtumbo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi