loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kikwete kakukumbusha vaa kondomu

Hongera kwa starehe za hapa na pale, kula bata kwa kiasi, kumbuka kuweka akiba ya kesho, na usisahau kujilinda utimize ndoto zako.

Starehe zipo, ulizikuta na utaziacha, wewe si wa kwanza kustarehe na hautakuwa wa mwisho, na kila wakati kumbuka kwamba, Mungu hapendi tuangamie lakini pia hapati hasara tukifa.

Linah na Diamond wanasema mapenzi kizaizai, yananyima furaha, yanakosesha raha, yasikie kwa mwenzako omba yasikupate. Kwa kiasi kikubwa huwezi kutofautisha mapenzi na Ukimwi, na naamini nipo sahihi kusema, Upungufu wa Kinga Mwilini (Ukimwi) nao ni kizaizai, usikie kwa mwenzako, omba usikupate.

Ukimwi si ugonjwa lakini wenye Virusi vinavyosababisha Ukimwi(VVU) wanaumwa, hawana raha, hawana amani, wanateseka, ‘ngoma noma’.

Ingawa tunashawishiwa tuamini kwamba Ukimwi ni kama malaria ukweli unabaki palepale kwamba, ‘umeme’ a.k.a gridi ya taifa unatisha, ukitaka kuamini nenda kapime mapigo ya moyo ya anayesubiri majibu ya kipimo cha malaria, na yule wa vipimo vya VVU.

Sehemu kubwa ya maisha ya mwanadamu imetawaliwa na mapenzi, suala la kujamiiana lilikuwepo, lipo na litaendelea kuwepo , na huhitaji kuwa profesa ili kufahamu uhusiano wa mapenzi na Ukimwi na si lazima uwe mwanasayansi utambue kuwa VVU vimekaa sehemu mbaya.

Rais Jakaya Kikwete anafahamu undugu wa ngono na Ukimwi ndiyo maana kakukumbusha uvae kondom. Rais kasisitiza kondom kwa sababu si siri, jamii imehalalisha uzinzi na uasherati, kuchepuka ni jambo la kawaida kama kutafuta embe Kibada, kumtafuta mwaminifu kwa asilimia 100 ni sawa na kukuta chungwa kwenye michongoma.

Nampongeza Rais Kikwete kwa kuwa muwazi kwenye suala la matumizi ya kondom, sijawahi kumsikia kiongozi mkuu wa nchi anazungumzia kondom kama alivyozungumzia yeye, big up JK.

Nampongeza kwa sababu, hata asiposema, watu wanafanya ngono, hivyo jambo la msingi si kutosema, ila kuwaeleza wananchi madhara ya matendo yao endapo hawatajilinda, na JK kasema, hata mwanamke anapaswa kwenda na kondom kwenye eneo la tukio.

Si hivyo tu, Rais kasisitiza kondom kwa sababu, huwezi kumtambua kwa macho hivyo kutovaa kondom ni ‘kujilipua’, raha ya muda mfupi inaweza kukusababishia majuto kwako na wanaokuhusu.

Ni bora uvae viatu hata kama hujaona miiba kuliko kusubiri uchomwe ndipo ujilaumu kwa kutovaa viatu. Kikwete kasisitiza kondom wakati mwafaka kwenye zama hizi za kambi popote, kwenye kizazi cha ‘ukikataliwa una gundu’, wakati huu wa mapenzi kama siti ya daladala, ukiamka mwenzako anakaa. bmsongo@gmail.com.

Naamka asubuhi,  sioni kilongalonga, 
Napapasa kitandani,  hamadi hiki hapa,  

foto
Mwandishi: Basil Msongo

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi