loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kikwete: Rasilimali zikitumika ipasavyo, umasikini kwisha

Nilikuwa kwenye msafara wa Rais Jakaya Kikwete alipofanya ziara katika mkoa huo kuanzia Julai 17 mwaka huu, kote alipopita aliwaeleza wananchi namna wanavyoweza kuzitumia fursa zilizopo kujikomboa kiuchumi. Kwa mfano wakati akiwa Mbinga, Rais Kikwete alieleza namna wananchi wa Mbinga wanavyoweza kuzitumia barabara kufanya biashara ili kuongeza vipato vyao.

“Tumepata barabara ya lami sasa, si kama nyingine hazitajengwa, zitajengwa tu,” anasema Rais Kikwete kabla ya kufungua barabara ya lami ya Peramiho- Mbinga yenye kilomita 78. “Hatuna deni na mtu hapa kwa yale tuliyoyaahidi…barabara nyingi sasa zinapitika vizuri kwa sababu serikali ilifanya kazi kubwa kuongeza fedha kwenye mfuko wa barabara,” anasema Rais. “Kama hujitumi barabara hii haina faida kwako, kama hujitumi, miundombinu hii haina faida kwako,” anasema Rais Kikwete.

Si hivyo tu, katika mkutano huo Rais Kikwete anawaeleza wakulima kuwa, mikopo wanayopata ni kwa ajili ya kuongeza vipato vyao na si kumaliza shida walizonazo. Anawataka wazitumie kwa nidhamu fedha wanazokopeshwa badala ya kuzitumia kujengea nyumba, kusomesha watoto, kuburudika na vimada au kuoa wake wengine.

Anasema, wakulima wanapaswa kutumia mikopo kuboresha kilimo chao ili kuongeza vipato vyao kuinua hali zao za maisha badala ya wengine kuitumia kula raha na nyumba ndogo. Rais anayasema hayo wakati anakabidhi hundi kwa vyama vinne vya ushirika vya Kilimo na Masoko (AMCOs) vya Mahilo, Ngaka, Ngima na Pilikano vilivyokopeshwa shilingi milioni 500 kila kimoja ili kuboresha kilimo cha kahawa.

Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limewakopesha wakulima wa Mbinga jumla ya shilingi bilioni mbili. “Hii fedha ni kwa ajili ya kilimo cha kahawa, msisomeshee watoto mtashindwa kulipa deni, na usipolipa hizi si unajua mali inapotea… ni kwa ajili ya kahawa sio kumalizia nyumba, mkisomeshea watoto, mkimalizia nyumba mtashindwa kulipa deni?” anasema Rais Kikwete.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu NSSF, Chiku Matesa anasema, shirika hilo limetoa fedha hizo kupitia mipango maalumu kwa wakulima na wachimbaji wadogo kutokana na changamoto zinazowakabili.

“Changamoto hizo ni pamoja na kukosa uhakika wa huduma za afya, kutokuwa na uwezo wa kununua pembejeo ili kuongeza uzalishaji, kutokuwa na uhakika wa kipato baada ya kufikia umri wa uzee na kushindwa kuendelea na shughuli za kilimo,” anasema Matesa.

“NSSF inatambua kuwa kadri tunavyomkwamua mkulima kiuchumi tutakuwa tumefanikiwa kuikwamua jamii kubwa ya kitanzania kutokana na hali duni ya kimaisha na hatimaye kuongeza tija katika uzalishaji,” anasema. Sanjari na fedha wanazokopeshwa, Rais Kikwete anawataka wakulima na wananchi kwa ujumla kuzitumia barabara kuboresha maisha yao kwa kufanya biashara.

Wakati anazungumza na wananchi wa Mkenda na Songea Vijijini kwa ujumla, Rais anasema, barabara zote zinazoiunganisha Tanzania na nchi nyingine zitawekwa lami hivyo wananchi waitumie fursa hiyo kuongeza vipato vyao. Anatoa changamoto kwa wananchi wa Ruvuma kufanya biashara halali na Msumbiji na kwamba, kituo cha biashara katika mpaka na nchi hiyo kitajengwa.

Ameagiza viwanja vipimwe kwenye eneo la Mkenda lilipo soko la kisasa, na pia yatengwe maeneo kwa ajili ya viwanda. “Soko hilo hapo, kazi kwenu, fanyeni biashara” anasema Rais Kikwete. Wakati akiwa njiani kwenda wilayani Namtumbo, Rais Kikwete anazungumza na wananchi wa Kijiji cha Utwango, akawaeleza kuwa, soko la mahindi linaanza Agosti mosi mwaka huu.

“Soko la mahindi linaanza tarehe moja mwezi wa nane, hilo nalijua,” anasema Rais wakati anazungumza na wananchi wa Kijiji la Suluti wakati akiwa njiani kwenda mjini Namtumbo. Rais anasema mjini Tunduru kuwa, wananchi Ruvuma wana fursa kufuga vizuri hasa ng’ombe wa maziwa.

Amewaagiza viongozi wa mkoa huo wazungumze na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, waipitie vizuri programu ya ufugaji ng’ombe wa maziwa. “Ipo programu ya kopa ng’ombe lipa ng’ombe lakini sio programu ya serikali,” anasema. “Kuna vitu ambavyo sisi viongozi tukifikiria vizuri, tukijipanga vizuri tunaweza kuwasaidia wananchi wetu kuondokana na umasikini wa kipato,” anasema.

Wananchi wa Kijiji cha Utwango wanamweleza Rais Kikwete upungufu wa pembejeo, naye anawajibu “Pembejeo zipo zinashughulikiwa, si kila mwaka zinaletwa?” “Bei ya mbolea inategemea huko tunapoinunua, wakishusha na huku inashuka, wakiongeza na huku inaongezeka” anawaeleza wananchi wa Suluti.

Anawaagiza viongozi wa mkoa wa Ruvuma wasimamie vizuri suala la pembejeo, watafute jibu kwamba ni kwa nini zinachelewa kufika kwa wakulima.

“Si busara sana, kwa hiyo hilo nadhani mlitafutie jawabu” anasema mjini Tunduru wakati wa majumuisho ya ziara yake na kusisitiza kuwa suala hilo lisimamiwe vizuri, wakulima wapate pembejeo kabla ya msimu wa kilimo. Rais Kikwete amewaagiza viongozi wawahamasishe wakulima walime karanga kwa wingi kwa kuwa hakuna tatizo la soko na pia wapande miche mipya ya kahawa.

Rais pia anaagiza viongozi wa Ruvuma wahakikishe miche mipya ya kahawa inapatikana na wawahamasishe wakulima wabadili miche na amefurahi kuona uzuri wa shamba kubwa la kahawa lenye hekta 2,000 linalomilikiwa na kampuni ya Aviv lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea.

“Ni mara yangu ya kwanza kuona shamba kubwa la kahawa kama lile,” anasema Rais Kikwete na kubainisha kuwa, amevutiwa na utaratibu wa kampuni ya Aviv kuwapatia wakulima miche ya kahawa hivyo kwa sasa watafutwe maofisa kilimo wa kahawa ili kuboresha kilimo cha zao hilo. “Maana huyu aliyezoea mahindi, kahawa anaisoma shuleni tu,” anasema na kuagiza maofisa kilimo wawezeshwe kusimamia zao la kahawa na kuondoa kasumba kwamba, kahawa inalimwa Mbinga, na mahindi yanastawi Songea Vijijini.

“Kumbe hata Songea vijijini kahawa inastawi na inaweza kustawi” anasema na kuhamasisha mapinduzi katika kilimo ikiwa ni pamoja na wakulima kutumia zana za kisasa za kilimo. Rais anasema, sehemu kubwa ya mkoa wa Ruvuma inafaa kwa kilimo cha matrekta hivyo viongozi mkoani humo watengeneze mpango wa kupata matrekta.

“Sasa kwa mapinduzi haya ya kilimo lengo ni kuwaondoa wakulima kutoka kwenye jembe la mkono na kuwapeleka kwenye matrekta…hatuwezi kuendelea na kilimo hiki cha jembe la mkono, halmashauri ziongoze njia kwenye hili,” anasema na kuagiza kuwa halmashauri zikope matrekta, ziwakopeshe wakulima. “Tupunguze asilimia hii kubwa ya jembe la mkono, jembe la mkono unatumia nguvu nyingi kwenye eneo dogo,” anasema Rais Kikwete.

Anawataka viongozi mkoani Ruvuma kuhamasisha wananchi walime embe kisasa kwa kuwa hali ya hewa kwenye eneo hilo inaruhusu. Rais Kikwete anasema, wakulima wakipanda miche ya kisasa ya miembe wataweza kuuza embe hata Ulaya hivyo kupata fedha za kuwaondoa kwenye umasikini. Amewahimiza viongozi Ruvuma kuwasaidia wananchi walime matunda na mboga ili kuongeza vipato vyao kwa kuuza ndani na nje ya nchi.

“Hebu lipeni uzito unaostahili, ninyi hali ya hewa inaruhusu kabisa,” anasema na kuongeza kuwa, maembe mengine ni matamu lakini ladha yake haishindi ile ya embe dodo. “Huyu mnamuondolea umasikini wa kipato maana the biggest problem (tatizo kubwa zaidi) ni income poverty (umasikini wa kipato)…ni vitu vinavyowezekana, maana hatuzungumzi vitu vya ajabu sana,” anasema na kusisitiza umuhimu kwa wakulima kuwa na mazao tofauti ili kuongeza vipato vyao.

Anasema, katika maeneo mengi alipopita mkoani humo aliona machungwa ya njano, hivyo wanaweza kuyauza Ulaya kwa kuwa ndiyo yanayotakiwa huko.

“Hilo mlifikirie sana…ni zao ambalo mnaweza kabisa mkalitilia mkazo…lazima muwe wabunifu , muwe creative (wabunifu), lakini motive (nia) yenu kubwa lazima mfanye kitu” anasema. “Ni vitu vinavyowezekana lakini havifanyiki kwa dhati, ni vitu vinavyowezekana, ni vitu ambavyo tunaweza lakini havifanyiki… chochote kinachoweza kufanya watu wakapata mapato tufanye” anasema Rais Kikwete.

“Na hapa nataka ku-ephasise (kusisitiza) kitu kimoja tu, ufugaji wa samaki,” anasema na kubainisha kuwa yeye hachoki kujifunza mambo mapya. “Hebu tuvitazame, ni vitu ambavyo wanaweza kufanya watu…kwa hiyo jamani tutafute vitu vinavyoweza kuwasaidia watu wetu.”

Anawataka viongozi Ruvuma watafute uwezekano wa kujenga viwanda vya kusaga unga ili Ruvuma iuze unga badala ya mahindi. “Badala ya ninyi kuuza mahindi sasa muuze unga, badala ya kuuza mpunga muuze mchele.. mimi nadhani ni wazo zuri, kaeni mlitafakari kimkoa,” anasema na kueleza kuvutiwa na uwepo wa viwanda vinne vya kusaga unga katika jimbo la Peramiho.

“Jambo hili nimelikuta pale, kaeni mlitafakari vizuri, lazima muwe wabunifu,” anasema. Kwa mujibu wa Rais, viwanda hivyo vitaboresha maisha ya wakulima kwa kuunua mazao yao na kwamba kuna soko kubwa la unga kwa kuwa wananchi mijini hawahitaji mahindi, wanataka unga.

Amewaagiza viongozi katika mkoa huo kuwasaidia wananchi kuondokana na umasikini katika mazingira yaleyale wanapoishi na kwamba, hawatarajiwi kufanya mambo ya ajabu sana ili kufanikiwa katika hilo. “Ajira yetu ni shamba, ile ardhi yenyewe ndiyo mwajiri wake… maisha yaliyo bora hayadondoki kama mana, maisha yaliyo bora hayaji kwa kugawiwa pesa,” anasema Rais.

Wakati akiwa katika Kijiji cha Suluti anawaeleza wananchi wamweleze matatizo yao yote aone namna ya kuwasaidia. “Mimi hapa ndiyo mwisho, mkiipoteza fursa hii ndiyo hampati tena,” anasema na kuwaaga kwa kuwaambia “ asanteni sana, ninyi ni watu wazuri” Wakati akiwa njiani kwenda Namtumbo, Rais aliitumia sana kauli hiyo, kwa mfano, wakati anawaaga wananchi wa Kijiji cha Litola anasema “Jamani asanteni sana, ninyi watu wazuri”.

Kabla ya kuaga, anaahidi kutoa shilingi milioni nne kuchangia ujenzi wa hosteli ya wanafunzi wa shule ya sekondari, na yupo tayari kuchangia zaidi wakimuomba. “Ila muwahi maana mwaka ujao Oktoba mie ndiyo napumzika,” anasema Rais Kikwete. Rais Kikwete kaondoka Ruvuma akiwa amefurahi, wananchi na viongozi wa huko watimize wajibu wao, Tanzania yenye asali na maziwa inawezekana.

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Basil Msongo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi