loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

'Kila mmoja aseme hapana kwa ndoa za umri mdogo'

Wataalamu wanasema msichana anapoolewa katika umri mdogo humsababishia kuingia katika majukumu makubwa katika wakati ambao hajakomaa lakini mbaya zaidi ni kumkosesha fursa za kuendelea na masomo na kushindwa kujiingiza katika shughuli za kiuchumi kwa uwanda mpana zaidi.

Wengi hubaki kuwa tegemezi la waume zao. Takwimu zinaonesha kwamba zaidi ya asilimia 42 ya wasichana barani Afrika, Tanzania ikiwemo, wameolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 18.

Muda huu unaposoma makala haya, mamilioni ya wasichana barani Afrika wako katika hatari ya kuingia katika majukumu ya familia kabla ya kufikisha umri unaostahili wa utu uzima na kujitambua.

Kutokana na kuendelea kukithiri kwa tatizo la ndoa za utotoni, serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kiraia imezindua kampeni ya kitaifa kwa lengo la kupinga vitendo hivyo itakayoanzia mkoani Mara.

Mashirika yanayoshiriki katika kampeni hiyo ni pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, (UN-Women), Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Taasisi ya Graca Machel Trust (GMT), pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA).

Licha ya kwamba tatizo la ndoa za umri mdogo ni tatizo la kidunia linalokwaza utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa milenia katika kupunguza umaskini, kuwa na usawa wa jinsia, afya bora kwa watoto, uzazi salama na kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi, utashi wa kisasi ni muhimu katika kuweka mazingira yatakayohakikisha yanalimaliza.

Malengo ya kukua kwa uchumi wa Tanzania yanaelezwa kwamba yanategemea kuwekeza katika programu zenye kuwainua wasichana na wanawake kwa kuwa na afya nzuri na salama, wawe na elimu bora na kulindwa na ukatili wa kijinsia pamoja na ndoa za umri mdogo.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo, Graca Machel, amewataka wananchi kutokubali mchakato wa Katiba Mpya kumalizika bila kuweka wazi umri sahihi wa mtoto wa kike kuolewa.

Graca, ambaye ni mjane wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, anasema kwa kufanya hivyo itasaidia kupunguza ama kumaliza kabisa vitendo vya ndoa za umri mdogo zilizoshamiri nchini.

Pamoja na kuzindua mfumo wa ujumbe mfupi wa simu za mikononi kwa mkoa wa Mara kwa ajili ya kutoa taarifa za waathirika wa suala hilo, Graca, mwanzilishi wa Taasisi ya Graca Machel Trust (GMT) anasema:

"Tuwaoneshe wabunge kuwa hakuna kutoa sababu katika Katiba haswa inapofikia wakati wa kuikubali kwa kura ya maoni.”

Anasema, bila shaka ndani ya Bunge Maalumu kuna wenye kujali mila na tamaduni zao na wengine wasiotaka kabisa mabadiliko na hata kuwa wabishi. Hivyo anasema ni vyema ikafahamika kuwa mila na tamaduni zipo na zinaweza kubadilika hasa pale zinapoleta madhara kwa watoto, familia na hata taifa kwa ujumla.

Anasema ingawaje kwa wengine sio rahisi kubadili mila na tamaduni zao harakaharaka, jamii haiwezi kuendelea kuishi katika hali hii na hivyo ni lazima sasa kuwepo na msukumo mpya utakaohakikisha ndoa za utotoni zinakoma.

Kuhusu mjadala kuwa umasikini ndio chanzo cha ndoa za utotoni, Graca anasema hilo ni suala la kuchunguzwa zaidi kwani katika nchi nyingi za Afrika zina familia masikini lakini zenye kuishi kwa upendo na kujaliana.

“Itafutwe njia mbadala ya kupambana na vitendo hivyo ili familia ziweze kuishi vizuri kwani pindi familia inapopokea mahari ya mifugo kwa sababu ya umaskini, baada ya hapo hakuna utajiri unaoonekana kwa familia hiyo badala yake binti huenda kuanza maisha akiwa mtoto," anasema Graca.

Anasema kwamba ipo haja ya kubadili mtazamo katika jamii ili mtoto wa kike awe na thamani kama alivyo wa kiume katika ngazi ya familia na kwamba watoto wa kike wapewe mamlaka ya kujitambua na kutoa maamuzi tangu wakiwa wadogo.

Kuhusu wazazi anaitaka serikali kutoa ujumbe sahihi kwao ili kufahamu kwamba maamuzi wanayoyatoa dhidi ya ndoa za utotoni kuwa ni batili na sasa wabadili mtazamo.

Kwa upande wa vijana anasema ni eneo ambalo linatakiwa kuhamasishwa na kuelimishwa kwa kina ili kufahamu madhara ya kuwa wazazi kabla ya kufikisha umri unaopaswa kwa majukumu hayo.

Vijana ni kundi ambalo pia anataka lijue madhara ya kuwa mama ama hata baba katika umri mdogo na kuhakikisha wanabadili mitazamo walio nayo.

Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, anasema katika kuzindua kampeni hiyo itakayoanzia mkoani Mara kila mwenye kumiliki simu atatumiwa ujumbe utakaomtaka kutoa taarifa za kuwepo kwa ndoa za utotoni mahala ili vyombo vya kisheria vichukue hatua.

Anasema ndoa za utotoni ni kitendo kisichokubalika na hivyo anataka watoto waachwe wasome na hatimaye waweze kuwa na maamuzi yao wenyewe baada ya kujitambua na sio kulazimishwa kwa njia yoyote ile.

Licha ya kwamba kampeni hiyo itaanzia Mara lakini pia itatekelezwa nchi nzima ikianzia mikoa ile ambayo ina kiwango kikubwa cha ndoa za utotoni, ikiwa ni pamoja na Shinyanga, Dodoma, Tabora na Lindi. Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, anawataka wasichana popote walipo kuendelea kudai haki zao kwa nguvu na asiwepo atakayetoa sababu katika kuhakikisha haki hizo zinapatikana na hata kutekelezwa.

Jambo la muhimu linalotakiwa kila mmoja kutambua anasema ni vijana wa kike kustahili kupatiwa haki zao za msingi, hususan elimu na kwamba waachwe hadi watakapoamua wenyewe juu ya kuanza maisha hayo ama la.

Mwakilishi mkazi wa UNFPA, Dk Natalia Kanem, anasema Tanzania inahitaji kupunguza kiwango cha ndoa za utotoni na kuhakikisha kuwa malengo ya maendeleo ya milenia yanafikiwa kwa wakati stahiki.

Inaelezwa kwamba haiwezekani kumaliza tatizo la ndoa hizo kwa mtu mmoja na hivyo ni suala linalohitaji ushirikiano katika maeneo husika pamoja na kuelimisha jamii.

Elimu inayopaswa kutolewa kwa jamii ni kuhusu jinsia, afya na haki kwa kila mmoja na kwamba inapaswa kuwashirikisha wasichana na wavulana, familia, jamii, viongozi wa dini na viongozi wa mila, viongozi wa serikali, wabunge, asasi mbalimbali na wengineo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Valerie Msoka, anasema lengo la kampeni hiyo ni kuipa jamii uelewa katika kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa kwani havina manufaa yoyote kwa jamii zaidi ya kuwaongezea matatizo wasichana.

“WANAOFANYA shughuli za maendeleo katika vyanzo vinavyotiririsha maji ...

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi