loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kilimo cha asali kinavyoweza kuinua maisha ya vijana nchini

Kati ya hizo, Ethiopia ndio inayoongoza kwa uzalishaji ikifuatiwa na Tanzania. Takwimu zinaonesha kuwa tani 400,000 za asali huingia katika soko la dunia, hata hivyo mauzo yanayofanywa na Tanzania ni kidogo licha ya ubora wa asali yake kukubalika katika soko hilo, baada ya Nchi za Umoja wa Ulaya kuridhia.

Mwaka jana, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Asali nchini, alisema Tanzania inakadiriwa kuwa na makundi ya nyuki milioni 9.2, yenye uwezo wa kuzalisha asali tani 138,000 na tani 9,200 za nta kwa mwaka. Kwa wakati huo pia Tanzania ilikuwa inazalisha wastani wa tani 8,153 za asali na wastani wa tani 578.78 za nta kwa mwaka.

Hata hivyo anasema ni kiasi cha asilimia 4.5 tu ya asali ndicho kinachouzwa nje na kilichobaki kinatumika nchini, huku asilimia 66 ya nta ikiuzwa nje ya nchi. Kiwango hicho alisema ni sawa na kutumia asilimia 6.7 ya fursa za asali zilizopo na asilimia 6.5 ya fursa za nta zilizopo.

Licha ya kasoro hiyo ya kutotumia vizuri fursa zilizopo, sekta ya nyuki bado ina mchango wa ajira nchini kwa wale walioziona na kuzitambua. Faraji Shemsanga, mhitimu wa Shahada ya Kwanza Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA), ni miongoni mwa vijana waliotumia fursa ya asali kujiajiri na kujiongezea kipato bila kujali umri na elimu yake.

Anachokifanya ni kununua asali kutoka kwa wakulima wa zao hilo na kuiuza katika harakati za kujipatia kipato. Wakati akiendelea kununua bidhaa hiyo kutoka kwa wakulima mkoani Tabora, Shemsanga anatarajia kuanza ufugaji wa nyuki wa kisasa katika kulenga mazao mengi zaidi.

Anasema wazo la kuanzisha biashara hiyo lilikuja baada ya kuona sekta ya nyuki ina fursa nyingi kwa soko la ndani na nje ya nchi. Anasema kwa mara ya kwanza alianzisha biashara ya uuzaji wa asali mwaka 2012 akiwa muajiriwa katika Kampuni ya tumbaku mkoani Morogoro na mtaji wa biashara hiyo ulitokana na sehemu ya mshahara wake wa kila mwezi.

Licha ya fursa nyingi alizokuwa akiziona, pia msukumo wa kujiingiza katika biashara ya asali uliongezwa na nia yake ya kujitegemea kiuchumi na kujitawala mwenyewe katika shughuli zinazomuingizia kipato. Anasema watu wengi bado hawana elimu ya kutosha kuhusu faida zitokanazo na bidhaa ya asali.

Hii inasababisha idadi ya watumiaji wa asali kuwa ndogo au kupungua kadri siku zinavyosogea na hivyo kuifanya biashara hiyo isiwe na wateja kadri inavyofikiriwa. “Asali ni bidhaa ambayo inaweza kubadilisha maisha yako kwa maana ya kukuongezea kipato. Lakini pia ni bidhaa ambayo inaweza kuboresha afya yako kwa kutibu baadhi ya magonjwa,” anasema Shemsanga.

“Kwa jinsi ninavyoona soko la asali lipo, lakini kwa sasa linategemea eneo ulilopo watu wanafahamu nini kuhusu asali, je wanajua kama asali inaweza kuimarisha afya zao,” anasema. Mikoa inayozalisha asali kwa wingi nchini ni pamoja na Tabora, Kigoma, Katavi, Rukwa, Singida na Kagera.

Anasema asali anayouza ananunua kutoka kwa wakulima mkoani Tabora na kuisafirisha kwa njia ya barabara kwa kutumia magari ya mizigo hadi mkoani Morogoro anakoishi. Anasema kazi ya ufungashaji wa bidhaa kama asali inahitaji usafi wa hali ya juu ili kutunza afya za watumiaji hivyo ametenga sehemu maalumu kwa ajili ya kuweka vifaa na malighafi zote.

Shemsanga amesema biashara yoyote lazima iwe na upinzani kutoka kwa wafanyabiashara wengine na hivyo inamlazimu kutumia ubunifu wa hali ya juu ili kuendana na ushindani wa kibiashara. Anasema pamoja na kuzingatia usafi na ubunifu, wakati wa ufungashaji pia anatumia mitandao ya kijamii ambayo kwa sasa inaonekana kutumiwa na watu wengi wakiwemo wafanyabiashara kuhamasisha umuhimu wa asali kupitia nembo yake ya Honey Spring.

Unapoanzisha wazo la biashara ni muhimu kufahamu wateja wako, Shemsanga anasema alitambua wateja wake mapema kuwa ni wafanyakazi walioko katika ofisi mbalimbali ambao wanaweza kutumia asali wakati wa kufungua kinywa kwa kupaka kwenye mkate au kuweka kwenye maziwa ili kuongeza nguvu mwilini.

Pia mfanyakazi huyo huyo anaweza kuitumia bidhaa hiyo nyumbani. Kundi lingine alilolenga na ambalo pia ni sehemu ya wateja wake ni wafanyabiashara wa vyakula hivyo anamudu kufanya biashara ya jumla na rejareja. Anasema wateja wengi wapo katika mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro ingawa analenga kufikia mikoa mingine zaidi nchini.

Anasema maonesho ya wakulima Nanenane ni sehemu iliyomkutanisha na wakulima wengine wenye bidhaa kama zake na hivyo amepata fursa ya kuongeza ujuzi na kupata maarifa kuhusu biashara. Kwa mara ya kwanza alishiriki maonesho hayo mwaka jana akiwa ndani ya banda la Chuo cha Kilimo, SUA.

Mwaka huu, anatarajia kushiriki na kutoa elimu zaidi kuhusu asali. Anasema ataelimisha kuhusu tofauti iliyopo kati ya asali ya nyuki wakubwa na wadogo, jinsi ya kupima asali halisi kwa njia ya kitaalamu na njia ya kienyeji unayoweza kutumika hata nyumbani. Elimu nyingine anayolenga kuitoa ni kuonesha na kuitambua asali iliyoganda na sababu zinazochangia kugandisha asali, pamoja na jinsi ya kutumia asali kutibu magonjwa mbalimbali.

Changamoto ni sehemu ya maisha kwa mfanyabishara yeyote aliyeamua kutimiza malengo yake. Kwa upande wake anasema upatikanaji wa asali yenye ubora ni kazi kubwa kwa sababu asali nyingi ‘inachakachuliwa’. Na ili usiuziwe asali isiyo na ubora ni muhimu kuwa na ufahamu wa ziada kuhusu bidhaa hiyo.

Anataja changamoto nyingine ni upatikanaji wa vifungashio vya bidhaa. Anasema vifungashio ilivyopo kwa sasa vinapatikana kwa tabu na bei ya juu. Hivyo amezitaka mamlaka husika kufanyia kazi kilio hiki cha muda mrefu.

“Katika biashara hii pamoja na changamoto nilizozitaja, pia nimegundua kuna tatizo la wafanyabiashara wasio waaminifu wanaochakachua asali na matokeo yake wanavunja uaminifu kati ya wafanyabiashara wengine na wateja. Hili ni tatizo kubwa sana,” anasema Shemsanga.

“Tatizo lingine ni wateja kukosa elimu kuhusu asali, watu wengi hatufahamu uzuri na faida ya asali katika maisha yetu ya kila siku. Mimi kama mdau wa asali najitahidi kutoa elimu,” anasema. Kuhusu mafanikio anasema, mpaka sasa ameweza kujiajiri, kufungua duka la asali mkoani Morogoro na zaidi ya yote amejenga kiwanda kidogo cha kuchakata asali.

Ujenzi wa kiwanda hicho kidogo umetokana na faida anayoipata kwenye biashara bila kuchukua mkopo kutoka kwenye taasisi yoyote ya kifedha. Kwa sasa analenga kutumia fursa mbalimbali za maonesho ya bidhaa yakiwemo maonesho ya Nanenane yanayofanyika kila mwaka, ili kuongeza soko la biashara pamoja na kubadilishana mawazo na wafugaji wa nyuki, wataalamu wa mazao ya nyuki na wafanyabiashara kutoka katika mikoa mingine.

Vijana wengi wana hofu ya kuthubutu kujiajiri kwa kuhisi wanaweza kupoteza muda wao na fedha kwa ajili ya mtaji na wakati mwingine kwa sababu ya kutaka mafanikio ya harakaharaka.

Hali hii ni tofauti kwa Faraji Shemsanga anayewashauri vijana wenzake kuwa “Ushauri wangu kwa vijana wenzangu ni kwamba waanze biashara taratibu huku wakiendelea kuisoma vizuri biashara watakayoamua kuifanya, wasiwe na haraka kwa sababu hakuna mafaniko ya haraka.”

Anasema unapoamua kuingia kwenye biashara lazima uwe na nidhamu ya fedha kwa kutofautisha matumizi binafsi na matumizi ya biashara. Hali kadhalika mfanyabiashara anatakiwa kujua hesabu za biashara yake yakiwemo mapato na matumizi.

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Kiyao Hoza

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi