loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kilimo cha pamba kinavyozidi kushuka ubora, wingi

Kilimo cha pamba kinavyozidi kushuka ubora, wingi

Hata hivyo, zao la pamba linaendelea kutoa ajira kwa wananchi wengi wa mikoa 13 inayolilima ambapo kati ya mwaka 2005 na 2009 lilikuwa ni zao linaloongoza kwa kuliingizia taifa fedha za kigeni likifuatiwa na tumbaku, kwa sasa tumbaku ndio inayoongoza. Wakulima wengi wanasema wanalima tu kimazoea kwa sababu hawanufaiki vya kutosha huku wakiwanyooshea kidole wajanja wachache kwamba ndio wanaofaidi jasho lao.

Wanashindwa pia kujinyooshea kidole kwamba wanaharibu ubora wa pamba ya Tanzania kwenye soko la dunia kwa kuongeza mchanga na maji ili kupata kilo zaidi. Ujanja kwenye mauzo ya pamba unaelezwa kuwa na sura mpya kila kukicha. Wakulima wamedai kukumbana na mizani ‘zilizochakachuliwa’ kwa maana ya kupunjwa kilo huku pia wakitaja changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na upewaji wa mbegu zisizoota na dawa feki.

Haya yote wakulima wanadai yanawafanya kuingia katika gharama mara mbili katika jitihada za kuhakikisha nguvu walizotupa katika kilimo hicho hazipotei bure.

Jimmy Luhende, mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuangalia utawala bora, uwajibikaji na kilimo (ADLG) anasema amekuwa akifanya kazi na wakulima 30, ikiwemo walimu katika vijiji vya Nkoma, Kinaweli, Budalabujiga, Mahembe, Kabale Sunzula, Sawida, Gaswa, Mwalushu, Saningu na Ng’esha vilivyopo wilaya za Itilima na Bariadi mkoani Simiyu.

Luhende anasema kuwa pamba inayotoka shambani ni safi, inavunwa kwa kutumia mkono lakini changamoto kubwa zinazowakabili wakulima ni gharama za uzalishaji kuwa juu huku kipato kikiwa chini. Anasema wastani wa kilo moja anayouza mkulima ni Sh 700 hadi 750 wakati gharama za kuzalisha kilo hiyo zinaweza kuwa kubwa wakati mwingine.

“Dawa ya kupulizia wadudu kwenye pamba ni hafifu katika utendaji wake na inauzwa bila stakabadhi wala sehemu aliyonunulia mkulima haijui. Hii ni kwa sababu zinatembezwa majumbani, hivyo wanashindwa kuwabaini wauzaji ili wawarejeshee fedha pale dawa hiyo inaposhindwa kufanya kazi,” anasema Luhende.

Kadhalika anasema vijiji vingi vinapunjwa na halmashauri kwani havijui kwamba asilimia 10 ya fedha zinazoingia kwenye halmashauri kutoka kijiji fulani zinapaswa kubaki kijijini hapo. Anatoa mfano wa kijiji cha Nkomo ambacho akaunti yao ya kijiji ilipata Sh laki mbili pekee wakati uchunguzi wake unaonesha kwamba kijiji kilipaswa kupata Sh laki tatu.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Bariadi, Bahati Magamula anasema kumekuwepo na changamoto nyingi kwenye zao la pamba hususan katika mkoa wa Simiyu ambao ni moja ya mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa zao hilo nchini, lakini jibu la kudumu la changamoto hizo limeshindwa kupatikana licha ya kila mwaka watu kukaa ili kuzipatia majibu.

Uzalishaji kushuka

Mkulima wa kijiji cha Zanzui, Japhet Mabilika anasema alilima ekari mbili za pamba huku shamba hilo akikodi kwa gharama ya shilingi 60,000. Gharama za kulimiwa anasema zilikuwa shilingi 40,000 ambapo alipanda mbegu za Quiton lakini hazikuota. Akaamua kuingia tena hasara ya kuondoa majani yaliyochipua kwa shilingi 15,000 na kisha akanunua madebe mawili ya mbegu kwa shilingi 10,000.

Hiyo mbegu aliyonunua mara ya pili anasema ilichipuka vizuri. Kisha anasema alinunua dawa ya kuua wadudu chupa 10 lakini wadudu hawakufa. Akalazimika kuingia gharama nyingine ya kununua dawa tofauti.

“Hasara niliyoipata ni kuingia gharama ya kusafisha shamba mara mbili, kupanda mbegu ya pamba mara mbili, kununua chupa kumi za kuua wadudu wanaokula matunda ya pamba zilizokuwa feki na kulazimika kununua zingine. Tathimini iliyopo naweza kuvuna kilo 89 za pamba katika mafurushi matatu nitakayoyapata lakini bado itakuwa ni hasara kama nililinganisha na miaka iliyopita,” anasema Mabilika.

Yeye anashauri kwamba serikali irejesha mfumo wa zamani wa kuchukua pembejeo kwa mkopo kisha mkulima akishauza pamba yake anarejesha gharama. Anasema mfumo wa sasa unasababisha vikundi vilivyoundwa kwa ajili hiyo kuwaletea wakulima pembejeo feki. Mkulima wa kijiji hicho, Magina Sayi anasema kuwa alijiunga na kikundi cha kilimo cha mkataba lakini mbegu alizotumia hazikuchipua kwenye baadhi ya maeneo.

Hata katika maeneo ambayo mbegu hizo zilionekana kuchipua mashina yake marefu yalikuwa na tunda moja lenye mbegu mbili au tatu pekee wakati kiwango kinachotakiwa kwa mujibu wa wataalamu ni tunda moja kuwa na mbegu 10 hadi 12. Diwani wa kata ya Mhanwo wilayani Bariadi, Martine Singibala anasema kuwa mfumo wa kilimo cha pamba bado si rafiki wa mkulima.

“Kwanza dawa huja kwa kuchelewa na wengine hawapulizii kabisa. Wakati mwingine huletewa chupa tatu ambazo hazitoshelezi. Kimsingi mkulima huanza kulima mwezi Novemba lakini huletewa pembejeo mwezi Machi na wakati huu huwa wamechelewa sana,” anasema.

Kilimo cha mkataba hakina lolote

Kuhusu kilimo cha mkataba, Diwani Singibala anasema,“Kilimo cha mkataba kilikuwa kizuri kukisikia kwenye maelezo na sio utekelezaji wake kwani waliokuwa wakikihamasisha walikuwa hawaelezi bei, na mbaya zaidi dawa zilizokuwa zikiletwa ni feki au zimekwisha muda wa matumizi. Kwa hiyo unaweza kuona kama uzalishaji wa pamba unaporomoka.”

Ernest Mwanai, diwani wa kata ya Mwanushi wilaya ya Itilima ambaye pia ni mkulima wa zao hilo anasema ulimaji wa zao la pamba umekuwa sawa na utumwa kwani ukikodisha ekari moja kwa Sh laki moja, kulima shilingi 60,000, palizi shilingi 20,000 pamoja na gharama za mbegu na dawa, mwisho wa siku mavuno yake hayafikii gharama ulizotumia.

Kadhalika anasema wakati mwingine pembejeo zinazoletwa zinakuwa chache. Anatoa mfano kwamba kijiji kinaweza kuletewa magunia 28 ya mbegu wakati kijiji kina vitongoji vinne na kaya zaidi ya 5,000 zinazolima pamba.

“Hapo utasikia wanajigamba kwamba wameleta pembejeo wakati hazitoshi kutokana na idadi ya wakulima. Ndio maana kilimo cha zao la pamba kinashuka na kitaendelea kushuka kila mwaka kwani ni kama kinakosa mtetezi. Hata hiyo Bodi ya Pamba, kwa mtazamo wangu sioni umuhimu wake hata kama ingefutwa wakulima hatuna cha kupoteza,” anadai.

Diwani wa kata ya Nyangokolwa wilayani Itilima mkoani Simiyu, Charles Nkenyenge anasema anapokwenda kuuza pamba hukatwa shilingi moja kwa kilo ambapo fedha hizo zinadaiwa kwenda kuboresha mfuko wa pamba kwa maana ya Bodi ya Pamba lakini mchango wa fedha hizo za mkulima yeye anasema hauoni.

Anasema ukulima wa pamba unashushwa na mambo mengi ikiwa ni pamoja na kodi nyingi anazolipia mkulima huku gharama za pembejeo na gharama nyingine za uzalishaji kama kulimiwa shamba zikimsubiri.

Hakuna uadilifu

Diwani wa kata ya Bariadi mjini, David Sendo, anasema kuwa uadilifu ni jambo ambalo limekosekana kwa wengi na ni tatizo kubwa nchini kwani linachangia sana kudidimiza kilimo cha pamba.

Anatoa mfano kwamba utakuta wafanyabiashara wanafanyiana hujuma na kwamba mbegu ya Quiton ilielezwa kuwa ukikosea masharti ya kuipanda haioti na kwamba kuna wengine walitumia fursa hiyo kuiharibu kwa kuikaanga. “Haya mambo ya kuchakachua mzani, kukaanga mbegu, kuweka mchanga, maji ama chumvi ili kuongeza kilo ni suala la jamii kukosa maadili na uaminifu,” anasema.

Zipo tuhuma kwamba katika hali ya kuharibiana soko la mbegu baadhi ya watu walikuwa wakikaanga mbegu za pamba ili kuonekana hazifai na mwisho wa siku wapate kuuza za kwao. Mtafiti wa kujitegemea wa zao la pamba, Geofrey Sayi anasema zao hilo lilishuka kuanzia mwaka 2005 hadi 2009 ambapo lilianza kuimarika kiasi.

Anasema miaka ya nyuma lilikuwa zao la kwanza kuliingizia taifa kipato, lakini hali ya uzalishaji imeendelea kushuka mwaka hadi mwaka ambapo, kwa mfano anasema mwaka 2012/13 zilizalishwa tani 351,151 za pamba kwa mikoa 13 inayolima zao hilo lakini mwaka 2013/14 uzalishaji ni tani 246,767.

Anasema kwamba mwakani huenda likazidi kushuka kutokana na wakulima kusumbuliwa na changamoto kubwa ya bei ya pembejeo na mbegu kutoota vizuri huku baadhi ya wanunuzi wa zao hilo wakijitoa mapema kutokana na bei yake kwenye soko la dunia kuporomoka.

Meneja wa chama kikuu cha ushirika mkoani Shinyanga (Shirecu), Joseph Mihangwa, anasema malalamiko ya utumiaji mbegu ya pamba iliyotangazwa kwa wakulima wa zao hilo katika maeneo tofautitofauti imekuwa ni kero na anasema tatizo ni wahusika kutofanya majaribio kwanza ya mbegu hizo kabla ya kuzitangaza kwa wakulima kuzitumia.

Anasema huenda zao la pamba kwa mwaka huu likapungua zaidi kwa sababu mbegu zimeonekana kutoota huku bei ya pamba ikiwa ileile na huku baadhi ya wanunuzi wa zao hilo wakijitoa mapema baada ya kuona bei ya soko la dunia ikiwa mbaya. Mbegu kushindwa kuota “Sisi chama kikuu cha ushirika ni wanunuzi wa pamba na tayari kwa mwaka jana tulinunua kilo milioni nane.

Lakini kitu kilichojitokeza sasa ni baadhi ya wanunuzi kujiondoa mapema kwa kutokubaliana na bei iliyopo kwenye soko la dunia. Wanahisi wanapata hasara. Tatizo lingine ni mbegu kutoota vizuri baada ya wakulima kutumia pesa nyingi kuzinunua. Hizi huenda zikawa sababu za kushuka kwa uzalishaji wa pamba mwaka huu,” anasema Mihangwa.

Taarifa zinaonesha kuwa wakulima wa zao la pamba zaidi ya 14,000 nchini wamepata hasara baada ya kupanda ekari 50,000 kwa kutumia mbegu zisizo na manyoya za Quiton na kushindwa kuota.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, katika mikoa sita na wilaya 23, ambapo ekari 50,000 zilipandwa mbegu hiyo ya Quiton UK 91 na UK 08 bila kuota, zilikuwa tayari zimefanyiwa utafiti katika chuo cha Ukiriguru cha jijini Mwanza na kuonekana zinafaa na kuelezwa kwamba zina ubora mkubwa utakaosaidia kuongeza uzalishaji.

Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya pembejeo za mbegu bora na mbolea kwa wakulima nchini kwa utaratibu wa vocha ambapo mwaka 2008/2009 kaya 737,000 zilipata, mwaka 2009/2010 kaya 1,500,000, 2010/2011 kaya 2,011,000, 2011/2012 kaya 1,780,000 na mwaka 2012/2013 kaya zilizopata ni 940,783.

Pamoja na mafanikio mazuri ya mpango wa ruzuku, kumekuwepo na changamoto katika ngazi mbali mbali ikiwemo ubadhilifu, upotevu wa vocha na ucheleweshaji wa vocha, hali ambayo imekuwa ikisababisha wakulima kushindwa kupata pembejeo wakati mwafaka.

Wizara kupitia Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu (TOSCI) imeanzisha kudhibiti ubora wa mbegu za viazi mviringo, mihogo na kuendeleza udhibiti wa mbegu ya pamba ambapo uzalishaji wa aina ya UKM 08 iliyopitishwa rasmi unaendelea.

Ubora wa pamba ya Tanzania

Diwani wa kata ya Bariadi, David Sendo, anasema kitu muhimu ambacho serikali na wadau wanapaswa kufanya ni kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora. Anasema ni muhimu kumuandaa mkulima ili kuhakikisha anapata mbegu bora huku pia tukijiuliza pamba inayolimwa nchi zingine ina ubora gani na nini kinaifanya iwe bora kuliko ya hapa nyumbani, hali inayosababisha bei yake kupanda na kushuka?

Anasema zamani kulikuwa kunatengwa pamba fifi na pamba safi (bora) hali iliyokuwa inafanya ushindani kwa wakulima kuiweka pamba yao katika madaraja. Lakini siku hizi wakulima wanafikia kuweka mchanga na kuifanya pamba kukosa ubora, na hii inaonesha kwamba hawana elimu ya ubaya wa kuharibu pamba yao katika soko la dunia kwa kuwa wanafikiria alimradi kuuza pamba kwa kilo nyinghi wapate pesa.

Akizungumzia ubora wa pamba yetu, mkulima Difficuit Mahella anasema sababu nyingine inayofanya pamba yetu kuonekana chafu na kukosa ubora kwenye soko la dunia ni uvunaji wake wa kutumia mikono kwani nchi nyingine wanavuna kwa mashine.

Pia mkulima wa kijiji cha Sawida wilayani Bariadi anaona kwamba ili kupata pamba bora ungekuwepo utaratubu wa ushindani ambapo anayeuza pamba bora zaidi analipwa bei kubwa zaidi. “Hapo kila mkulima atajitahidi kuhakikisha analima na kuvuna pamba bora, siyo hali ya sasa anacholima anaona hakuna faida ya maana iwe bora ama kinyume chake,” anasema.

Mtafiti wa zao la pamba, Geofrey Chambua anasema kuwa ni swali la kujiuliza ni nani anaweka mchanga au kumtuma mkulima aweke wakati kwa majirani zetu, Kenya, pamba yao haiko juu kwenye ubora lakini wana soko la uhakika. Anasema zipo tuhuma kwamba, katika kujiongozea faida, mkulima anaweka mchanga ama maji ili apate kilo nyingi na baadhi ya wahasibu wasio waaminifu nao wanaongeza sukari au chumvi.

“Katika mazingira hayo wanaharibu soko zima la pamba ya Tanzania ambayo ilikuwa ikipendwa sana huko miaka ya nyuma,” anasema. Mdau wa zao la pamba, Moses Msosoma anasema mpaka sasa kilimo cha pamba kinalimwa sio kibiashara zaidi bali kwa ajili ya kujikimu kwa kupata fedha kidogo ya kulipa ada za shule, chakula na mahitaji madogo na ndio maana wengi hawaoni umuhimu wa kuboresha ubora wa pamba yao.

Katibu wa mtandao wa wakulima wadogo nchini (Mviwata) wilaya ya Bariadi, Zabron Sayi, anasema kuwa tatizo lililopo ni kuwepo kwa soko huria ambao wanunuzi wamekuwa wakipanga bei bila kushirikisha wakulima na kuangalia ni gharama ngapi walizotumia na kiasi gani wanastahili kupata baada ya kuvuna.

Wengine wanaamini kwamba namna ya kunyanyua ubora wa pamba na kunyanyua bei kwa mkulima ni kuimarisha zaidi viwanda vya ndani vinavyohitaji malighafi hiyo, husuan viwanda vya nguo na nyuzi.

Uchakachuaji wa mizani

Suzana Ncheye, mkulima kutoka kijiji cha Buzinza, anasema siku moja alipokwenda kupima pamba yake katika mizani tofauti ili kuona kama kuna uchakachuaji matokeo yalikuwa kama ifuatavyo; mzani wa kwanza ulionesha ana kilo 67, mwingine kilo 61 wa mwisho ukaonesha kilo 87 katika mzigo ule ule wa pamba na mpaka sasa hajui zilikuwa kilo ngapi hasa.

Diwani Ernest Mwanai anasema kuwa ukienda na tela moja la pamba kupima unapata vifurushi pungufu ya kumi tofauti na zamani wakati wa utumiaji wa mzani wa rula mtu ulikuwa ukipata vifurushi zaidi ya kumi. “Kinachotakiwa ni kupatikana kwa mizani au usimamizi wenye kuweza kudhibiti uhalali wa kilo na kama ikishindikana basi heri irudishwe mizani ya rula iliyokuwa imezoeleka,” anasema.

Afisa kilimo wa halmashauri ya wilaya ya Bariadi, Oswin Mlelwa anasema katika mizani 135 iliyokuwa ikitumiwa ilibainika mizani 35 ilikuwa imechakachuliwa na hivyo kuwapunja wakulima. Anawashauri wakulima kuchukua risti na kama kuna malalamiko inakuwa rahisi kujua wameuza kwa nani.

Anasema tatizo lingine katika mkoa mpya wa Simiyu ni kukosa wakala wa vipimo ili kukagua mizani mara kwa mara na kwamba wanapokuja mkoani humo huwa wametokea Shinyanga ambako pia walioko ni wachache. “Inasadikika kwamba wakulima wamekuwa wakiwafahamu baadhi ya wachakachuaji lakini hawatoi ushirikiano na kubaki kulalamika tu,” anasema.

Juma Chacha ambaye ni kaimu wakala wa vipimo kwa mkoa wa Shinyanga na Simiyu anasema kuwa halmashauri ya wilaya ya Meatu imefanikiwa kudhibiti uchakuachuaji wa mizani kwa kuweka mitego yao ili kuweza kubaini mizani iliyochezewa. Kadhalika anasema wakulima kupitia halmashauri hiyo walinunua jiwe la kilo 20 kwa gharama ya shilingi 80,000 na sasa wanasimamia wenyewe na sasa halmashauri inapata mapato ya kutosha tofauti na awali.

“Ilikuwa mtu akipeleka kilo100 anaibiwa hadi kilo 30 na wakulima wengi hawana elimu ya utambuzi wa mizani hizo za digitali kama zinasoma sawia. Akiuangalia mzani anaona kama unasoma sawa kumbe anaibiwa,” anasema Chacha

*Ni salama asilimia 99.99

foto
Mwandishi: Karren Masassy

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi