loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kilombero kuinua uchumi kwa kuimarisha ukusanyaji wa mapato

Hivyo ni wajibu kila halmashauri kuwa na vyanzo vya mapato vilivyo imara na vinavyoweza kusimamiwa vizuri ili kuziwezesha kutekeleza majukumu ya msingi ya kutoa huduma za jamii. Miongoni mwa huduma hizo za msingi ni pamoja na afya, elimu, miundombinu ya barabara, kilimo na huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama mijini na vijijini. Kilombero, ni kati ya halmashauri saba zilizopo mkoani Morogoro.

Ina watu 407,880 kulingana na takwimu ya sensa ya taifa ya watu na makazi ya mwaka 2012, kati ya hao wanaume ni 202,789 na wanawake 205,091 ambao wote wanahitaji kupatiwa huduma bora za kijamii. Hivyo makala haya yanaangalia jinsi halmashauri hiyo ilivyoweza kupata mafanikio katika ukusanyaji wa mapato yake ya ndani kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2007/2008 hadi kufikia Juni, 2014 na kuweza kuboresha huduma za kijamii.

Halmashauri zingine katika mkoa wa Morogoro ni Kilosa, Mvomero, Ulanga, Gairo , Manispaa ya Morogoro pamoja na Halmashauri ya wilaya ya Morogoro.

Mkuu wa wilaya ya Kilombero, Hassan Masala, anabainisha hayo katika taarifa ya wilaya hiyo kwa Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia alipoitembelea halmashauri hiyo na alielezwa namna iliyoweza kuongeza makusanyo ya ndani, ambapo katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 iliweka makisio ya makusanyo ya ndani ya kiasi cha shilingi bilioni 5.013.

Mkuu wa wilaya anasema halmashauri iliweza kukusanya shilingi bilioni 3.9 sawa na asilimia 78 .90, wakati katika mwaka wa fedha wa 2012/2013 ilikisia kukusanya mapato ya shilingi bilioni 3.9 , lakini ilikusanya kiasi cha shilingi bilioni 2.3 sawa na asilimia 65.39.

Hata hivyo anasema, mapato ya ndani yaliyopatikana katika bajeti ya fedha ya mwaka 2013/2014, kiasi cha shilingi milioni 710 zilitumika kwenye miradi ya maendeleo kama ununuzi wa trekta la kijiji cha Udagaji, ujenzi wa Ofisi ya Mamlaka ya Mji Mdogo Ifakara na Uanzishwaji wa kituo cha Televisheni na Redio ya Halmashauri.

Miradi mingine ya maendeleo iliyochangiwa na mapato ya ndani kwa mwaka huo ni ujenzi wa jengo la utawala la halmashauri, ujenzi wa choo katika geti la Mkamba, uzio wa dampo la Kiogosi na wodi kituo cha Afa Kibaoni kwa kiasi cha shilingi milioni 200. Katika bajeti ya 2014/2015, halmashauri ya wilaya imetenga shilingi bilioni 3.5 ili kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwa na kununua ‘grader’ kwa ajili ya matengenezo ya barabara za wilaya.

Pia Mkuu huyo wa wilaya anasema katika bajeti hiyo, kiasi kingine ni mchango wa asilimia 20 ni ya miradi ya vijiji, na asilimia 10 ni kwa ajili ya kuwakopesha wanawake na vijana.

“Ili kupunguza hali ya umasikini miongoni mwa wananchi wa wilaya ya Kilombero...wilaya imeendelea kutekeleza sera ya mikopo kwa vijana na wanawake ambao wamejiunga katika vikundi mbalimbali vya uzalishaji mali,” anasema Mkuu wa wilaya hiyo. Hivyo anasema, kuanzia mwaka wa fedha wa 2012/2013 hadi Juni 2014, vikundi 70 vya wanawake na vijana vilipatiwa mikopo yenye jumla ya shilingi milioni 94.5 na hadi sasa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 48.3 imerejeshwa.

“Wilaya inazidi kuhamashisha vijana na wanawake wajiunge katika vikundi vya uzalishaji mali ili iwe rahisi kwao kutumia fursa ya mikopo inayotolewa na mfuko wa wanawake na vijana, na pia kutoka taasisi mbalimbali za kifedha zilizopo wilayani,” anasisitiza Masala. Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Azimina Mbilinyi, anaweka wazi mikakati iliyofanikisha kuongeza mapato ya halmashauri ni pamoja na kuwepo kwa vyanzo vipya vya mapato vilivyobuniwa na ushirikiano wa pamoja wa wadau.

Hivyo anasema , mikakati mingine ya kuongeza mapato ya halmashauri ni kusimamia matumizi ya sheria ndogo za ukusanyaji wa mapato, kuboresha sheria ndogo iliyopo kwa kufanya marekebisho ya kuongeza vyanzo vingine vya kukusanya mapato. Hata hivyo anavitajaa vyanzo hivyo ni kama vile ushuru wa matunda, viungo na mazao ya bustani na mengineyo.

Mbali na hilo, mkakati mwingine ni kudhibiti mianya yote ya uvujishaji mapato ya halmashauri kwa kufanya ufuatiliaji wa karibu kwa watendaji ambao wanajukumu la kusimamia ukusanyaji wa mapato. Pia anasema suala lingine lililowekwa kipaumbele ni kutoa motisha kwa watumishi wanaokusanya mapato kwa kuwapatia vitendea kazi kama vile pikipiki na baiskeli ili kurahisisha kazi zao.

Mbali na mkakati wa kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani, halmashauri hiyo imeendelea kusimamia kwa karibu suala la upatikanaji wa huduma bora zikiwemo za maji safi na salama kwa wananchi. Hivyo anasema, halmashauri ikishirikiana na wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kama vile Shirika la Plan International, Caritas Mahenge – Ifakara na Serikali kuu imeweza kupunguza tatizo sugu la maji wilayani humo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, ambapo mpaka sasa inakadriwa kuwa asilimia 74 ya wakazi wa wilaya ya Kilombero wanapata maji safi na salama kutoka asilimia 59 .1 iliyokuwepo awali mwaka 2010.

“Ni matarajio yetu kuwa idadi ya wananchi wanaopata maji safi na salama itaongezeka mara baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa maji safi na mazingira unaotekelezwa katika vijiji 14 vilivyobahatika kuingizwa kwenye mpango huu,” anasema.

Hata hivyo anasema, miradi hiyo ilipangwa kukamilika Juni mwaka 2014, ambapo wastani wa watu 49,753 wananufaika na huduma ya maji safi na salama ambapo ni sawa na asilimia 12 na hivyo kufanya jumla ya wananchi watakaonufaoka na huduma hiyo kufikia asilimia 86.

Anavijata vijiji vilivyopata maji chini ya mpango huo ni Katurukila , Msolwa Steshani, Msufini, Mang’ula A na B ,Signal, Idete, Namawala, Mlimba A na B, Viwanja Sitini, Kamwene, Matema na Tanganyika Masagati. Kwa upande wao wananchi Kijiji cha Katurukila, Kata ya Sanje, wilayani Kilombero wanaonufaka na mradi wa maji safi na salama kwa nyakati tofauti wanalezea kuwa wamekombolewa kwa kuwepo kwa mradi huo.

Hata hivyo wanasema, kabla ya kupata mradi huo wa maji hayo, walikuwa wakitumia muda mwingi kusaka maji , jambo lilolokuwa linarudisha nyuma shughuli zao za uzalishaji mali hasa kilimo cha mpunga na mahindi. Naye Katibu wa Bodi ya Maji ya Kijiji hicho, Elizabeth Manduke anasema mradi huo ni moja ya mipango ya Serikali kuu ya kuvipatia maji safi na salama vijiji 10 kila halmashauri ya wilaya nchini.

Manduke anasema, mradi huo wa maji ya mserereko uliogharimu Sh milioni 278.7, ulianza kutekelezwa Septemba mwaka 2013 ulikamilishwa Februari mwaka huu (2014) na umeanza kutumia. “Mradi huu unawanufaisha wakazi 2,785 katika kijiji cha Katurukila kwa mujibu wa sensa ya taifa ya watu na makazi ya mwaka 2012,” anasema Katibu wa Bodi ya maji ya Kijiji hicho.

Kwa upande wake, Waziri Ghasia, alipopata fursa ya kuzungumza na watumishi wa kada mbalimbali wa halmashauri ya Kilombero, aliwapongeza kutokana na ufanisi wao katika ukusanyaji wa mapato ya ndani. Waziri huyo anasema, ukusanyaji mkubwa wa mapato ya ndani ni moja ya nyenzo ya kuiwezesha halmashauri kwenye utekelezaji wa miradi mipya sambamba na kukamilisha ya zamani ili kuwaletea wananchi maendeleo.

“Halmashauri nyingi nchini zinashindwa kufikia malengo ya makusanyo ya mapato yao ya ndani kutokana na baadhi ya wanasiasa wanawahubiria wananchi wao wasichangie shughuli za mandeleo ama kulipa ushuru, na watumishi kukosa uadilifu katika ukusanyaji wa mapato,” anasema.

Mbali na hayo, pia anasema suala la usimamizi hafifu wa ukusanyaji wa mapato na matumizi mabaya ni sababu nyingine zinazorudisha nyuma halmashauri nyingi kuweza kufikia malengo waliyojiwekea ya kukusanya mapato ya ndani yanayowezesha kuhudumia maendeleo ya wananchi wake kijamii na kiuchumi.

“Nimefurahishwa na ukusanyaji wa mapato, mko vizuri mmeonesha hapa asilimia ya makusanyo kuanzia mwaka wa fedha wa 2007/2008 mlikuwa asilimia 60,” anasema na kuongeza.

“Mmekuwa mkipanda kulingana na makisio yenu na makusanyo, pia mmewahikufikia hadi asilimia 96.20 na mwaka 2013/2014 ni asilimia 78.90,” anasema Waziri Ghasia. Hivyo anasema, halmashauri zinapokusanya mapato makubwa ya ndani zinakuwa na uwezo wa kupanga na kutekeleza mipango ya kimaendeleo iliyojiwekea na kutoa huduma bora kwa wananchi.

“MTU niliyefanya naye mahojiano alikuwa anafanya kazi kwenye ...

foto
Mwandishi: John Nditi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi