loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kinana: Hawa nao ni wenzetu

Kinana: Hawa nao ni wenzetu

Ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana imebainisha kwamba chama hicho bado kinapendwa na watu si kama watu wanavyodhani. Tathmini imeonesha kwamba katika maeneo ambayo CCM ilipoteza uwe ubunge au udiwani au ilikosa kura za urais, si kutokana na kwamba wapinzani ni imara sana, bali ni mikorogano ndani ya chama chenyewe.

Kinana ameona, kusikia na kuthibitisha kwamba mikorogano ndani ya CCM ilichangia kupoteza CCM kupoteza nafasi za udiwani na ubunge katika baadhi ya maeneo. Ni ukweli usiopingika baadhi ya wana-CCM kutokana na wagombea waliokuwa wakiwataka kushindwa kupitisha, waliamua kuwapigia kura wapinzani.

Maadui wa CCM walikuwa ndani ya chama chenyewe, baada ya kundi lenye nguvu ndani ya chama kumsimamisha mgombea ama udiwani au ubunge wasiyemtaka. Maeneo ambayo CCM iligalagazwa, ilitokana na ama baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Siasa, viongozi wa chama na makada, kumteua mwenzao na kumwacha mgombea aliyetakiwa na wanachama.

Hivyo kushindwa kwa chama kulitokana na migawanyiko au makundi ndani ya CCM, mengi kati yake hadi leo yapo, ndiyo yanayoendelea kukidhoofisha chama. Wagombea waliokuwa wakitakiwa na wanachama wapigwa chini, wakachukuliwa wagombea waliokuwa wakitakiwa na viongozi wa chama.

Ugomvi wa madaraka au ya nani asimame kugombea, yalikuwa chimbuko kubwa kupoteza majimbo baadhi nchini. Usimamishaji wa wagombea wasiotakiwa na wanachama, ulichangiwa na viongozi maslahi, ambayo waliwasimamisha wagombea ambao wanatoa fedha kwa lengo la kupata madaraka.

Kundi la wanachama itikadi, ambao walikuwa wakijua ukweli kuhusu mgombea gani anaweza kushinda jimbo, waliamua wengine kugeuka CCM nyakati za mchana na usiku waliungana na upinzani, wakapiga kura za chuki. Ubinafsi huo uliwafanya wagombea wa CCM wapoteze, kwa sababu waliungwa mkono kwa maneno lakini kura wakampigia mpinzani, kuwakomoa wagombea ambao hawawataki.

Katika maeneo hayo, mfumo wa tukose wote, ulitawala au wa kukomoana, umeinyima CCM ushindi katika majimbo mengi nchini. Kutokana na kumsimamisha mgombea ambaye hakubaliki na wanachama, ulikuwa sawa na mtindo wa kumwaga mboga, wanachama wakaamua kumwaga ugali ili mradi chama kikose ushindi, ili wajifunze.

Kinana amebainisha na kuwazungumzia wajumbe wa halmashauri kuu za CCM za wilaya kwamba, mahali pengi ambapo CCM ilipoteza ubunge au udiwani si kwamba wapinzani walikuwa imara, bali ni mikorogano ndani ya CCM. “Kushindwa kwa CCM katika kata au majimboni si kwamba Upinzani ulikuwa na nguvu kubwa kisiasa bali ni mikorogano iliyoibuka ndani ya chama,” anasema Kinana.

Mkoani Ruvuma katika majimbo ambayo wapinzani walishinda kata likiwamo la Songea Mjini, inatokana na baadhi ya wanachama wa CCM kupiga kura za chuki dhidi ya wagombea wa chama chao ambao walipendwa na viongozi wala si wanachama. Mkoani Mbeya, CCM ilipoteza majimbo ya Mbozi Magharibi na Mbeya Mjini, na kata kadha wa kadha, mtindo wa kusimamisha wagombea wasiokubalika, ulichangia kwa kiasi kikubwa kukosa majimbo na kata nyingine.

Mtindo wa kwamba viongozi wa chama wamemwaga mboga kwa kumsimamisha mgombea asiyeuzika na sisi tunamwaga ugali kwa kumpigia mpinzani, umekigawa chama, umetengeneza makundi na kukifanya kishindwe katika baadhi ya maeneo. Baadhi ya wana-CCM ambao walipinga mtindo wa kusimamisha wagombea wanaopendwa na viongozi badala na wanachama, walipigia kura upinzani.

Ubinafsi wa wenye mamlaka ya kuteua wagombea,kutokana na maslahi waliopata, ulikinyika Chama Cha Mapinduzi (CCM) ushindi katika baadhi ya majimbo na kata. Katika uchaguzi mkuu wa 2010, wagombea ambao walipendwa na wanachama, walikuwa wakikubalika, walishinda hata bila kutumia fedha nyingi kupata ushindi.

Baadhi ya maeneo ambayo CCM ilishindwa ilitokana na uwajibikaji mbovu wa viongozi wa Serikali ya CCM, baadhi yao si wanachama wa chama tawala. Katika maeneo ambayo baadhi ya watendaji si wapenzi wa CCM, Utendaji wake umekuwa mbovu kiasi cha kukwamisha maendeleo.

Baadhi ya watendaji hao kutokana na itikadi zao, wanawavuruga watendaji na kutekeleza sera wanazozijua wao wala si za CCM. Watendaji ambao wana itikadi zao, katika baadhi ya maeneo wana mchango mkubwa katika kukwamisha maendeleo, ili mwisho wa siku CCM ionekane haijatekeleza ilani yake.

Lakini pia wanataka kuonesha kwamba CCM imeshindwa kuisimamia Serikali, kumbe ni wao ambao wanakwamisha utekelezaji na ufanisi wa miradi mbalimbali. Baadhi ya watendaji ambao usiku wanavaa nguo za kijani kuonesha wana-CCM, usiku wanavaa magwanda ya upinzani na kukisaliti chama.

Halmashauri ambao baadhi ya watendaji wanatekeleza ilani ya vyama vingine, kumekuwa na mikorogano na utendaji wake unafifia katika maeneo hayo. Kinana anaonya kwamba watendaji ambao, wapo ndani ya Serikali, lakini wanatumia itikadi zao kukwamisha maendeleo ya Serikali ya CCM, chama kitawamlika na kuwabaini.

Lakini kukwama kwa maendeleo katika baadhi ya maeneo ni kampeni za chini chini zilizozinduliwa na baadhi ya wana-CCM. Wanachama hao wameanza kujipitisha kwenye kata au majimbo, kujinadi au kujitangaza na kugawa zawadi na kuwarubuni wanachama.

Wanafanya hivyo ili kuandaa mazingira, ili wakati utakapofika wa kuteua wagombea, basi waonekane wao wametangulia na hivyo wapate nafasi za kupitishwa. Katika majimbo mengi, tayari baadhi ya wana-CCM wanajipitisha kuwarubuni wananchi kwa takrima ili wakati ukifika wachaguliwe.

Mbaya zaidi wamekuwa wakipita na kuwachafua wabunge au madiwani waliopo madarakani, kitendo ambacho chama hakitabaki kimya. Kinana anaagiza, kwamba kamati za siasa na nidhamu zina wajibu mkubwa wa kufuatilia nyendo za watu hao, wakalishwe, waonywe na taarifa zao ziandikwe.

Vikao vya juu vya chama, Mkutano Mkuu, Halmashauri Kuu na Kamati Kuu vitakapokaa, watachambuliwa na kuenguliwa kugombea nafasi hizo. Kinana anasema, muda muafaka ukifika watapewa nafasi, lakini anayejipitisha na kuanza kuwavuruga watendaji au wabunge au madiwani waliopo sasa, chama kitamwadhibu.

Katika hali hiyo, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi anasema, baadhi ya watu wameanza kuzunguka majimboni, likiwamo jimbo la kwake, la Mbozi Mashariki, kitendo ambacho kinamfanya ashindwe kufanya kazi. Wengi wa watu wanaopita majimboni au kwenye kata saa hizi, wanawavuruga waliopo madarakani, wanashindwa kufanya kazi zao vizuri.

Mikorogano hiyo ndani ya chama na Serikali yake, inayojitokeza mfano wa kuchagua wagombea wanaopendwa na viongozi, watendaji kukihujumu chama na wana-CCM kujipitisha majimboni na katani kabla ya wakati, CCM imenoa panga, watakaofumwa watakiona.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi