loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kinana, Nape, Dk Migiro wameirudisha CCM relini

Wamezunguka katika mikoa na majimbo mbalimbali kurudishia chama mvuto wake, kwa kufanya mikutano ya ndani na hadhara zaidi ya 121 na kusafiri zaidi ya kilometa 6,000 na wamethubutu kushiriki shughuli za maendeleo, kutembelea viongozi waliosahauliwa na kuthubutu kutumia usafiri hatari ili mradi kuhakikisha chama kinahuishwa upya.

Miongoni mwa misafara ya Kinana ule wa siku 26, akianzia mikoani Mtwara, Ruvuma, Mbeya na kumalizia Njombe. Katika ziara hiyo, amefanya kazi kubwa ambayo haitasahaulika miongoni mwa wana-CCM kuanzia kwa mabalozi, halmashauri za chama hadi wenyeviti wa CCM mikoa na wapenda chama, mashabiki popote alipopita.

Viongozi wa mitaa, badala ya kumpokea na kula, kuzungumza nao walikuwa wakishangaa, ni kiongozi gani huyo wa chama anaweza kukaa kwenye mikeka, kula chakula na kunywa chai kwenye vikombe vya wazee wa kijijini.

Miongoni mwa watu walioshangaa kuthubutu kwa Kinana ni Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, wakati tukiwa kwenye meli ya Mv. Songea akasema, hawajawahi kumwona kiongozi aliyejishusha kutoka makao makuu ya CCM, Dodoma au makao madogo Lumumba, Dar es Salaam na kula chakula walichoandaa watu wa kawaida kabisa kama mabalozi.

Mwenyekiti Mwisho alishangaa mengi yakiwamo ya kushiriki kila kazi za maendeleo kwa vitendo, ama kujenga nyumba, kufyatua tofali, kuchimba mitaro, kupiga ripu nyumba, kulima, kujenga mabwawa na kazi nyingine nyingi.

Hata Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi katika kila mkutano alipotakiwa kuzungumza kabla ya Katibu Mkuu Kinana alionesha wazi kukongwa moyo na uthubutu wa kiongozi huyo kutaka kwa dhati kukirudisha chama kwenye reli.

Zambi mara zote amekiri hadharani kwamba hapo nyuma chama hakikuweka utaratibu mzuri wa kuwatembelea mabalozi na kushiriki kila walichokiandaa mbele yake, lakini awamu hii kimefanya hivyo.

Zambi bila kumung’unya maneno amesema, Kinana ni miongoni mwa mtendaji katika chama ambao wamedhamiria kwa thati kurudisha mvuto wa chama kwa kuwatembelea wanachama kwenye mitaji ya chama yaani matawini na kusikiliza kero zao na kuzitatua kwa kushiriki maisha yao.

Katika kampeni ya kukirudisha chama kwenye reli, Kinana na msafara wake, ukiachilia mbali kushiriki shughuli za maendeleo, jambo kubwa zaidi alithubutu kutumia usafiri ambao hatarishi ambao kwa muda mrefu wananchi wa maeneo husika walikuwa wakipigia kelele, akashiriki ili kuona kero zao.

Kinana alishiriki adha za kusafiri katika mto Ruhuhu kwa kutumia mtumbwi mdogo kwenda wilayani Ludewa katika Mkoa wa Njombe na kurudi kwa mtumbwi huo huo wilayani Nyasa katika Mkoa wa Ruvuma, kitendo hicho kiliwatoa machozi ya furaha wenyeji wa Ruhuhu.

Wananchi wa mpakani wanaotumia mto huo wa wilaya zote mbili wamekuwa katika adha ya kuvuka kwenye mto huo wenye mamba na viboko wengi, si kwamba hawana kivuko bali ni kikubwa mno kinafanya kazi miezi sita wakati wa masika kwenye maji mengi na kinasimama kwa miezi mingine sita wakati hakuna maji ya kutosha.

Hivyo, miezi sita wanatumia mitimbwi midogo ambayo mara ikitokea tufani inapinduka na kuua watu. Safari hiyo ya kwenda Ludewa na kurudi Nyasa akivuka mto Ruhuhu, kuliacha gumzo na simulizi miongoni mwa wakazi wa Lituhi, Nyasa mahali msafara ulipolala.

Wenyeji wa Mpanga wilayani Ludewa, walimshangaa kiongozi huyo kuthubutu kuvuka mto huo wenye mamba wengi kwa kutumia mtumbwi, wakati viongozi wengi wameshindwa.

Kama hilo halijatosha, Kinana alithubutu kushiriki usafiri wa majini katika Ziwa Nyasa kutoka katika Bandari ya Mbambabay, Nyasa hadi Bandari ya Itungi, Kyela, mkoani Mbeya. Safari hiyo ya saa 26, haikuwa nyepesi, lakini kwa wana CCM na wafuasi wa chama, hicho ilikijengea chama heshima kubwa.

Safari hiyo ya usiku mmoja kwa kiongozi huyo na msafara wake wa watu 38, uliwatoa machozi wakazi wa Nyasa waliokuwa wakimsindikiza kwa mitumbwi pembeni na kutangulia kwenye bandari inayofuata kumpokea walimwacha hadi anapoingia kwenye bandari za Wilaya ya Ludewa.

Wananchi wa mwambao mwa Ziwa Nyasa, kwenye bandari zote, walikesha wakimsubiri kumwona Kinana, kiongozi aliyethubutu kusafiri kwa meli ya Mv Songea, ambayo ni ya zamani, imechoka na kabla yake ilikuwa haifanyi safari kutokana na ubovu wake.

Alipanda meli hiyo iliyotoka matengenezo siku moja kabla yake. Katika safari hiyo, Kinana na msafara wake, walijichanganya na wasafiri wengine waliotumia meli hiyo kama si kuvaa fulana nyeusi za ‘Umoja ni Ushindi,’ ingekuwa vigumu kuwatofautisha. Safari hiyo imeandika historia kwa kiongozi huyo wa ngazi yake kutumia usafiri wa meli chakavu na isiyoaminika.

Angeweza kusafiri kwa magari lakini aliyaacha yazunguke bila abiria, lakini msafara wake ushiriki adha za abiria wanaotumia Ziwa Nyasa ambao wamekuwa wakililia meli kwa muda mrefu.

Kwa kusafiri huko, kulimpa nguvu ya kwenda kuhimiza utengenezaji wa meli tatu moja katika kila ziwa ambayo ni ahadi ya Rais Kikwete kwa ajili ya ziwa hilo, Tanganyika na Victoria.

Kitendo cha kusafiri kwa meli na kuingia asubuhi katika Bandari ya Itungi na asubuhi hiyo hiyo kuendelea na ziara kutembelea Wilaya na jimbo la Kyela la Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, kulionesha nia ya dhati ya kukirudishia chama mvuto wake.

Wanachama wa CCM wa Mkoa mzima wa Mbeya waliokusanyika katika eneo la Kiwira mahali ilipo bandari hiyo, walibaki midomo wazi wakishangaa Katibu Mkuu wa chama chao, aliyekuwa akishuka kwenye meli ya Mv Songea, ambayo haikuwa ikiaminika sana. Kitendo hicho kilionesha udhati wake, kwamba CCM imeamua kuwafuata wanachama wake, kusikiliza vilio vyao na kushiriki katika maisha yao.

Ameamua kukihuisha chama kama wengi walivyoamini kwamba chama ni kama samaki, ambaye mmoja akioza wote wameoza, bali kina watu waliodhaminia kukirudisha kwenye reli.

Mwenyekiti wa CCM Njombe, Deo Sanga, alitoa trekta kwa ajili ya vijana walioamua kujiunga katika vikundi kuondoa umasikini, kwa wakazi wa Makete na Wang’ingombe, ambako alikuwa akitembelea mara ya pili, walikuwa wakinong’ona kwamba sasa viongozi wa CCM wameamua kuimarisha chama hicho.

Kitendo cha kuamua kurudi jijini Dar es Salaama kwa usafiri wa treni ya Tazara kutoka Makambako, kilirudisha imani kwa wana-CCM katika mikoa aliyopita ya Njombe, Iringa, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.

Akiwa Mlimba kiongozi huyo pamoja na uchovu wa safari, alishuka na kuwasalimia na wana-CCM waliokusanyika mahali hapo wakimshangaa kutumia usafiri huo, wakijiuliza nini kilimfanya asafiri na usafiri huo, wakati angeweza kutumia usafiri wa barabara ambao ni wa uhakika.

Kuingia kwake Dar es Salaam asubuhi siku ya pili yake, viongozi na wanachama wa CCM waliokesha wakidhani angefika mapema usiku, ikawa usiku, ikawa asubuhi, kuliwapa hamasa ya kumsubiri hadi asubuhi kutokana na kitendo chake cha kuthubutu kutumia usafiri huo wakati angeweza kurudi kwa ndege au barabara.

Kushiriki kwake kusafiri kwa mtumbwi kwenye mto Ruhuhu, kusafiri kwa Mv Songea kutoka Mbambabay hadi Kyela katika Ziwa Nyasa na kutumia usafiri wa treni kutoka Makambako hadi Dar es Salaam, kumeonesha nia ya dhati ya kukirudishia chama mvuto lakini kukirudisha kwenye reli ya kushiriki maisha ya wananchi na kutatua kero zao.

Kinana amethubutu kushiriki maisha ya mabalozi katika wilaya zote alizotembelea, amezungumza na halmashauri za wilaya zote na kuzungumza na wananchi azma ya CCM kurudisha imani kwa wanachama wake.

Amekiri kwamba kuna wakati chama kilikwenda alijojo, kama anavyosema Zambi kilitoka nje ya reli, sasa Kinana anakirudisha kwa mtindo mpya wa kuiwajibisha Serikali.

Maneno ya Mwenyekiti wa CCM mkoani Ruvuma, Mwanzo kuhusu Kinana bado nayakumbuka, “Ametupa changamoto ya kukirudisha chama kwenye reli kwa kuwatembelea viongozi wa chama wa chini wakiwamo mabalozi, tulijisahau, sasa tumekumbushwa.”

MAKALA ya leo yanaangazia jamii ya ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi