loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

KIU ni mfano wa kuigwa na vyuo vingine

Kwa faida ya wasomaji wetu, KIU ni Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala, ambacho kina tawi lake hapa Tanzania lililopo Gongo la Mboto.

KIU imetangaza wazi bila kumung'unya maneno kwamba watatoa udhamini kwa wanafunzi 1,800 kuanzia mwaka huu wa masomo kwa kuwalipia nusu ada.

Sambamba na hatua hiyo, chuo hicho kimepunguza ada kwa masomo ya Jamii kutoka Sh milioni 2.8 za awali hadi Sh milioni 1.6. Mradi huu ambao umeelezwa kuwa ni endelevu, utagharimu chuo hicho Sh bilioni 2.5 kila mwaka.

Tunapenda kukipongeza kwa dhati chuo hicho kwa hatua madhubuti kama hizo, ilizoamua kuchukua kwa lengo la kuongeza wigo wa wasomi katika nchi yetu.

Hakuna ubishi kwamba hatua hii ni faraja kubwa kwa wazazi, walezi na wanafunzi husika na bila shaka kwa upande wa wanafunzi wataitumia fursa hii kusoma kwa bidii ili kukamilisha ndoto zao za kujipatia elimu ya juu.

Tanzania hivi sasa ina vyuo vikuu vipatavyo 19 vikiwemo vya umma, binafsi na mashirika ya dini. Kila chuo kina kiwango chake cha ada mbalimbali, zikiwemo za masomo na malazi.

Sote ni mashuhuda jinsi maelfu ya wanafunzi wanavyoshindwa kuendelea na masomo yao, kwa sababu hawakufanikiwa kupata ufadhili kutoka Bodi ya Mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu.

Tayari Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imeliona tatizo hilo la kila chuo kujipangia gharama zake kadiri kinavyoona. Badala yake wametoa mpango wa ada elekezi kwa vyuo vyote.

Hatua hiyo inasisitiza tu kwamba hali ya ada kwa elimu ya juu ni kubwa na hivyo hakuna njia mbadala, kama kweli tunataka watu wetu wengi kujiunga na masomo ya vyuo vikuu, hawana budi kupunguza ada hizo ili ziendane angalau na uhalisia wa kiuchumi tulionao wananchi wengi.

Ni matarajio yetu kwamba vyuo vikuu vingi hapa nchini, vitachukua hatua zinazofanana na KIU ili kuongeza wigo wa wanafunzi watakaopata nafasi ya kujiunga na ngazi hiyo ya elimu.

Kama KIU wanaweza, kwa nini wengine nao wasiige mfano huo mzuri ili kuwa na mfumo wa elimu endelevu kwa watu wetu? Hapa tunapenda kuwakumbusha wadau wote wa setka ya elimu, kwamba sekta hiyo siyo biashara ya moja kwa moja, bali kwa kiasi kikubwa ni huduma kwa jamii yetu kama huduma nyingine.

Ni vyema tukatambua kwamba siyo sahihi kuitumia sekta hiyo, kama njia moja wapo ya kujitajirisha. Wakati umefika sasa wa kuirejesha sekta hiyo katika mstari wake wa huduma zaidi na siyo biashara.

Wadau wote kwa ujumla wake wakiwemo wananchi, wizara na wamiliki wa vyuo tushikamane katika kubadili mtazamo huo hasi katika jamii yetu na mwisho wa siku kila upande utakuwa unanufaika inavyostahili.

RIPOTI ya 15 kuhusu uchumi wa Tanzania ya ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi